31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mawazo tofauti safari ya Dodoma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

FLORIAN MASINDE Na NORA DAMIANI – DAR ES SALAAM

SERIKALI imewataka mawaziri na watendaji wote serikalini kuhakikisha ifikapo Septemba, mwaka huu, wawe wamehamia mkoani Dodoma kama ilivyoagizwa na Rais Dk. John Magufuli.

Taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata Dar es Salaam jana, zinasema tayari Serikali imetoa waraka kwenda kwa wakuu wa idara na vitengo kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma.

“Utekelezaji huu, ni agizo lililotolewa na Rais Dk. John Magufuli mwishoni mwa wiki wakati akikabidhiwa rasmi nafasi ya uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Rais Magufuli alielekeza kabla ya mwaka 2020 makao makuu ya Serikali yawe yamehamia Dodoma.

“Pia maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyoyatoa juzi kuwa mawaziri na watendaji wa wizara zote wawe wamehamia Dodoma ifikapo Septemba mwaka huu, hivyo basi kwa dokezo hili unaelekezwa kuanza maandalizi ya kuhamia huko,” ilisema sehemu ya waraka huo.

PROFESA MOSHI

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, aliishauri Serikali isikurupuke kuhamia Dodoma kwa sababu  katika bajeti ya mwaka 2016/17, hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya mpango huo.

“Kuhamia Dodoma ni jambo zuri, tunategemea linaweza likafanyika kwa sababu rais tuliyenaye ni mtu ‘commited’ (yuko makini), lakini lazima pawepo na maandalizi ya kutosha, hivyo viongozi wa chini wasikurupuke.

“Kuna gharama nyingi ambazo hazikuainishwa katika bajeti hii, lazima bajeti ijayo itenge fedha,” alisema Profesa Moshi.

TUCTA

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholas Mgaya, alisema mpango huo ni mzuri, unakwenda sambamba na falsafa ya Serikali ya kubana matumizi.

Alisema Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa, hasa wakati wa vikao vya Bunge, kama kutoa wafanyakazi na magari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

“Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliposema tuhamie Dodoma, wenzetu wa Nigeria na Malawi walikuja nchini kujifunza na wamefanikiwa kuhamia katika miji ya Abuja (Nigeria) na Lilongwe (Malawi), lakini sisi huku imekuwa ni danadana tu.

“Wakati wa sherehe za wafanyakazi mwaka huu (Mei Mosi), tulimkumbusha Rais Magufuli, tunashukuru ameanza taratibu za kuhamia,” alisema Mgaya.

PROFESA MPANGALA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema Dodoma ni katikati ya Tanzania, hivyo hatua ya kuhamia huko itasaidia watu wa kanda za mashariki, magharibi, kaskazini na nyanda za juu kusini kupata mahitaji muhimu.

“Huu si mpango mpya kwa sababu uamuzi ulifanywa tangu mwaka 1973, utekelezaji wake umekuwa wa kulegalega, jambo jema ni kwamba Serikali ya sasa inaonekana imedhamiria kutekeleza azimio hilo,” alisema Profesa Mpangala.

PROFESA BAREGU

Mtaalamu wa masuala ya sayansi ya siasa na uhusiano, Profesa Mwesiga Baregu, akizungumzia hatua hiyo, alisema ni uamuzi ambao ulikuwapo miaka 20 iliyopita, lakini ulishindikana kutekelezeka.

“Kimsingi kinachotakiwa sasa ni kuonyesha kama kuna sababu za msingi kuhamia Dodoma na ni kipaumbele kuliko vingine kulingana na hali ya kiuchumi wa nchi, na inapaswa kurejea na kuona kama vikwazo vilivyosababisha kukwama kwa uamuzi huo awali vimeondolewa, tusije kuwa watumwa wa maamuzi yetu wenyewe,” alisema Profesa Baregu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

KATABARO

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk. Jovita Katabaro, alipongeza uamuzi huo na kusema Serikali imeweza kuthubutu.

Alisema kuna wataalamu wengi waliandika juu ya Serikali kuhamia Dodoma na kuelezea faida za uamuzi huo, kwani mkoa huo ni muhimu na wa kihistoria, ndiyo katikati ya nchi ya Tanzania.

Alisema ujenzi wa ofisi na nyumba za watumishi unaweza kufanywa taratibu na kwa muda mfupi kwa kushirikisha taasisi mbalimbali na mashirika kama Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

MCHUNGAJI MSIGWA

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema uamuzi huo ni mzuri, lakini ana wasiwasi na utekelezaji wake.
Alisema kuhamisha wizara kama ya Nishati na Madini, Serikali inahitaji kujipanga zaidi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles