27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

KATIBA INAYOPENDEKEZWA INASUBIRIWA KWA HAMU

katiba-mpya-2

BADO Watanzania wanasubiri kwa hamu kuipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa.

 Jumapili iliyopita JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA) limemshauri Rais Dk. John Magufuli kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kukamilisha mchakato wa Katiba mpya.

Vilevile limeishauri Serikali kutekeleza ahadi yake iliyoitoa kwenye mkutano wa Kimataifa wa Universal Period Review Mechanism (UPR), Mei 2016 Geneva, Uswisi.

Katika mkutano huo aliahidi kupitisha Katiba mpya mapema iwezekanavyo. Ahadi hiyo ya Serikali ilitolewa wakati wa kuwasilisha hali ya haki za binadamu Tanzania chini ya mpango huo.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Rais Dk. Magufuli hakuwa mgombea binafsi bali alipitia kwenye chama cha siasa cha CCM ambacho kilikuwa na Ilani yake, hivyo anapaswa kuitekeleza bila vikwazo.

Kwamba kwa kuwa CCM iliwaahidi wananchi ambao ndiyo waliompigia kura Rais Dk. Magufuli, litakuwa ni jambo jema kutimiza ahadi hiyo kwa faida ya Taifa.

Huu ni mwendelezo wa mchakato mrefu ambao umekwisha kufanyika tayari yapata karibu miaka mitatu sasa. Mwaka 2013 ulikuwa wa mvutano kati ya vyama vya upinzani na chama tawala, CCM, kuhusu aina ya Katiba mpya itakayoratibu maisha ya Watanzania kwa miaka mingi ijayo.

Tangu Bunge Maalumu la Katiba lilipoanza kikao chake mjini Dodoma Februari 18, 2013, liligeuzwa kuwa mkusanyiko wa watu wasio na mwelekeo na ambao hawakuonekana kujua tofauti kati ya ukumbi wa Bunge na vilabu vya pombe!

Lilikuwa Bunge la matusi kwenda mbele, na hakuna kiongozi yeyote wa ngazi ya juu aliyesimama kukemea mwenendo huo wa kishetani!

Wajumbe wa Bunge hilo walieendelea kuvutana, kukejeliana, kukashifiana na hata kutukanana matusi ya nguoni na kufanya siasa badala kutumia muda mwingi kuangalia njia bora ya kupata Katiba mpya kwa pamoja.

Tunasema kuwa hii haikuwa sahihi, ulikuwa ni uhuni uliokuwa unaelekea kulipasua Taifa moja kwa moja. Wajumbe wanaounda Ukawa hatimaye walilisusia Bunge hilo kabla ya Katiba Inayopendekezwa kutolewa bila kuwapo kwao na kwa maridhiano!

Mara kadhaa kupitia safu hii tumekuwa tukisisitiza kuwa Katiba ya nchi hupatikana kwa maridhiano na njia za wazi zisizo na ila pamoja na hila. Bila haya, katu Katiba haipatikani, na ikipatikana itakuwa Katiba inayofusha moshi!

Tunasema kuwa kujaribu kupata Katiba kwa hila na ila, na kwa shinikizo au kwa kulazimisha, Taifa litavunjika vipande vipande tu!

Tunasema hii isiruhusiwe, hata wakati ukifika wa kuipigia kura ya maoni Katiba Iliyopendekezwa. Kwa kujiepusha na ila na hila, tutakuwa tunaweka ithibati na kuchagiza maendeleo chanya kwa nchi yetu kwa miaka mingi ijayo.

Kwa hiyo hatuna budi kukumbusha kuwa Katiba Inayopendekezwa ilipitishwa kwa mbinu chafu, bila kuwapo kwa maridhiano kati ya wajumbe wa CCM na Ukawa.

Aidha, mambo mengi ya msingi ambayo watu walipendekeza yaliondolewa ambayo hayaleti tija kwa ustawi wa nchi yetu.

Tunasema kuna haja ya kuangalia upya kurejesha kwenye Katiba Inayopendekezwa yale ambayo yanaipa nchi manufaa na tija kwa maendeleo yake na kuipa heshima Katiba mpya itakayopatikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles