27 C
Dar es Salaam
Friday, May 27, 2022

Mashauri 4,700 yaendeshwa kwa njia ya mtandao

Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Tanzania imefanikiwa kuendesha mashauri 4,711 katika kipindi cha miezi miwili kwa njia ya Mahakama Mtandao (Video Conference), ikiwa ni hatua mojawapo za kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Mashauri hayo yamesikilizwa kwa njia  hiyo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alilolitoa Machi 23 mwaka huu, ili kuwaepusha watumishi wa mahakama, magereza, wafungwa na mahabusu na wateja wengine dhidi ya maambukizo hayo, wakati shughuli za utoaji haki zikiendelea kufanyika.

Agizo hilo lilitolewa na Profesa Juma kupitia  mkutano wake na waandishi wa habari  uliofanyika Mwanza, akitaka chombo hicho kuongeza kasi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kipindi hiki ambacho taifa na dunia nzima inapambana na janga la ugonjwa huo.

Akizungumzia kuhusu usikilizaji wa mashauri kwa kutumia teknolojia hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Tehama, Machumu Essaba alisema umelipunguzia pia Jeshi la Magereza gharama za usafiri wa kila siku za kuwaleta wafungwa au mahabusu mahakamani na msongamano.

“Njia hii imetumika katika kipindi cha ugonjwa huu, kuanzia Machi 23, mwaka huu hadi Mei 26, mwaka huu, ambapo Mahakama ya Rufani Tanzania imesikiliza mashauri 48 kupitia vikao vitano, kati ya hivyo vitatu vilifanyika katika Jiji la Dar es Salaam, vilivyohusisha mashauri 30 na kimoja Tabora kilichohusisha mashauri tisa na kingine Iringa kilichokuwa na mashauri tisa,” alisema Essaba.

Alisema Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imesikiliza mashauri 3,188 kati ya hayo, 804 yamesikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama za Wilaya Kinondoni 714, Ilala 992, Temeke 523 na  Kigamboni 155.

Alisema Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mahakama ya Mkoa na Wilaya mashauri yaliyosikilizwa kwa teknolojia hiyo ni 367.

Alisema kanda zingine ni Tanga mashauri 310, Musoma 158, Tabora 130, Dodoma 78, Mtwara 66, Moshi 46, Arusha 41, Kigoma 37, Sumbawanga 23, Iringa 15, Songea 14, Shinyanga 12, Mwanza 28 na Bukoba 5.

Essaba alifafanua kwamba Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imesikiliza mashauri 55 na Kazi mashauri 90, ambazo zilitumia vifaa vilivyopo kwenye maeneo yao.

Aidha aliongeza kwamba  zaidi ya mashauri 300 yamesikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kwa kutumia simu ya mezani (Teleconference) kwa sababu kuna tatizo la ukosefu wa huduma ya  mtandao (internet) kwenye ofisi  za Mwanasheria wa Serikali.

Uongozi wa Mahakama katika kuunga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na virusi vya corona, ulikabidhi vifaa vya Tehama kwa maofisa Tehama wa kanda 16 za Mahakama Kuu Aprili 21, mwaka huu ili kuziwezesha mahakama nyingine kuanza kusikiliza mashauri  kwa Mahakama Mtandao.

Awali teknolojia hiyo ilikuwa inatumika katika vituo sita vilivyofungwa mfumo huo ambavyo ni  Mahakama Kuu ya Tanzania katika kanda za Dar es Salaam, Mbeya na Bukoba pamoja na Kituo cha Mafunzo cha Kisutu, Gereza la Keko na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,454FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles