23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mbaroni kwa kukutwa na magogo ya sh milioni 383

 KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

SERIKALI imemfikisha mahakamani mfanyabiashara, Edgael Lema (43) akikabiliwa na mashtaka nane ikiwemo kukutwa na kontena 18 za magogo yenye thamani ya Sh milioni 383.

Mfanyabiashara huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Vicky Mwaikambo.

Wakili wa Serikali Mwamdamizi, Maternus Marandu, akimsomea mashtaka alidai mshtakiwa ambaye ni Mkazi wa Goba anadaiwa kuongoza genge la uhalifu, kusafirisha magogo, kugushi, kutoa nyaraka za uongo, kukwepa kodi na utakatishaji wa fedha.

Marandu alidai katika shtaka la kwanza kati ya Novemba 2015 na Januari 2016 maeneo yasiyojulikana nchini Tanzania, mshtakiwa akiwa na watu wengine ambao hawapo mahakamani hapo, walijipanga kuongoza genge la uhalifu huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Katika kosa la pili kati ya Novemba 2015 na Januari 2016 maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo akiwa na watu wengine ambao hawapo mahakamani wanadaiwa walisafirisha kontena 18 yenye vipande 5,296 vya magogo aina ya mkurungu yenye thamani ya Sh 383,140, 840 ambazo ni mali ya Tanzania bila ya kupewa kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Maliasili.

Shtaka la tatu na la nne ni la kugushi ambapo kati ya Mei 14 mwaka 2015 na Machi 16 mwaka 2015 maeneo yasiyojulikana nchini Tanzania, mshtakiwa huyo akiwa na watu wengine ambao hawapo mahakamani wanadaiwa kutengeneza nyaraka za uongo wakijaribu kuonyesha kuwa imetolewa na ofisi ya Serikali ya Zambia huku wakijua si kweli.

Katika shtaka la tano na sita inadaiwa tarehe isiyojulikana makao makuu ya Bandari ya Dar es Salaam, mshtakiwa  akiwa na watu wengine ambao hawapo mahakamani wakijua ni udanganyifu walitoa nyaraka za uongo kwenye ofisi hiyo wakionyesha nyaraka hizo zimetolewa na ofisi ya Serikali ya Zambia huku wakijua si kweli.

“Shtaka la saba inadaiwa kati ya Novemba 2015 na Januari 2016 maeneo ya Jiji la Dar es Salaam mshtakiwa akiwa na nia ya kukwepa kodi alitoa nyaraka za uongo ili kukwepa kulipa kodi ya Sh 383, 140, 840 huku akijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

“Shtaka la mwisho kati ya Novemba 2015 na Januari 2016 jijini Dar es Salaam mshtakiwa anadaiwa kujipatia Sh 383, 140, 840 huku akijua fedha hizo zilikuwa zimetokana na uhalifu wa kukwepa kulipa kodi,”alidai.

Wakili Marandu alidai upelelezi haujakamilika anaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles