ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM
MAJAJI, watumishi wa mahakama na wanafamilia, wameendelea kukusanyika nyumbani kwa marehemu Jaji Projestus Rugazia kuomboleza kifo chake.
Jaji Rugazia aliripotiwa kufariki dunia Agosti 4, akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Jana, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande walikuwa miongoni mwa viongozi walioungana na wanafamilia kutoa pole ya msiba huo, nyumbani kwake Kinondoni, Dar es Salaam.
Akizungumzia taratibu za msiba huo, mratibu wa mazishi ya jaji huyo, Charles Gabikwa, alisema kila kitu kinaendelea kama kilivyopangwa, japokuwa ni mapema sana kwa msemaji wa familia kuzungumza lolote.
Alisema kutokana na utaratibu ambao hadi sasa unaratibiwa na Ofisi ya Mahakama, mwili wa marehemu utawasilishwa nyumbani leo jioni, kisha kufanyiwa misa maalumu kesho Jumatano, na baadaye utasafirishwa kwa maziko Alhamisi.
“Taratibu zote zinaendelea vizuri, tunatarajia mwili wa marehemu utasafirishwa kwa ndege kwenda Kagera kuhifadhiwa baada ya taratibu zote za ibada na maandalizi kukamilika,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama Kuu ya Tanzania, iliyotolewa juzi, Jaji mstaafu Rugazia alifariki dunia alfajiri ya kuamkia Agosti 4, akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Taarifa hiyo kupitia tovuti ya Mahakama Kuu ya Tanzania ilieleza kuwa Jaji Rugazia alizaliwa Agosti 28, 1954 mkoani Kagera na alianza kazi rasmi Januari 1, 1983 kama hakimu mkazi.
Aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Machi 28, 2003 na alistaafu rasmi Agosti 28, 2016 akitokea Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi.
Taarifahiyo ilieleza kuwa Mahakama ya Tanzania imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo chake.