31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Manhattan inapowaamsha wagombea urais Marekani

Polisi wakilinda usalama baada ya mlipuko Manhattan.
Polisi wakilinda usalama baada ya mlipuko Manhattan.

NA RAS INNO,

KABLA ya shambulio la kigaidi lililofanyika siku nne zilizopita huko Chelsea Manhattan, New-York nchini Marekani, kilichokuwa kikiendelea kugonga vichwa vya habari nchini humo ni afya za wagombea urais wa vyama vya Republican na Democrat.

Afya iligeuka habari kubwa baada ya Hillary Clinton kutaka kudondoka katika maadhimisho ya miaka 15 ya shambulio la kigaidi kwenye kituo cha biashara cha Word Trading Centre, lililopelekea Marekani kumsaka hadi kumwangamiza kinara wa ugaidi duniani, Osama Bin Laden.

Licha ya kuuawa, ugaidi bado ni mwiba duniani kutokana na kuibuka makundi yenye mbinu za kisasa zaidi yanayohusudiwa hadi ndani ya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani, kutokana na vijana wengi kujipeleka kujiunga nayo hususan Islamic State (IS) ambalo ni kiini kinachoigonganisha Urusi na Marekani katika mapigano yasiyo na mwelekeo yanayoendelea Syria, Iraq na Uturuki.

Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imekuwa mfariji wa nchi marafiki zinazoshambuliwa na magaidi kwani haijawahi kutikiswa kwa shambulio kubwa kutokana na kujizatiti baada ya kupigwa na Osama mwaka 2001.

Wanaoiunga mkono katika vita dhidi ya ugaidi ndiyo wanaokumbana na kisago cha mashambulizi ikiwemo Ufaransa, Ubelgiji, Uturuki na Ujerumani.

Lakini muktadha wetu leo unanasibisha tukio la Manhattan na ajenda zilizokosa mashiko za wagombea urais wa Marekani, kwani kama ilivyo chaguzi za duniani kote wamejikita zaidi katika kuzungumzia mambo binafsi ikiwemo afya zao, huku Trump akitoa ripoti ya afya yake kwenye kipindi cha runinga, Hillary akigeuka mjadala kutokana na kuficha kuugua Pneumonia hadi alipotaka kuanguka na kulazimika kusitisha kampeni zake kwa muda ili kupata mapumziko.

Walichojisahau ni kwamba wasiowatakia mema wakiwemo magaidi wamesoma udhaifu wa mambo wanayozingatia, wakatumia ombwe hilo na kujipenyeza kwa shambulizi la Mahhattan ambalo hadi sasa haijafahamika kama lina mkono wa makundi ya kimataifa ya kigaidi au ni suala la ugaidi wa ndani tu.

Lakini kwa shambulizi kufanyika siku chache baada ya maadhimisho ya Septemba 11 na miezi miwili na ushei kabla ya uchaguzi, inamaanisha kwamba Marekani inapoteza mweleko wa ajenda kupitia wagombea wote kwani badala ya kuzingatia mambo nyeti kama usalama, siasa zimegeuka kama ushabiki wa michezo kutaka kujua Pneumoia ya Hillary na uzito wa ziada wa Trump.

Nani anayejua yaliyoko kwenye akili za magaidi waliotekeleza shambulizi? Kama waliweza kufyatua bomu moja kati ya mawili hata kama ni la kutengenezwa nyumbani tu, maana yake ni kuwa wanajiandaa kwa makubwa zaidi wakati wa uchaguzi, kama hatua za kudhibiti usalama hazitachukuliwa kwa haraka.

Manhattan imejeruhi watu 29 lakini licha ya Meya Bill de Blassio kusema kuwa bado hawana uhakika kama ni ugaidi wa ndani au wa kimataifa na pengine haihusiani na ugaidi, lakini bomu la pili ambalo liliwahiwa kabla ya kulipuka lililotengenezwa na kwa kutumia nyenzo ya jiko la mgandamizo wa hewa, linafanana na lililotumika katika tukio la shambulizi la ugaidi katika michezo ya mbio ndefu jijini Boston mnamo mwaka 2013.

Hiyo ikimaanisha kuwa licha ya nyenzo kubwa za ulinzi za taifa hilo,  bado magaidi wameweza kutumia mbinu za kawaida kabisa zisizotarajiwa kupenyeza madhara, katika hulka ya kawaida ya magaidi kwamba wakishindwa nguvu basi watawaumiza wanaowahusu mahasimu wao hata kama hawahusiki na mapambano kwani wanafahamu kuwa kufanya hivyo ni kuwavuruga kisaikolojia.

Mbinu zinazoonekana kuwa dhaifu ndiyo mtaji wa magaidi na ambazo wagombea urais wa Marekani bado hawajazingatia madhara yake, kwani ni jukumu la Serikali iliyoko madarakani kuhakikisha usalama wa raia wake na kwa tukio la Manhattan vyuma vilivyorushwa na bomu hilo ndivyo vilivyojeruhi wapita njia kwa mlipuko uliotikisa na kuvunja madirisha, kuharibu magari na watu kutaharuki na kukimbia ovyo huku wengine wakirushwa hewani na kutupwa mbali na eneo la kiini cha mlipuko.

Lakini katika hulka inayoonekana ya kutozingatia ugaidi kwa mashiko yake, wagombea wakatoa kauli kuhusu tukio hilo wakilitumia kurushiana vijembe, Trump alisema kuwa ni bomu kabla hata taarifa rasmi za polisi kubainisha ni nini hasa kilitokea akijinadi kuwa lazima kujiimarisha kiusalama maana hatari za mashambulizi ya kigaidi bado zinawakabili Wamarekani. Hillary Clinton alipopewa taarifa rasmi akatoa kauli ya kumnanga Trump kwamba: “nadhani ni busara kusubiri taarifa rasmi za wanausalama kabla ya kutoa hitimisho kuhusu nini hasa kimetoa badala ya kukurupuka!”

Mahnattan ni ujumbe tosha kwa wagombea urais wa Marekani kuwa yoyote kati yao atakayeshinda ana kazi kubwa ya kuhakikisha usalama, kwani licha ya matukio mfululizo ya kigaidi ukiwemo wa ndani kulikumba taifa hilo lakini pengine makosa makubwa ni namna wanavyohesabu madhara yanayotokea.

Iwe bomu la kutengenezwa nyumbani au la kitaalamu lakini maana yake ni kuwa magaidi wanajua kusoma alama za nyakati wakikoleza hila zao kuelekea uchaguzi, kwani kumbukumbu zinaonesha kuwa tangu Januari hadi shambulio la hivi majuzi huko Manhattan, jumla ya waathirika waliouawa inafikia 63 kwa mashambulizi mbalimbali, idadi ambayo si ndogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles