25.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Mahabusu kuanza kufanya kazi kama wafungwa

Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha mahabusu waliopo katika magereza nchini wanaanza kufanya kazi kama ilivyokuwa kwa wafungwa. 

Amesema mchakato huo ambao tayari umeanza, utakapokamilika utaleta mapendekezo ya jinsi gani ya kuwatumia mahabusu hao na wafungwa kufanya kazi za uzalishaji mali na kuhakikisha Jeshi la Magereza linajitegemea kikamilifu. 

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na maofisa na askari magereza katika magereza ya Segerea, Ukonga na Keko Dar es Salaam, alipofanya ziara ya kusisitiza magereza kujitegemea.

Alisema ili binadamu ale ni lazima afanye kazi na pia vitabu vitakatifu vinasisitiza hilo, hivyo mahabusu wanapaswa kufanya kazi kwa kuwa nao wanakula vyakula magerezani. 

“Kuna mjadala mkubwa tunaendelea kuchakata kuhusu mahabusu waweze kufanya kazi, lengo letu si kuwafanyisha kazi za sulubu, au kazi zinazotweza utu wao, hapana, wao pamoja na wafungwa wana adhabu wanayoitumikia, tunataka kuwatumia katika kuzalisha, kwahiyo watafanya kazi kama watu wengine wanavyofanya kazi, hili naomba lieleweke.

 “Mjadala unaendelea na tutakuja na majibu ya jinsi ya kuwatumia mahabusu na wafungwa, tunataka kuwatumia kwa nia njema ya kuzalisha, kama mnavyojua binadamu asipofanya kazi asile na imeandikwa katika vitabu vitakatifu.

“Kama mtu umemfungia ndani alafu hafanyi kazi na anadai chakula, na ajue kwamba asipofanya kazi hana haki ya kula, wewe umekuja ni mahabusu, ili upeleke tonge lazima uzalishe, huwezi kusema sifanyi kazi kwa sababu ni mahabusu, hapana, tutakulinda hata kwa bunduki utafanya kazi,” alisema Simbachawene.

Alisema lazima kuwepo na mtazamo mpana, mkubwa katika masuala ya kuzalisha na kujitegemea kwa Jeshi la Magereza, kuzalisha pamoja na kutatua matatizo mengine ndani ya jeshi hilo, ikiwemo kujenga nyumba, kulipa umeme pamoja na mahitaji yake mbalimbali.

“Kama nilivyosema, mjadala bado ni mkubwa kwa wafungwa na tunafahamu wapo chini ya magereza, lakini hao wengine tumepewa tuwatunze, wapo chini ya vyombo vingine, hivyo tunaendelea na mchakato wa kujadiliana kuhusu hilo, na ukikamilika tutawaletea majibu,” alisema Simbachawene. 

Alisema dhana ya jeshi hilo kuzalisha na kujitegemea ni agizo la Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dk. John Magufuli kulitaka kuzalisha kwa wingi ili kujitosheleza na kujitegemea. 

Aidha, alilitaka jeshi hilo kuhakikisha magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam yaanze kufanya kilimo cha mboga za majani na matunda pamoja na ubunifu wa uzalishaji mwingine katika mkoa huo.

Kwa magereza yaliyopo mikoani alisema yaendelee na kilimo cha mpunga, mahindi, ufugaji na uzalishaji wa aina nyingine wanaoendelea nao katika maeneo yao. 

Alisema kupitia uzalishaji mali huo, utawezesha kupata fedha baada ya kuuza na kusaidia majukumu mengine ya jeshi kuliko kutegemea fungu la fedha za matumizi mengine (OC) ambalo utolewa na Serikali kwa jeshi hilo. 

Simbachawene alilitaka jeshi hilo kuhakikisha linahakiki mali zake zote, ikiwemo mashamba yajulikane na pia ijulikane yana hati au hayana, na mifugo ya jeshi hilo ipo wapi na idadi yake, ikiwa ni lengo la kutambua mali hizo na kuwekwa wazi kwa sababu ni mali za umma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Solomon Urio, alimshukuru waziri huyo kwa kufanya ziara katika mkoa huo na kuwaomba viongozi nchini waweze kutembelea magereza ili waweze kujifunza na kujua kazi zinazofanywa na jeshi hilo mkoani humo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,567FollowersFollow
517,000SubscribersSubscribe

Latest Articles