24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mbaroni kwa kuweka juisi ya tende viagra

MWANDISHI WETU-ZANZIBAR

MAMLAKA ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA), imewakamata watu wawili kwa tuhuma za kuuza juisi ya tende iliyochanganywa na dawa ya kuongeza nguvu za kiume inayotambulika kwa jina la ‘4G’ – viagra.

Juisi hiyo ya tende inadaiwa kuchanganywa na viagra pamoja na mchanganyiko wa dawa nyingine mbalimbali na kuuzwa katika eneo la Fuoni, Kiembesamaki, Mwanakwerekwe na Magari ya mawe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Unguja, Kaimu Mkurugenzi wa ZFDA, Nassir Ali Buheti, alisema kitendo kilichofanywa na watuhumiwa hao si cha kibinadamu kwani kinaweza kuleta madhara kwa afya za binadamu.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Hamid Hemed Salum (39) na Saidi Hemed Salum (40), ambao wamekuwa wakiuza juisi hiyo kwa watu mbalimbali kisiwani Unguja.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio Fuoni, Buheti alisema kitendo kilichofanywa na watu hao si cha kibinadamu kwani dawa walizochanganya kwa kawaida huwa na utaratibu maalumu na hutolewa kwa aina ya watu si ya kuchanganya kwenye juisi ili kuvutia wateja wao kama njia ya kuongeza nguvu za kiume.

“Walichofanya ni jambo la hatari kwa afya ya binadamu, lengo lao ni kuwavutia watu kuongeza nguvu za kiume, kumbe wanachanganya na dawa hizi wanaziita ‘4G kifurushi cha wiki’, pia hawana kibali kwa upande wa chakula. Na aina ya dawa wanazoziuza zinatakiwa kutolewa kwa cheti maalumu,” alisema Buhetri.

Wakizungumza wakati wakihojiwa, walikiri kuchanganya juisi ya tende na dawa hizo kuwavutia wateja, hasa wanaume ambao hupenda kunywa juisi hiyo.

Mmoja wa watuhumiwa hao, Said Salum, alisema kuwa dawa hizo huzichukua katika maduka la dawa mbalimbali na kuzichanganya katika juisi hiyo ingawa awali aliuliza kwa mamlaka husika kuhusu kuuza dawa hizo akajibiwa kuwa hawana utaratibu wa kuwaruhusu kuuza dawa hizo.

“Biashara tumeifanya takribani miezi sita na tulikuwa tukitumia gari aina ya Spacio,” alisema Salum.

Baada ya mahojiano hayo, watuhumiwa hao walipelekwa Kituo cha Polisi Fuoni kwa taratibu za kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles