24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mauzo ya mkonge nje Dola milioni 56

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mauzo ya nje ya mkonge yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 42 hadi kufikia Dola milioni 56 kwa kipindi cha miaka miwili.

Mkakati wa Serikali ni kuongeza uzalishaji wa mkonge hadi kufikia tani 120,000 ifikapo 2025/26.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saad Kambona, akionesha mkonge unavyopandwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka (Watatu kulia), baada ya kutembelea bodi hiyo kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Akizungumza Agosti 7, 2023 Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saad Kambona, amesema mauzo ya ndani yameongezeka kutoka Sh bilioni 41 hadi kufikia Sh bilioni 43.

Kambona alikuwa akizungumza kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) Kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

“Mapato ya Serikali yameongezeka tangu ilipochukua jitihada za kulifufua zao hili mwaka 2019 na kulifanya kuwa la kimkakati. Soko la nje limefanya vizuri zaidi kwa sababu mkonge mwingi umeuzwa nje kuliko ndani,” amesema kambona.

Amesema pia uzalishaji wa mkonge umeongezeka kutoka tani 36,000 (2020) hadi kufikia tani 48,000 (2022) na kwamba malengo ya mwaka huu ni kufikia tani 60,000.

“Hadi kufikia Juni 2023 tayari tumezalisha tani 34,000 na tuna mategemeo hadi kufikia mwisho wa mwaka huu tutazalisha tani 60,000 bila wasiwasi,” amesema.

Kambona amesema jitihada kubwa zimefanyika kama vile kuongeza bajeti ya maendeleo ya bodi hiyo kutoka Sh milioni 100 mpaka kufikia Sh bilioni 2 kwa mwaka.

Amesema hatua hiyo imeiwezesha bodi kupata vitendea kazi yakiwemo magari yanayosaidia kurahisisha ukusanyaji wa takwimu, kuboresha mitambo, kugawa mbegu bure na ugawaji mashamba kwa wakulima wadogo ambayo yalitaifishwa na Serikali wilayani Kilosa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, wastani wa bei ya nyuzi za mkonge kwa tani moja kwa sasa ni Sh milioni 3.5 .

Amesema zao hilo lina fursa nyingi na linastahimili ukame hivyo linaweza kubadilisha hali za maisha ya Watanzania kwa muda mfupi.

“Tangu kupanda mpaka kuvuna ni miaka mitatu na baada ya hapo unaanza kuvuna mfululizo mara mbili kwa mwaka kwa muda wa miaka 15 mpaka 20.

“Unaweza kuchagua kulima mkonge au kuuza nyuzi au bidhaa za mkonge na kufanya ubunifu mbalimbali…ni sekta ambayo ina uwanja mkubwa wa kujiajiri,” amesema Kambona.

Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni tanzu ya NSSF inayojihusisha na uongezaji thamani zao la mkonge, Elizabeth Kalambo, amesema wanazalisha kwa wingi kamba za mkonge lakini wanakabiliwa na changamoto ya kukosa soko kutokana na kuwepo kwa kamba za plastiki.

Kalambo amesema kampuni hiyo ina wafanyakazi 1008 lakini wanazalisha chini ya kiwango kwa sababu ya ukosefu wa soko la uhakika la bidhaa za mkonge.

Katika maonesho hayo bodi hiyo inatoa elimu ya kilimo hicho ambapo pia imepanda mkonge kama shamba darasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles