Na MANENO SELANYIKA -DAR ES SALAAM
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuph Manji, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, amedai mahakamani kuwa, hatambui kuvuliwa udiwani wa Kata ya Mbagala Kuu.
Manji alisema hiyo ni kwa sababu hajapokea taarifa kutoka Manispaa ya Temeke, inayoonyesha kuwa amevuliwa nafasi hiyo.
Manji amesema hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, wakati kesi yake ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Alidai taarifa hizo alizisoma kupitia kwenye gazeti moja la kila siku (si Mtanzania) kwamba amevuliwa udiwani, ambapo hajui kama ni kweli au la.
“Naiomba mahakama yako imwagize Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) awaambie Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kwamba walimkamata na sababu za kutohudhuria vikao kwa miezi miwili ni kwa kuwa hana dhamana,” alidai Manji.
Alidai kuwa, anachotambua yeye ni kwamba bado ni Diwani wa Mbagala Kuu, hatambui kama amevuliwa wadhifa huo, kwani tayari ametumia fedha zake binafsi zaidi ya Sh milioni 70 na si za Halmashauri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake.
Mara baada ya kusema hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, Hakimu Shaidi aliwataka upande wa mashtaka kufuatilia malalamiko ya Manji kuhusu udiwani wake.
Mbali na Manji, washtakiwa wengine ni Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda, Mtunza stoo, Abdallah Sangey na Thobias Fwere.
Kwa upande wa utetezi, uliokuwa unaongozwa na Wakili Seni Malimi, aliomba tarehe fupi kwa ajili ya kuleta maombi maalumu.
Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.
Inadaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A, wilayani humo, washtakiwa wote kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya Sh milioni 192.5.
Shtaka jingine ni kwamba, Julai Mosi mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe A, wilayani Temeke, Dar es Salaam, washtakiwa wote walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo nane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ, vyenye thamani ya Sh milioni 44.
Kwamba Juni 30, mwaka huu maeneo ya Chang’ombe A, kwa pamoja walikutwa wakiwa na mhuri wa JWTZ ambao uliandikwa “Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha JWTZ’’ bila kuwa na uhalali, kitendo kinachohatarisha usalama wa nchi.
Pia inadaiwa, tarehe hiyohiyo maeneo ya Chang’ombe, washitakiwa walikutwa na mhuri uliokuwa umeandikwa “Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma” bila kuwa na uhalali, kitendo kinachohatarisha usalama.
Ilidaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo hayo, washitakiwa kwa pamoja walikutwa na mhuri ulioandikwa “Commanding Officer 835 KJ, Mgambo P.O. Box 224 Korogwe” isivyo halali.
Katika shtaka la sita, inadaiwa Julai Mosi mwaka huu, maeneo hayo ya Chang’ombe, washitakiwa walikutwa na gari lenye namba za usajili SU 383, mali waliyojipatia isivyo halali.