29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

NEC yaongeza vituo vya kupigia kura 2020

CHRISTINA GAULUHANGA Na TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeongeza vituo vya kupigia kura 858 kutoka 36,549 vya mwaka 2015 hadi 37,407 ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana na wawakilishi wa vyama vya siasa, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage,  alisema ongezeko hilo ni matokeo ya uhakiki unaoendelea nchini.

Alisema mbali ya kuongeza idadi ya vituo pia vituo 6,208 vimebadilishwa majina na vituo 817 vimehamishwa kutoka kijiji au mtaa mmoja kwenda mwingine.

“Vituo 19 vimeongezwa kutoka kata moja kwenda nyingine. Matokeo ya uhakiki wa vituo vya kupigia kura kwa Tanzania Zanzibar yanaonyesha vituo vimeongezeka kutoka 380 bado vituo 407,” alisema Jaji Kaijage.

Akizungumzia kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, Mwenyekiti huyo wa NEC, alisema mchakato wa kupata vifaa vya kukarabati machine za BVR umekamilika.

‘Kinachosubiriwa ni kuvifanyia majaribio ya uandikishaji katika kata mbili za Kihonda Manispaa ya Morogoro na Kata ya Kibuta Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe,” alisema 

Alisema kwa Zanzibar vimeongezeka kutoka 380 na kufikia 407. 

Mwenyekiti huyo wa NEC alisema tume yake imefanya uhakiki kuona kama vituo hivyo vinakidhi matakwa ya kisheria na kufanya mabadiliko na hivyo kubaini ongezeko hilo. 

“Lengo la kukutana hapa ni kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 pamoja na kuangalia namna ya kuboresha  Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na mchakato wa uchaguzi mkuu ili kuhakikisha unakuwa huru na haki,” alisema Kaijage.

Alisema mchakato wa kuboresha  daftari hilo ni mkakati wa kujiandaa na Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.

“Katika maandalizi hayo ,Tume chini ya Ibara ya 74(6) ya Katiba ya nchi yetu ya mwaka 1977 imepewa mamlaka ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya msingi ikiwa ni pamoja na jukumu la kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura.

“Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ,sura ya 324 na ya kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa sura ya 292 ,Tume inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la wapiga kura kwa mara mbili katika Uchaguzi Mkuu mmoja na uchaguzi mwingine unaofuata,’’ alisema Jaji Kaijage.

Alisema ni kawaida kabla ya kuanza kwa mchakato wa uandikishaji, hufanyika majaribio ili kuona namna na jinsi vifaa vya uandikishaji vinavyofanya kazi katika mazingira tofauti ,lengo likiwa ni kupata na kuwa na namna  bora ya kufanikisha mchakato huo.

“Maandalizi mengine ambayo tayari yamefanyika ni uchapishaji wa miongozo mbalimbali kwa wadau ikiwamo ya kutoa elimu kwa mpiga kura na maelekezo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, kwa watendaji na wadau wa uchaguzi vikiwamo vyama vya siasa.

“Tume imejiwekea utaratibu wa kuwashirikisha wadau katika hatua mbalimbali za uchaguzi, kwa lengo la kuhakikisha inajenga na kutekeleza misingi ya kidemokrasia katika kusimamia, kuratibu na kuendesha chaguzi zilizo huru, wazi, za haki na kuaminika,” alisema 

Jaji Kaijage, alisema wameona ni vema ikawapitisha katika kanuni hizo kwa kuangalia yale maeneo ambayo yamefanyiwa marekebisho ama kwa kuondoa au kuongeza vifungu lakini kwa kueleza sababu za marakebisho hayo.

WADAU

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema ushirikishwaji wa wadau kutoka vyama vya upinzani ni mdogo kutokana na kushirikishwa baada ya kanuni hizo kutungwa.

“Hatua hii ni mchakato muhimu kwetu ilitakiwa tushirikishwe mapema lakini cha ajabu kanuni zipo tayari zimepata nguvu za kisheria ndipo tunaletewa suala hili linatufanya  nchi hii hakutakuwa na mabadiliko ya kweli,” alisema Shaibu.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA ), Hashimu Rungwe, alisema wameshindwa kutoa maoni kwa sababu vituo vingi vimeongezwa na tume hiyo bila kushirikisha wadau.

“Kwa hiyo tutaangalia mchakato unavyokwenda kama tutaweza tutaingia kwenye uchaguzi na tukishindwa tutakaa pembeni kwa kuwa tangu kuanza kwa mchakato huu hatukushirikishwa,” alisema Rungwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles