32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, February 2, 2023

Contact us: [email protected]

Marehemu waandikiwa barua za kujieleza

 Kiomoni Kibamba
Kiomoni Kibamba

NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

SUALA la wanafunzi  hewa 5,559  wa shule za sekondari na msingi   Mwanza, limechukua sura mpya baada ya kubainika walimu 60 waliosimamishwa kazi  na Mkurugenzi wa Jiji hilo, Kiomoni Kibamba na kupatiwa barua za kujieleza,  miongoni mwao wamo marehemu, wastaafu na wengine ni wakuu wa wilaya walioteuliwa hivi karibuni.

Kutokana na utata huo, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Mwanza, kimempatia  siku tatu  Kibamba kuomba msamaha kuhusu  taarifa aliyoitoa kwenye vyombo vya habari kwa kuwavua madaraka, kuwasimamisha kazi na kuwadhalilisha walimu, vinginevyo watamfikisha mahakamani.

Wakati CWT ikitishia kwenda mahakamani, Kibamba alisema amezaliwa kwenye sheria  na kusisitiza hakubahatisha kuchukua uamuzi  dhidi ya walimu hao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa CWT Mkoa  wa Mwanza, Sibora Kisheri alisema  amesikitishwa na hatua iliyochukuliwa na Kibamba kuwavua madaraka walimu wakuu na kuwasimamisha kazi kwa tuhuma za wanafunzi hewa wakati wengine si wahusika katika shule tajwa.

Kisheri alisema walimu wa shule za msingi 37 na wengine 23 wa  sekondari walipokea barua zilizoandikwa Septemba 21, mwaka huu na kutakiwa kujieleza  sababu za kuwapo na  ongezeko  la wanafunzi hewa.

Alisema baada ya walimu kukimbilia CWT, waliamua kukaa na kupitia nakala ya kila shule na kubaini takwimu zao ziko sahihi, ispokuwa  ofisi ya mkurugenzi wa jiji inatumia takwimu za mwaka 2015 ambazo hazina uwiano.

“Kasoro nyingine iliyogundulika ni baadhi ya walimu waliosimamishwa kazi hawahusiki na shule tajwa kwa kuwa walihamishwa miaka mingi kabla ya mfumo wa elimu bure kuanza,  wengine wapo masomoni…kibaya zaidi wapo walimu waliofariki dunia, waliostaafu na wengine wameteuliwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa wakuu wa wilaya, nao wamepewa barua za kujieleza.

“Aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Nyakurunduma, January Lugangika ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga. Wakati anateuliwa alikuwa  Shule ya Sekondari  Nsumba… cha kushangaza alikuwa mwalimu wa kawaida lakini naye amepewa barua ya kujieleza.

“Kwa mfano mwalimu Nassoro Rashid kutoka Shule ya Msingi Makongoro ni marehemu, naye amepewa barua ya kujieleza, pia wapo waliostaafu akiwamo Abbas Mohamed aliyekuwa Shule ya Msingi Nyakato C amepewa barua, wote hao hawajui chochote juu ya elimu bure,”alisema.

Kisheri aliwataja walimu waliopewa barua za kujieleza wakati hawahusiki na shule tajwa kuwa ni   Lowa Paul,  Regine Kipeja, Annastazia Maswi,Wande Muknkyala,Aidan Dotto na Jumanne Nyanda.

Kibamba alipotafutwa alisema hawezi kuomba radhi wala kutengua barua hizo kwa kuwa anaamini uamuzi wake ni sahihi kwa kuwa kamati mbili zilizoundwa kufuatilia zilitoa majibu yanayofanana.

“Ndugu mwandishi nikuambie sijakurupuka kuwapumzisha walimu hao, tumeunda kamati mbili zimekuja na takwimu hizo hizo. Kama kuna mtu ameonewa basi wasubiri TSD ifanye kazi yake atarudi kazini lakini najua sijabahatisha katika hilo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles