23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge Masele ampongeza Rais Magufuli

Na MWANDISHI WETU-SHINYANGA

MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Stephen Masele (CCM), amempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kazi anayoifanya ya kusimamia nidhamu ya fedha na watumishi wa umma, hali ambayo imesukuma kutekelezwa kwa miradi mingi ya maendeleo.

Masele ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), aliyasema hayo jana mjini hapa, katika ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo lake ambapo pia alizunguka na wananchi wa Kata ya Kolandoto.

Alisema kuwa kazi nzuri ambayo anaifanya Rais Dk. Magufuli ya kusimamia nidhamu ya fedha na watumishi wa umma, kazi yake imeonekana ambapo miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa, kitendo ambacho kimezidi kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM)  na kuwa na imani kwa wananchi.

Masele alisems kutokana na kazi nzuri inayofanywa  na mkuu huyo wa nchi Uchaguzi Mkuu mwaka 2020,  CCM itashinda kwa kishindo kama ilivyofanyika uchaguzi Serikali za mitaa mwaka 2019.

 “Nampongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia nidhamu ya fedha, na mimi mbunge wenu nitaendeleza kasi hii ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama anavyofanya rais wangu.

“Nadhani mnaiona Shinyanga jinsi ilivyobadilika kimaendeleo kwa sasa ndani ya miaka yangu tisa ya ubunge, ambapo kuna barabara za lami kila mtaa, pamoja na taa zake.

“Huduma za afya  nimeziboresha, elimu, maji yapo, ujenzi wa madaraja, na sasa hivi tumeshatenga tena kilomita 18 za ujenzi wa barabara mpya kwa kiwango cha lami tofauti na hizi kilomita 13 ambazo zimejengwa, yaani nataka Shinyanga uwe  mji wa kisasa ninaposema Shinyanga ni Paris ya Tanzania nina maana kubwa ya kuifanya shinyanga kuwa pahala pazuri pa kuishi kama ilivyo miji ya kisasa na uwezo huo ninao,” alisema Masele.

 Pamoja na hali hiyo aliahidi kuendelea kumalizia baadhi ya ahadi zake ambazo amebakiza kwenye baadhi ya maeneo, huku akitoa mifuko ya Saruji 150 ili kumalizia majengo ya ujenzi wa Zahanati za Mwanubi, ambapo wamepatiwa saruji mifuko 100, Mwamagunguli  mifuko 50 ambazo zote ni za Kata ya Kolandoto mjini hapa.

Nao baadhi ya wananchi wa Kata hiyo ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga akiwemo Naimani Ngeleja, wamempongeza mbunge Masele kwa kazi nzuri ambayo ameifanya kwenye uongozi wake, ikiwa ahadi nyingi amezitekeleza huku wakiomba awasaidie kupeleka huduma ya umeme wa REA kwenye baadhi ya vijiji ambavyo havijapitiwa na mradi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles