25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAUAJI POLISI KIBITI YATUA BUNGENI

Na ELIZABETH HOMBO-DODOMA


BAADA ya kutokea mauaji ya askari wanane wilayani Kibiti mkoani Pwani katikati ya wiki iliyopita, vyombo vyote vya ulinzi na usalama nchi hizi nzima hivi sasa vipo katika hali ya tahadhari.

Hayo yalielezwa bungeni jana na Spika wa Bunge, Job Ndugai wakati akijibu miongozo ya wabunge waliotaka Bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili suala hilo.

Ndugai akimnukuu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema amezungumza na kiongozi huyo wa Serikali na amemhakikishia kuwa vyombo hivyo vya ulinzi na usalama vyote viko kazini.

 “Ninaomba wabunge tuwe watulivu na kwamba nimezungumza na Waziri Mkuu na amenihakikishia kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama wa nchi hivi sasa vipo kazini na si kwenye maeneo hayo tu bali nchi nzima,” alisema Ndugai.

Pamoja na hilo, kiongozi huyo wa Bunge alisema Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imekutana jana na mawaziri wenye dhamana ili kupata taarifa rasmi kuhusu matukio hayo.

Alifafanua kuwa tayari kamati hiyo ipo kazini na kupitia kikao hicho, Serikali itaeleza namna ilivyojipanga na kwamba itatoa maelezo ya namna ya kukabiliana na matukio mengine yanayoweza kujitokeza na kuhatarisha hali ya usalama wa polisi, raia na mali zao.

 “Niungane na waheshimiwa wote mlioonyesha kuguswa sana na suala hili la askari wetu, kiwango cha kufikia wanane wakati mmoja kuuawa kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha sana.

“Kwahiyo kwa niaba ya Bunge hili, ningependa kutoa pole na rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na kipekee kwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa jambo hili kubwa ambalo limetushtua wote katika nchi yetu,” alisema.

Alisema kamati hiyo inakusudia kukutana na mawaziri husika na baada ya kulifahamu vyema jambo hilo, ndipo Bunge litaweza kujadili.

“Baada ya kamati kulifahamu kwa undani wake, tutaweza kulijadili. Lakini nashukuru tayari kamati imeshaanza kuchukua hatua.

“Kwahiyo tuwape nafasi na kamati yetu ifanye kazi hii badala ya sisi wote kuifanya kwa sasa, kama kamati itaona umuhimu wa jambo hili bado tupo, tutapeana taarifa na bado tunaweza tukarudi na tukalizungumza ikibidi hapa mbele,” alisema Ndugai.

Wabunge waliosimama kuomba mwongozo kwa Spika ni pamoja na Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko (CCM), ambaye alitumia kanuni ya 69 kuomba kutoa hoja ya kuahirisha Bunge ili kujadili suala hilo.

Alisema Aprili 13, mwaka huu, katika Kijiji cha Makengeni wilayani Kibiti mkoani Pwani, waliuawa askari wanane na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.

“Mheshimiwa Spika, askari hawa walikufa wakiwa wanatekeleza majukumu ya kutulinda sisi raia na mali zetu, tukio hili si la kwanza katika Wilaya ya Kibiti, liliwahi kutokea Februari 21, mwaka huu ambapo watu watatu waliuawa akiwamo Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kibiti, Peter Kubeza.

“Kama askari hawapo salama kwa kiwango hiki, raia wa kawaida hali yao ikoje? Jambo hili limetokea Kibiti, lakini linaweza kutokea Kongwa, linaweza kutokea Bukombe, linaweza kutokea mahali kwingine kokote kama taifa halijachukua hatua madhubuti,” alisema.

Mbunge huyo alitaka suala hilo lijadiliwe ili Bunge litoe kauli kwa Serikali juu ya jambo hilo.

“Bunge lijadili ili kuondoa hofu wananchi, maana kwa matukio haya yanayoendelea kutokea wana hofu kubwa juu ya usalama wao, maisha yao na mali zao juu ya matukio haya, naomba tuahirishe Bunge tujadili suala hili,” alisema Biteko.

Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim Masoud (CCM), aliomba suala hilo lijadiliwe na kumwomba Spika atumie busara ili lipate nafasi.

Wengine ni Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM) na Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel, ambao waliunga mkono mwongozo ulioombwa na Biteko.

Kutokana na hilo, Spika Ndugai alitoa nafasi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, kuzungumzia suala hilo.

Alisema Serikali inalichukulia tukio hilo kwa uzito mkubwa ili kuhakikisha wanarejesha hali ya usalama katika maeneo hayo.

Aliwatoa hofu wananchi huku akisema kuwa tukio hilo limewapa chachu zaidi ya kupambana na uhalifu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa katika mazingira salama, wao na mali zao.

Tukio la kuuawa askari hao wanane lilitokea Alhamisi ya wiki iliyopita wakati wakitoka lindoni kuelekea kambini.

Askari hao waliouawa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Peter Kigugu, F.3451 Koplo Francis, F.6990 Konstebo Haruna, G.3247 Konstebo Jackson, H.1872 Konstebo Zacharia, H.5503 Konstebo Siwale, H.7629 Konstebo Maswi na H.7680 Konstebo Ayoub.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles