22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wahuni wampiga chenga Rais Magufuli

Pg 1*Wamkimbia Dar kukwepa kodi , watimkia bandari za Tanga na Mtwara

NA MWANDISHI WETU

MTANDAO wa wafanyabiashara wasio waaminifu unaojihusisha na ukwepaji kodi wa bidhaa mbalimbali zinazoingizwa nchini kupitia bandari, umekimbia Dar es Salaam na kuhamishia shughuli zake kwenye mikoa ya Tanga na Mtwara.

Taarifa za uhakika zilizolifikia MTANZANIA Jumamosi zimeeleza kuwa wafanyabiashara hao na mawakala wao wameondoa maskani yao kwenye Bandari ya Dar es Salaam na kuyapeleka bandari za Tanga na Mtwara.

Imeelezwa kuwa kuhama kwa wakwepa kodi hao kumesababishwa na msako wa wakwepa kodi katika Bandari ya Dar es Salaam ulioanzishwa na Rais John Magufuli, ambaye amekwishawatia kitanzani baadhi ya maofisa wa Serikali wanaotuhumiwa kushirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kukwepa kulipa kodi halali ya Serikali.

Miongoni mwa maofisa wa Serikali waliosimamishwa kazi na wengine uteuzi wao kutenguliwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kuikosesha Serikali mapato ni wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA).

Taarifa zimeeleza kuwa mbali na kuikimbia Dar es Salaam, mtandao huo wa wakwepa kodi pia umebadilisha mbinu za kupitisha mizigo isiyolipiwa kodi lengo likiwa kuwakwepa maofisa wa TRA.

Mmoja wa wafanyabiashara anayepitisha mizigo yake katika Bandari ya Dar es Salaam, ameliambia gazeti hili kuwa hivi sasa mawakala wa wakwepa kodi wanawahi makontena wanayoyalenga yanaposhushwa tu bandarini wanapakua mizigo yote na kuyaacha tupu hivyo wakifika maofisa wa TRA huyakuta yakiwa hayana mizigo.

“Wamemkimbia Rais Magufuli, wamemuacha Dar es Salaam wao wamepeleka maskani yao kwenye bandari za Tanga na Mtwara na hata mbinu za kufaulisha mizigo yao isiyolipiwa kodi nazo wamebadilisha.

“Sasa hivi wana mtindo mpya, wanavizia makontena yao yanapoingia tu bandarini wanapakua mizigo yote na kuyaacha tupu hivyo wanapokwenda maofisa wa TRA wanakuta hayana mizigo, yako tupu na wanapata hela nzuri kweli kwa sababu kufaulisha kontena moja siyo chini ya Sh milioni tano,” alisema mfanyabiashara ambaye jina lake tunalihifadhi.

Mfanyabiashara huyo alieleza zaidi kuwa hivi sasa kazi ya kuvusha mizigo bila kulipiwa ushuru inafanywa kwa umakini mkubwa na mara nyingi imekuwa ikifanyika nyakati za usiku kwa msaada wa baadhi ya watumishi wa idara za Serikali.

Mfanyabiashara mwingine aliyezungumza na gazeti hili ambaye pia jina lake tunalihifadhi alieleza kuwa mtandao wa wafanyabiashara wakwepa kodi ni mkubwa na unawahusisha pia watumishi wa Serikali ambao wamekuwa katika ushirika huo kwa muda mrefu.

Alizitaja bidhaa zinazoongoza kupitishwa kwa magendo kuwa ni sukari inayotoka katika nchi za Brazil na India pamoja na makaa ya mawe yanayotolewa nchini Afrika Kusini.

“Wanaingiza sukari kutoka Brazil na India na ukichunguza sukari hiyo utabaini muda wake wa matumizi ya binadamu umekwisha. Wanapoipakuwa wanakwenda kuifunga katika mifuko mipya inayoonyesha kuwa ni sukari iliyozalishwa katika viwanda vya hapa nchini.

“Bandari ya Tanga hivi sasa ndiyo kichochoro cha wakwepa kodi na siku hizi kuna makaa ya mawe yanayotoka Afrika Kusini ambayo yanaingizwa kwa wingi hapa nchini ingawa hatujui yanapelekwa wapi,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu ukweli wa taarifa hizo, Kaimu Meneja Mawasiliano wa TPA, Janeth Luzangi, hakukataa wala kukubali bali alionyesha mshangao huku akiahidi kufuatilia na kutoa tamko hivi karibuni.

Jitihada za kumpata Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa  Kodi wa TRA, Richard Kayombo, hazikuweza kufanikiwa na hata alipopigiwa simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.

Taarifa hizi zimepatikana ikiwa ni wiki kadhaa sasa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam na TRA na kuibua upotevu wa makontena 329 ambayo pia hayakuwa yamelipiwa ushuru.

Kuibuliwa kwa kashfa hiyo ilifuatiwa na hatua za kutenguliwa kwa uteuzi wa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade na kukamatwa kwa Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki pamoja na maofisa wengine waliohusishwa nayo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles