28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Matumaini mapya dawa ya ukimwi

SEATTLE, MAREKANI

KWA mara ya pili tu tangu kuibuka kwa janga la maradhi ya UKIMWI duniani, mgonjwa ameonekana kupona virusi vinavyosababisha ugonjwa huo (VVU).

Taarifa hizo kutoka kwa jopo la wanasayansi, zinakuja karibu miaka 12 tangu mgonjwa wa kwanza afahamike kuondokana na VVU kwa njia ya upandikizaji wa uboho (bone marrow)  kutoka kwa mtu asiye na maambukizo mwenye uwezo wa kuhimili maambukizo ya VVU.

Mafanikio hayo ya kushangaza, kwa sasa yanathibitisha kwamba tiba dhidi ya maambukizo ya VVU inawezekana ingawa kazi ngumu bado ingalipo, watafiti walisema.

NACP WAZUNGUMZIA MATOKEO YA UTAFITI HUO

Akizungumzia utafiti huo, Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk. Gissege Lija, alisema kuwa huo ni utafiti ambao umefanywa nje hivyo, ili kuoanisha na hapa nchini ni lazima ufanyike mwingine kama huo na yapatikane matokeo kama hayo.

Alisema kila nchi hufanya utafiti kulingana mazingira waliyopo, kwa hiyo haiwezekani kukubali moja kwa moja kile kilichofanywa na wengine bila ya wao kufanya utafiti kama huo na kupata matokeo yanayolingana.

“Utafiti ukishafanyika na ukaonekana unawezekana na unakubalika, huwa ni lazima Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo ndio linalotushauri mambo mbalimbali ya kiafya, liandike taarifa ya ushauri kwa nchi nyingine. 

“Likishaandika nasi tunapokea, tukishapokea tunaangalia kama ushahidi unaonyesha kwamba huko kulikofanyika utafiti mambo yamekuwa safi nasi tunajiridhisha,” alisema Dk. Lija na kuongeza:

“Sisi huwa tuna kitu tunafanya tunakiita ‘acceptability and implementation pilot’ kwamba, sasa tunachukua hicho kilichoandikwa kwa wenzetu, tunaanza kukifanya katika nchi yetu kwa mazingira ya kwetu.

“Hii ni kwa sababu kwenye utafiti huwa kuna vitu wanaita ‘confounding factors’ –vitu vinavyoweza kutoa matokeo yasiyotarajiwa kwenye utafiti.”

Alisema kwahiyo ili kuukubali utafiti uliofanywa na wengine, ni lazima nao wafanye kwenye nchi yao ili waweze kuona kwamba je, hicho kitu ambacho kimetoa matokeo husika, na hapa nchini kinaweza kutoa matokeo kama hayo? 

Dk. Lija alisema pia huwa wanaangalia utekelezaji wake, changamoto za hapa nchini zinazoweza kuchangia ni zipi ili wajue namna ya kufanya utafiti huo.

UBOHO HUPONYA SARATANI

Matukio yote mawili yalitokana na upandikizaji wa uboho wanaopatiwa wagonjwa walioathirika. Lakini upandikizaji huo ulilenga kutibu wagonjwa wa saratani si VVU.

Ingawa wanasayansi wanasifu mafanikio ya kisa hiki cha pili baada ya kile cha kwanza mwaka 2007, wanaonya kuwa ni mapema mno kuthibitisha kwamba mgonjwa huyo amepona kabisa.

Watafiti wametangaza kuwa mtu huyo aliyepachikwa jina la ‘mgonjwa wa London kwa sasa yuko katika hali nzuri. 

Jina hilo pia linatokana na mgonjwa huyo aliyeondolewa virusi hivyo vilivyowaathiri takriban watu milioni 37 duniani kote, kuiomba timu yake ya madaktari kuficha utambulisho wake.

Tiba na matokeo yaliyochapishwa katika jarida la kimataifa la Sayansi la Nature na yalitarajiwa kutangazwa rasmi jana katika mkutano wa masuala ya tiba unaofanyika mjini Seattle, Marekani.

Wanasayansi walitumia njia ile ile ambayo ilitumiwa na kuonyesha mafanikio kwa mgonjwa wa VVU mjini Berlin, Ujerumani mwaka 2007.

Kiongozi wa jopo la utafiti huo, Ravindra Gupta, alinukuliwa akisema, “Uamuzi wa kuitumia njia hii kunakoonyesha ahueni kwa mgonjwa huyu wa pili kulikotokana na mbinu ileile iliyotumiwa awali iliyoonesha mgonjwa wa kwanza wa Berlin hakupata matatizo yoyote.”

Katika visa vyote viwili, wagonjwa walipandikizwa uboho kutoka kwa watu waliokuwa na uwezo wa kuhimili VVU. 

Lakini pia alisema, kubadilisha chembe hai za mwathirika na za watu hao kumeonekana kumwezesha mgonjwa kuzuia VVU kurejea baada ya matibabu.

Kwa mujibu wa Gupta, mgonjwa wa London aligundulika na VVU mwaka 2003 na amekuwa akitumia dawa ya kudhoofisha makali ya virusi hivyo (ARV) tangu 2012. 

Mgonjwa huyu wa pili alifanikiwa kupandikizwa uboho mwaka 2016, lakini aliendelea kutumia tiba ya ARV kwa muda wa miezi 16 kabla ya kuacha matibabu hayo. 

Na tangu hapo, hajaonesha dalili yoyote za kuwa na VVU kwa miezi 19 sasa.

Hupta amesema hawajaona virusi hata baada ya kumpima mara nyingi. 

Hata hivyo, mtaalamu huyo alionya kwamba ni mapema mno kusema kwamba amepona.

Mtafiti huyo alisema mafanikio haya ya mara ya pili ya kuondoa VVU kwa kutumia njia hiyo ya kupandikiza uboho itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa tafiti za kimatibabu.

Lakini alisisitiza kuwa upandikizaji huo wa uboho, ambao ni hatari, unaouma na wenye gharama kubwa, hauwezi kuwa chaguo bora zaidi la tiba ya VVU kwa vile unaweza kuwa na madhara yanayoweza kudumu kwa miaka mingi.

Lakini kuingiza mwilini na chembe stahimilivu kunaweza kuzuia VVU na hilo linaweza kuwa chaguo bora la majaribio ya tiba, wataalamu walisema.

WACHANGIAJI WA UBOHO

“Hiyo itachochea watu kuamini kuwa tiba si ndoto. Bali inayoelekea kutimia,” alisema Dk. Annemarie Wensing, mtaalamu wa afya katika Chuo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Utrecht nchini Uholanzi.

Wensing ni kiongozi mwenza wa IciStem, ubia wa wanasayansi wa Ulaya wanatafiti upandikizai wa chembe hai kutibu maambukizo ya VVU.

Ubia huo unasaidiwa na AMFAR, taasisi ya utafiti wa UKIMWI nchini Marekani.

Wengi wa watu wanaoishi na chembe hai zinazohimili VVU, ziitwazo 32, wana asili ya Kaskazini mwa Ulaya. 

IciStem hutunza kanzi data za watu kama hawa wapatao 22,000.

Hadi sasa wanasayansi wanafuatilia watu 38 walioathiriwa na VVU, ambao wamepokea uboho kutoka kwa watu hao ikiwamo watano ambao hawana chembe zenye uwezo huo wa kustahimili VVU.

Mgonjwa huyu wa London alikuwa wa 36 katika orodha hiyo. 

MGONJWA AONGEA

“Najihisi wajibu wangu wa kuwasaidia madaktari kufahamu namna inavyotokea ili waweze kuendeleza sayansi,” mgonjwa huyo aliliambia gazeti la The New York Times kwa njia ya barua pepe.

Kupata taarifa kuwa naweza kupona saratani na maambukizo ya VVU ilikuwa kitu cha ajabu na kustaajabisha,” alisema na kuongeza. “Kamwe sikuwahi kufikiria kama kungekuwa na tiba ya VVU katika kipindi cha maisha yangu.”

ALIKO MGONJWA WA KWANZA

Katika mkutano kama huo mwaka 2007, daktari wa Ujerumani alitangaza tiba ya kwanza kwa ‘mgonjwa wa Berlin’, ambaye baadaye alitambulika kama Timothy Ray Brown (52) ambaye kwa sasa anaishi Palm Springs, California, Marekani.

Lakini pia Julai 2012, Brown alitangaza kuanzishwa Mfuko wa Hisani wa Timothy Ray Brown Foundation mjini Washington, ambao umejikita kupambana na VVU/UKIMWI.

Awali bango lililokuwa nyuma ya ukumbi wa mkutano kama unaofanyika jana likieleza habari hizo njema, halikupewa uzito.

Lakini mara ilipobainika kuwa ni kweli Brown alipona, wanasayansi wakaiga njia hiyo kwa wagonjwa wengine wa saratani walioathirika VVU.

SABABU ZA KUCHUKUA MUDA MREFU BAADA YA MGONJWA WA KWANZA

Katika kesi moja baada ya nyingine, virusi vilionekana kurejea baada ya miezi tisa wakati mgonjwa alipoacha kutumia ARV, au wagonjwa waliiishia kufa kwa saratani.

Kushindikana huku kuliwaumiza vichwa wanasayansi na kujiuliza iwapo pona ya Brown ilitokea kibahati tu.

Brown alikuwa na maradhi ya leukemia, na baada ya tiba ya chemotherapy kushindwa kuizuia, alihitaji kupandikizwa uboho mara mbili.

Upandikizaji kwa kawaida unatoka kwa mtu mwenye mabadiliko katika protein iitwayo CCR5, huku nyingine zikiwa na chembe hai zenye kinga. VVU hutumia protein kuziingilia chembe hizo lakini haiwezi kuzikabili toleo la protein inayoweza ubadilika.

Brown alipewa kinga kali ya dawa, ambayo haitumiki tena na alipata madhara mbalimbali kwa miezi mingi baada ya upandikizaji.

Kwa wakati fulani alipoteza fahamu na hata kukaribia kufa.

“Aliathirika vibaya na mchakato wa tiba,” alisema Dk. Steven Deeks, mtaalamu wa UKIMWI katika Chuo Kikuu cha California, San Francisco, ambaye alimtibu Brown.

“Na daima tumekuwa tukijiuliza iwapo hali zote hizo, ukubwa wa kiwango cha uharibifu katika mfumo wake wa kinga, unaeleza sababu ya kwanini Timothy alikuwa mtu pekee kupona si mtu mwingine.”

Lakini mgonjwa wa London ameweza kujibu swali hilo: hali ya kukaribia kufa ili upone haihitajiki kwa mchakato huo kufanya kazi.

Huyu alipandikizwa chembe hai stahimilivu na kupokea upandikizaji wa ubongo kutoka mtu mwenye CCR5 Mei 2016.

Kwa taarifa, CCR5 ni protein, ambazo katika miezi ya karibuni zilikuwa gumzo duniani baada ya mwanasayansi wa China, He Jiankui kudai ameweza kuzirekebisha pamoja na vinasava katika watoto wawili.

Kwa kufanya hivyo amesema watoto hao wataweza kuhimili VVU — zoezi ambalo lililaaniwa vikali duniani.

Mgonjw wa sasa pia alipokea dawa katika mfumo kinga kama ya mgonjwa wa kwanza, lakini haikuwa kali bali iliyoendana na viwango vya sasa vya upandikizaji wagonjwa.

Aliacha kutumia ARV Septemba 2017 na kumfanya kuwa mgonjwa wa kwanza tangu Brown kufahamika kutokuwa na VVU zaidi ya mwaka mmoja tangu aache kuzitumia.

“Nadhani kumebadili mtazamo kidogo,” alisema Dk.Ravindra Gupta.

“Kila mtu aliamini baada ya mgonjwa wa Berlin kwamba ilihitaji akaribie kufa ndio apone VVU, lakini tumebaini hilo si kweli.”

Ijapokuwa mgonjwa wa London hakuwa mgonjwa sana kama Brown alivyokuwa baada ya kupandikizwa, mchakato wa safari hii ulifanya kazi vyema: upandikizaji uliangamiza sararani bila kuwapo madhara mabaya ya kuumiza.

Chembe hai zilizopandikizwa sasa zinazuia VVU, zinaonekana zimeondoa kabisa zile chembe zake zilizoathirika.

Ni asilimia 59 tu ya watu wanaoishi na VVU duniani kote wanapata ARV huku watu milioni moja wakifariki kila mwaka kutokana na magonjwa yanayohusiana na VVU na UKIMWI. 

Karibu watu milioni 35 wamekufa kutokana na UKIMWI tangu kuanza kwake miaka ya 1980.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles