22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, June 22, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAKILI WACHEMSHA BONGO KESI YA LEMA

Na JANETH MUSHI  -ARUSHA


pg-4

SAKATA la dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), limeendelea kuchemsha  bongo za mawakili wa pande zote mbili baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutoa uamuzi kuwa mbunge huyo ana haki ya kukata rufaa.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya mawakili wa Serikali kuwasilisha hoja za kisheria za pingamizi Novemba 17, mwaka huu, wakipinga Mahakama Kuu kusikiliza maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na mawakili wa Lema.

Awali kabla ya kutoa uamuzi huo jana mjini hapa, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Jaji Sekela Moshi, alilazimika kuwaita mawakili ndani (chamber court), hata hivyo kutokana na wingi wa watu, alilazimika kulipeleka shauri hilo mahakama ya wazi.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Moshi alikubaliana na hoja ya Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, kuwa mshtakiwa alitakiwa atumie haki yake kukata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama ya chini badala ya kuiomba Mahakama Kuu ifanye mapitio ya majalada ya kesi zinazomkabili.

Jaji Moshi alikubaliana na hoja ya pili ya Wakili Kadushi, aliyedai maombi ya Lema hayakuwa yamekidhi matakwa ya kisheria chini ya kifungu 359 (1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Kifungu hicho kinaelekeza mtu asiporidhika na uamuzi wa mahakama ya chini, anatakiwa kukata rufaa Mahakama Kuu.

“Wakili Kadushi alidai mshtakiwa hajaonyesha chochote kitakachohalalisha mahakama ifanye marejeo, huku Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, akisema mshtakiwa asingeweza kukata rufaa kwa sababu amri iliyotolewa mahakama ya chini haiwezi kukatiwa rufaa,” alisema Jaji Moshi akinukuu hoja zilizotolewa na mawakili hao.

Jaji Moshi aliendelea kueleza kwamba uamuzi wa mahakama ya chini unaolalamikiwa unaangukia kuanzia kifungu 148 hadi 160 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Kifungu 161 cha sheria hiyo hapo juu, kinaelezea uamuzi unaotolewa chini ya vifungu hivyo ambavyo vinashughulikia dhamana, kuwa vinaweza kukatiwa rufaa.

“Nimetilia maanani hoja hizi, naona ni wazi kwamba maombi haya yanaweza kukatiwa rufaa na haki ya kukata rufaa haiondoi haki ya marejeo. Pande zote mbili sheria inataka mtu ambaye hajaridhika na uamuzi akate rufaa au atoe sababu ya kuifanya mahakama ifanye marejeo,” alisema Jaji Moshi na kuongeza:

“Nilivyoangalia kwa kuwa vifungu hivyo vinaweza kukatiwa rufaa, mshtakiwa alitakiwa atumie haki yake kukata rufaa. Nakataa ombi la kufanya marejeo ambayo mahakama iliyafungua baada ya kupitia malalamiko ya Lema, nayafuta na ninaamuru hivyo,” alisema.

Jaji Moshi aliendelea kusema kuwa mahakama hiyo iliwaita wadaawa wa pande zote mbili Novemba 17, mwaka huu, ambapo hoja ya kwanza ya mawakili wa Serikali ilikuwa ni mahakama hiyo haiwezi kufanya marejeo au masahihisho ya mwenendo wa kesi ya mahakama ya chini.

Alikataa hoja hiyo ambapo mawakili wa Serikali walidai kifungu 372 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambacho kinaipa Mahakama Kuu kufanya mapitio ya mashauri ya kesi za mahakama za chini, baada ya mabadiliko ya kisheria yaliyofanyika mwaka 2002

yaliondoa haki za pande zozote katika kesi za jinai, kuomba rufaa au mapitio ya uamuzi mdogo uliofanywa katika mahakama za mahakimu nchini.

Mawakili hao walidai kwa mujibu wa kifungu 43(2) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu, maombi hayo yanakinzana na kifungu hicho kwani uamuzi huo mdogo unaopingwa na mawakili wa Lema haujamaliza shauri la jinai katika mahakama ya chini.

“Naona hoja ya kuwa mshtakiwa angezingatia kifungu cha 43(2) ni hoja ambayo si sahihi, sitaenda kuzungumzia kifungu hicho. Hivyo hoja hiyo siikubali na naitupilia mbali, na nimetilia maanani hoja za pande zote kwani mahakama ndiyo iliwaita ili waje wafafanue malalamiko na ijiridhishe iwapo itafanya marejeo au la,” alifafanua Jaji Moshi.

Jana Serikali iliwakilishwa na Wakili Mwandamizi, Matenus Marandu akisaidiana na Elizabeth Swai huku Lema akitetewa na Wakili Kibatala, akishirikiana na Adam Jabir, Sheck Mfinanga na Faraji Mangula.

Akizungumzia uamuzi huo, Kibatala alidai kuwa wanataka kukata rufaa kama walivyoelekezwa na mahakama chini ya hati ya kiapo.

Jalada la maombi hayo lilifunguliwa na Mahakama Kuu chini ya kifungu cha 372 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, baada kupokea malalamiko kutoka kwa mshtakiwa kupitia mawakili wake, ili iweze kujiridhisha na uamuzi uliolalamikiwa.

Kutokana na hatua hiyo, mawakili wa Serikali waliweka pingamizi za awali wakipinga Mahakama Kuu kusikiliza maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na mshtakiwa.

Katika maombi hayo, Lema kupitia mawakili wake, waliiomba Mahakama Kuu ifanye mapitio ya majalada ya kesi za jinai namba 440 na 441 ya mwaka huu, ambako anakabiliwa na makosa ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Mawakili hao wa Lema waliomba maombi hayo kutokana na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Desderi Kamugisha, aliyesoma uamuzi uliokuwa na kurasa 22 hivi karibuni, kusema kuwa anamwachia Lema kwa dhamana kwa masharti atakayopewa na mahakama hiyo.

Hata hivyo, kabla hajakamilisha uamuzi huo, akiwa katika ukurasa wa 21 kati ya 22, mawakili wa Serikali walisimama na kudai Serikali inakusudia kukata rufaa juu ya uamuzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles