23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Marekani yaiadhibu Tanzania

usaid-fund*Ni kwa makosa yaliyofanyika Zanzibar

*Sheria ya makosa ya mtandao yaumiza

Na Mwandishi Wetu

MAREKANI imeinyima Serikali ya Tanzania msaada wa dola milioni 472 (zaidi ya Sh trilioni moja) za msaada za mfuko wa changamoto za milenia (MCC).

Wakati Tanzania ikinyimwa fedha hizo nchi za Ivory Coast, Kosovo na Senegal zimepewa huku Niger, Nepal na Ufilipino zikifuzu vigezo vya kupatiwa msaada huo kwa mwaka 2016.

Ripoti ya MCC ambayo MTANZANIA Jumamosi imeiona inaonyesha kuwa Bodi ya kuidhinisha msaada huo ilikaa Desemba 16 mwaka huu na kufikia uamuzi wa kuinyima Tanzania msaada huo.

Ripoti hiyo inataja sababu zilizozingatiwa kuinyima Tanzania mamilioni hayo ya dola kuwa ni kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar licha ya kuwa katika hali ya amani ya utulivu.

Inataja sababu nyingine kuwa ni matumizi ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

“Bodi iliahirisha kupiga kura kwa Tanzania. Bodi ilijadili wasiwasi unaoendelea kuhusu uchaguzi wa Zanzibar pamoja na matumizi ya sheria ya makosa ya mtandao wakati wa uchaguzi. Bodi inaweza kupitia upya uamuzi wake katika kipindi cha mwaka 2016 kama taarifa zaidi zitapatikana,” inasomeka taarifa hiyo.

Jana Balozi wa Marekani nchini, Mark B. Childress, alitoa tamko kuhusu uamuzi wa Bodi ya MCC kuahirisha kupigia kura ya kuipatia msaada huo Tanzania.

“Bodi ya MCC haikuichagua Tanzania katika mkataba wa pili. Bodi iliahirisha kupigia kura mkataba wa pili, ikisubiri kutatuliwa kwa masuala ya kiutawala. Bodi inaweza kuangalia upya iwapo Tanzania inastahili kupewa msaada huo mwaka 2016.

“Ninatumaini kwamba Serikali ya Tanzania itachukua hatua hivi karibuni zitakazotatua masuala hayo ya kiutawala,” alisema Balozi Childress.

Alisema baada ya kuchukuliwa kwa hatua hizo Bodi ya MCC itaweza kupiga kura kuichagua tena Tanzania na kuidhinisha maendeleo ya mkataba.

Balozi huyo alisema masuala ya kiutawala ya Bodi yanaakisi maadili ya muda mrefu ya MCC hivyo kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar kulisitisha mchakato wa uchaguzi uliokuwa unaenda vizuri.

Alisema matumizi ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 kwa kuwakamata watu waliokuwa na kibali halali kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi yalikwaza uhuru wa msingi wa kujieleza na kukutana.

Hata hivyo, Balozi Childress, alisema MCC imetiwa moyo na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli za kuimarisha vita dhidi ya ubadhirifu na rushwa.

“MCC inatumaini kuwa jitihada hizo zitaendelea na kuleta mabadiliko ya kimfumo,” alisema Balozi Childress.

MCC imefikia hatua ya kuinyima Tanzania fedha hizo ikiwa ni siku chache baada ya Kamishna wa Bajeti wa Wizara ya Fedha, John Cheyo, kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza kuwa fedha za MCC zitapatikana mwezi Juni mwakani.

Kauli hiyo ya Cheyo aliitoa siku moja baada ya vyombo vya habari kuripoti kuhusu barua ya MCC ya Novemba 19 iliyoandikwa kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, ikionya kuwa mgogoro wa Zanzibar na sheria ya uhalifu wa mtandao vinaweza kuathiri vigezo vya kuiwezesha Tanzania kupata msaada huo wa dola milioni 472.

“Vigezo vilivyotajwa katika barua hiyo vinafanyiwa kazi na fedha hizo zinatarajiwa kupatikana ifikapo Juni mwakani kwa ajili ya kutumika katika bajeti ya 2016/17.

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta tena jana Kamishna huyo kwa njia ya simu ili kulizungumzia jambo hilo lakini hakupatikana.

Machi mwaka huu, Marekani ilisema bado ilikuwa ikiendelea kuichunguza Tanzania kama inakidhi vigezo vya kupewa msaada wa MCC uliokuwa ukifikia dola za Marekani milioni 700, sawa na Sh trilioni 1.3.

Mwaka jana pia Marekani iligoma kutoa fedha za MCC kiasi cha dola 472 sawa na Sh bilioni 765 hadi utekelezaji wa azimio la Bunge kuhusu ufisadi katika Akaunti ya Tegeta Escrow utakapofanyiwa kazi.

Hata hivyo, Serikali ya awamu ya nne iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, iligoma kutekeleza agizo hilo kwa shinikizo la msaada.

Licha ya kusainiwa mkataba husika kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, fedha hizo hazikutolewa kwa kile kinachodaiwa baada ya kuibuliwa kwa sakata la Escrow na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila bungeni mwishoni mwa Novemba, 2014.

Akichangia katika mjadala wa ripoti ya PAC bungeni kuhusu suala la Escrow, Kafulila alisema moja ya athari zilizosababishwa na uchotwaji wa fedha hizo ni pamoja na Marekani kupitia MCC kusitisha utolewaji wa USD milioni 472 kwa Serikali ya Tanzania. Kauli ambayo ilipingwa vikali na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya.

Bodi ya MCC ilitoa masharti kwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuona inawachukulia hatua wale waliohusika katika sakata hilo la kuchotwa kwa zaidi ya Sh bilioni 206 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles