25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

ASKOFU KILAINI, NZIGIRWA WARUDISHA FEDHA ZA ESCROW

Na EVANS MAGEGE

MAASKOFU wawili wa Kanisa Katoliki waliopatiwa mgawo wa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow wameamua kuzirudisha serikalini ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za uhujumu uchumi unaomkabili muumini aliyewagawia, ambaye ni James Rugemalira.

Maaskofu hao ni Method Kilaini na Eusebius Nzigirwa, ambao Februari, 2014 walipatiwa mgawo wa fedha hizo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira.

Katika mgawo huo, Askofu Kilaini alipokea Sh milioni 80.5 na Askofu Nzigirwa alipokea Sh milioni 40.4.

Kwa mujibu wa tangazo la pamoja la maaskofu hao lililosambazwa juzi katika mitandao ya kijamii siku hiyo hiyo, kabla ya kuthibitishwa na Askofu Kilaini jana kwa njia ya ujumbe mfupi, limesema maaskofu hao wamechukua uamuzi wa kuzikabidhi serikalini fedha hizo hadi uchunguzi wa kesi hiyo utakapokamilika na uamuzi kutolewa.

Tangazo hilo lilisomeka: “Mnamo mwezi Februari, 2014, sisi Maaskofu Method Kilaini na Eusebius Nzigirwa, tulipokea fedha zilizotumwa na James Rugemalira (kupitia kampuni yake ya VIP Engineering) kwenye akaunti zetu zilizopo Benki ya Mkombozi, Dar es Salaam.

“Tulipokea matoleo hayo kutoka kwa muumini wetu kwa moyo wa shukrani na roho safi. Lakini mnamo Juni, mwaka huu Rugemalira alikamatwa na vyombo vya dola na kutuhumiwa na makosa ya kuhujumu uchumi, ambapo fedha alizozituma kwa watu mbalimbali zikihusishwa.

“Kutokana na kuwepo kwa kesi kuhusu fedha hizo (bila kutoa hukumu) tumeona ni vema tuzikabidhi kwa Serikali hadi uchunguzi kuhusu kesi hiyo utakapokamilika na uamuzi kutolewa, ili yule mwenye haki ya kuwa na fedha hizo aweze kupewa kama ilivyostahili.”

Januari 23, mwaka juzi, wakati sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Escrow likiwa bado limepamba moto, gazeti hili lilimuuliza Askofu Kilaini  kama ameshahojiwa na Serikali kuhusu mgawo wa fedha hizo na alijibu kuwa hajahojiwa na taasisi yoyote, ikiwamo Kanisa Katoliki au Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Katika maelezo yake, alisema wazi kuwa, yupo tayari kuhojiwa na Takukuru kama taasisi hiyo itamhitaji afanye hivyo, kwa sababu hana cha kuficha juu ya fedha alizogawiwa na Rugemalira.

“Sijahojiwa na taasisi yoyote, liwe Kanisa au Takukuru. Hata wakinihitaji nipo tayari kwa kuhojiwa kwa sababu sina cha kuficha na hili jambo la kupokea fedha kwa wafadhili kwa ajili ya kusaidia jamii ni sehemu ya maisha yangu kwa kipindi cha miaka 40 sasa,” alisema Kilaini.

Katika ufafanuzi wake, alisema kama fedha za Escrow zitathibitishwa kuwa ni chafu, atazirudisha kwa aliyemgawia.

“Hizi fedha hazijathibitishwa kama ni chafu na kama ikitokea hivyo nitamrudishia Rugemalira,” alisema.

Alipoulizwa kama fedha hizo zipo au katumia na kama amezitumia atazirudisha kwa utaratibu upi, alijibu kuwa fedha hizo ametumia kiasi, hivyo ikitokea zikathibitishwa kuwa ni chafu itambidi  azitafute.

“Fedha zimetumika kiasi ambazo itabidi nizitafute kukamilisha kiasi nilichopewa, hii ni changamoto, lakini sitaacha au kukata tamaa katika azma ya kuendeleza kanisa na jamii nikitumia misaada mbalimbali, yalipoanza maneno nilisitisha matumizi ya fedha hizo hadi mambo yawe wazi,” alisema Kilaini.

Alipoulizwa kiasi kilichotumika hadi anasitisha matumizi ya fedha hizo, alijibu kwa ufupi kwamba mahali alipo hakuwa na hesabu kamili, hivyo alihofia kusema uongo.

Hata hivyo, alisema matumizi ya fedha hizo yalikusudia kuanzisha vituo vya wagonjwa wa saratani pamoja na kusaidia jamii yenye uhitaji.

Alifafanua kwamba, wakati anachukua uamuzi wa kusitisha matumizi ya fedha hiyo alikuwa katika hatua ya upembuzi yakinifu wa kuanzisha vituo vya wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Kagondo, Lubya na Mgana, zote za Mkoa wa Kagera.

“Tayari kulikuwa na wataalamu kutoka India niliwaleta kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa hospitali nilizozitaja, pia nilikusudia kuanzisha kituo cha wagonjwa wa saratani huko Biharamulo na Morogoro,” alisema Kilaini.

Mbali na vituo vya wagonjwa wa saratani, pia alisema fedha hizo alizitumia kusaidia vikoba vinne vya akina mama wa Jimbo la Bukoba na wanafunzi 14 aliokuwa anawasomesha.

“Kuna mambo mengi katika jamii ambayo yanahitaji misaada, kuna vikoba kwa ajili ya kuwakwamua akina mama kiuchumi, kuna wazee wasiojiweza, pia kuna vijana 10 wa shule za sekondari na wanne wa vyuo vikuu wote ninawasomesha, hivyo sehemu ya fedha ilitumika katika mahitaji yao,” alisema.

Pia alifafanua uhusiano wake na Rugemalira kwamba ulianza tangu mwaka 1975, wakati huo akiwa Padri wa Parokia ya Bukoba na alimsifu kuwa ni mkarimu siku zote katika kanisa na jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles