23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Mawaziri watano wachunguzwa kwa ufisadi Kenya

NAIROBI, KENYA

RAIS Uhuru Kenyatta juzi alijitenga na mawaziri wafisadi wakiwamo watano wanaochunguzwa, akisema watakaopatikana na makosa wabebe misalaba yao kwa kufungwa gerezani na mali zao kutaifishwa.

Akihutubia akiwa ziarani Kaunti ya Kisii, Rais alisema: “Wezi wa mali ya umma hawapaswi kuhusisha jamii zao kwa maovu yao. Kila mtu abebe msalaba wake.”

Hii ni kuhusiana na uchunguzi unaoendelea ukilenga takriban mawaziri watano kuhusu madai ya kula hongo kutoka kwa kampuni zinazopewa tenda katika wizara zao.

Duru zinadokeza kuwa Rais Kenyatta anasubiri ripoti ya uchunguzi unaoendeshwa na Idara ya Upelelezi (DCI) chini ya George Kinoti na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inayoongozwa na Twalib Mbarak kuhusu mawaziri hao kabla ya kuchukua hatua.

Maafisa wa wa EACC walisema uchunguzi huo pia unahusisha magavana kadhaa wa sasa na wa zamani.

Waziri wa Utalii, Najib Balala tayari amepewa mwito wa kukutana na maafisa wa EACC kuhusu madai ya ufisadi katika wizara yake.

Mwenzake wa Fedha, Henry Rotich alihojiwa Jumatatu wiki hii katika afisi ya DCI akihusishwa na kashfa ya ujenzi wa mabwawa mawili yaliyogharimu Sh bilioni 65 za Kenya sawa na Sh trilioni 1.3 za Tanzania.

Ujenzi wa mabwawa hayo, Arror na Kamwarer, katika eneo la Keiyo Kusini, Kaunti ya Elgeyo Marakwet umekwama licha ya serikali kuwekeza mabilioni ya fedha.

Uchunguzi umebaini kuwa tayari maafisa wa EACC na wale wa DCI wamepiga kambi nchini Italia kuchunguza utoaji kandarasi zenye utata za ujenzi wa mabwawa hayo.

Kampuni ya CMC di Ravenna, yenye makao yake makuu nchini Italia, imepewa kandarasi ya kujenga bwawa la Arror kwa Sh bilioni 38.5 na la Kimwarer kwa Sh bilioni 28.

Jumatatu iliyopita, EACC ilikuwa imemwandikia Waziri Balala ikimtaka afike ofisini kuhusiana na sakata la Sh milioni 100 za hapa sawa na Sh bilioni 2.2 za Tanzania zilizolipwa na wizara yake kwa kampuni ya American Society of Travel Agents (ASTA), kutangaza utalii wa Kenya mwaka 2017.

Tayari aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Utalii, Fatuma Hirsi pamoja na maafisa wengine wakuu wa wizara hiyo wamefika mbele ya EACC.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, Waziri Balala amehusishwa na kashfa hiyo baada ya stakabadhi kuonyesha kuwa alikuwa anawasiliana kila mara na maafisa wa ASTA walioko Kenya.

Naye Waziri wa Elimu, Amina Mohammed anatarajiwa kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Elimu, kujibu madai ya ufisadi katika usambazaji wa vitabu katika shule za umma nchini.

Amina anatarajiwa kutoa maelezo kuhusu usambazaji wa vitabu vingi kupita kiasi katika shule za umma, hatua ambayo inashukiwa kunufaisha baadhi ya maafisa katika wizara yake na wachapishaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles