29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

WAFANYAKAZI WAJIPANGA KUMNG’OA KATIBU MKUU TUCTA

DAR ES SALAAM


pictuctasecretary

WAGOMBEA wanane kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi, wamejitokeza kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) inayoshikiliwa na Nicolaus Mgaya.

Katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho mkoani Dodoma, mchuano mkali katika nafasi hiyo unatarajiwa kuwa kati ya Yahaya Msigwa kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) na Mgaya ambaye anatetea nafasi yake.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya shirikisho hilo, kimelieleza MTANZANIA kuwa Mgaya ambaye ameshikilia nafasi hiyo kwa vipindi viwili mfululizo, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Msigwa ambaye ni mara yake ya kwanza kuingia katika kinyang’anyiro hicho.

Hoja inayojengwa kwamba inaweza kuwa kikwazo kwa Mgaya ni umri. Kwa mujibu wa Katiba ya TUCTA kiongozi anatakiwa asiwe na umri wa miaka 60.

“Hoja ya umri iliwahi kumwondoa Rais wa TUCTA wakati huo, Omar Ayub, baada ya hoja iliyoletwa na Mgaya mwenyewe katika kikao cha kamati tendaji, lakini tunashangaa kanuni hiyo yeye hataki itumike,” kilisema chanzo chetu.

Hii ni mara ya pili kwa Mgaya kuwania nafasi hiyo. Kwa mara ya kwanza alichaguliwa mwaka 2011  baada ya kushikilia nafasi ya Naibu Katibu Mkuu kwa vipindi viwili.

Chanzo chetu kinasema baadhi ya wanachama wanaliona shirikisho hilo limekosa nguvu ya kuwatetea na kuwaunganisha wanachama ili wawe na sauti moja ya kudai masilahi yao, hasa baada ya katibu mkuu huyo kugombea ubunge wa Muheza kupitia CCM na kuangushwa kwenye kura za maoni jambo ambalo pia linaweza kuwa kikwazo kurudi kwenye kiti chake.

Aidha kuyumba kwa mitaji ya mifuko ya hifadhi ya jamii kunatajwa kuwa ni kutokana na TUCTA kutokuwa imara kusimama kidete kuiambia Serikali, kwamba fedha hizo ni za wafanyakazi, hivyo zisikopeshwe wala kuingizwa katika miradi isiyokuwa na tija.

“Leo hii walimu waliostaafu tangu Juni mwaka jana wanadai zaidi ya Sh bilioni 230 kutoka Mfuko wa PSPF ambao hawajapeleka pensheni zao, tulitarajia TUCTA ilisimamie hili kwa sababu ndiyo kazi yake kuhakikisha masilahi ya wafanyakazi yanalindwa.

“Lakini shirikisho limekosa kabisa nguvu za kuikosoa Serikali, kibaya zaidi limeshindwa kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo sasa inayumba,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.

Uchaguzi wa TUCTA unafanyika kila baada ya miaka sita kuchagua viongozi mbalimbali watakaowakilisha vyama vyao kwenye chama shiriki pamoja na kupanga mikakati ya kutetea masilahi ya wafanyakazi katika nyanja mbalimbali.

Akizungumzia uchaguzi huo, Mgaya hakutaka kuingia kwa undani kuzungumzia ushindani uliopo.

Kuhusu wingi wa wagombea wanaotaka kumwangusha katika uchaguzi huo, Mgaya alisema kuwa, amejipanga kutetea nafasi yake licha ya watu wengi kuwania nafasi hiyo.

“Wakati naingia madarakani 2010, nilikuta wafanyakazi wanapata kima cha chini cha Sh 250,000, lakini nilipotangaza mgomo na maandamano, Serikali iliongeza mshahara hadi Sh 300,000,” alisema.

Hata hivyo alikiri kwamba bado kima hicho cha chini kwa sasa hakitoshi kulingana na hali halisi ya maisha, hivyo anayo nafasi ya kukaa na kuzungumza na Serikali ili kurekebisha mshahara huo.

Uchaguzi huo ambao unatarajiwa kufanyika kesho Mkoani Dodoma mpaka sasa zaidi ya watu 316 wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Shirikisho hilo.

Mbali na nafasi ya ukatibu mkuu, nyingine zinazowaniwa ni ya rais yenye wagombe tisa, makamu rais (30) na naibu katibu mkuu ikiwaniwa na watu 26.

Nafasi nyingine ni ya mtunza hazina, mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake, makamu, vijana, makamu mwenyekiti na nafasi ya wadhamini.

 

MGAYA NA JK

Mwaka 2010, Mgaya aliwahi kuingia kwenye mgogoro na Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, baada ya kutangaza kufanyika kwa maandamano ya wafanyakazi nchi nzima kwa madai kwamba Serikali imeshindwa kusikiliza kero zao ikiwa ni pamoja na kushindwa kuongeza kima cha chini hadi kufikia Sh 350,000 pamoja na kupunguzwa kwa kodi hadi kufikia tarakimu moja.

Baada ya kutangaza mgomo huo, Rais Kikwete aliibuka na kuponda hatua hiyo ya wafanyakazi huku akidai kwamba mgomo huo ni batili na atakayekiuka angefukuzwa kazi huku akiacha msamiati maarufu hadi leo wa “mbayuwayu, akili za kuambiwa changanya na zako”.

 

CHANGAMOTO KATIBU MKUU AJAYE

Hata hivyo, Katibu Mkuu atakayebahatika kuchaguliwa kwenye uchaguzi huo, anatarajiwa kukumbana na changamoto kadhaa zikiwamo nyongeza ya mishahara.

Nyingine ni ajira mpya, makato yanayomkabili mfanyakazi, ikiwamo kodi, michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii, hususan kuwapo kwa sheria ya fao la kujitoa ambayo inatajwa kuwa mwiba kwa wafanyakazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles