25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 6, 2022

Contact us: [email protected]

Urusi inamsaidia Trump kumshinda Clinton?

trump-putin

NI kawaida kusikia taifa fulani, iwe Ulaya au Asia, Afrika au Amerika ya Kusini ama Amerika ya Kati likilia na Marekani kuingilia mambo yake ya ndani, ikiwamo chaguzi ili kushawishi matokeo inayotaka.

Nyingi ni tuhuma za kweli, tangu wakati wa Vita Baridi hadi hivi karibuni Marekani imeshiriki waziwazi kubadili tawala za nchi nyingine iwe kwa nguvu za kijeshi au ujanja ujanja wa kupenya ndani ya mfumo kufanikisha azma yake hiyo.

Kamwe yenyewe haikuwahi kulia kufanyiziwa kitu kama hicho, lakini katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hali ni tofauti.

Mamlaka za Marekani zinalia na Urusi kuwa inataka kushawishi matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu kwa ajili ya mgombea ambaye inamtaka.

Wasiwasi huo unatokana na mashambulizi ya hivi karibuni ya mtandaoni dhidi ya mifumo wa takwimu za uchaguzi wa Marekani katika majimbo mawili na dhidi ya chama cha siasa.

Licha ya hofu ya jumla ya kuingizwa kwa ushawishi wa Urusi kunakolenga pia kuidhoofisha Marekani, kambi ya Clinton na chama chake cha Democratic ina wasiwasi zaidi kutokana na kuwa walengwa zaidi.

Kwa mujibu wa vyombo vya usalama nchini humo, kundi la intelijensia la Urusi lilikuwa chanzo cha mtandao wa Wikileaks kumwaga maelfu ya barua pepe za chama hicho kwa lengo la kushawishi mwelekeo wa uchaguzi huo.

Kundi hilo liliiba maelfu ya ujumbe wa siri na kuuchapisha wakati Democratic wakijiandaa kumpitisha Clinton kuwa mgombea wao wa urais Julai, mwaka huu.

Miongoni mwao ni pamoja na barua pepe 20,000 zilizoibwa kutoka Kamati ya Taifa ya Chama cha Democratic.

Mkuu wa kamati hiyo, Amy Dacey, alijiuzulu baada ya barua pepe hizo kuonesha mapendekezo ya chama hicho kumuunga mkono Clinton dhidi ya Bernie Sanders, waliyechuana kuwania kuiwakilisha Democratic.

Kuachia ngazi kwa Dacey kulimfanya awe mtu wa pili baada ya mwenyekiti wa wanawake wa chama hicho, Debbie Wasserman Schultz naye kujiuzulu kwa sababu kama hizo.

Ufichuzi umeendelea kuwagusa wanasiasa wengine, lakini zikimlenga Clinton, ikiwamo madai kuwa amekuwa akimchukia Obama kutokana na kumwangusha katika kinyang’anyiro cha uteuzi ndani ya Democratic mwaka 2008.

Hiyo ni mifano michache tu kati ya mingi, kwani barua pepe zaidi zikimhusu Clinton ikiwamo madudu aliyofanya akiwa waziri zinatarajia kuanikwa baadaye mwezi huu huku tarehe ya uchaguzi mkuu-Novemba 8 ikikaribia.

Hali hiyo, inaonekana kumfurahisha Trump, ambaye alikwenda mbali zaidi akiwataka wahalifu hao wa mtandaoni kuzidisha mashambulizi dhidi ya mpinzani wake huyo.

Licha ya kauli hiyo kulaaniwa, Trump hakuonekana kujali, ndiyo maana hivi karibuni ametoa kauli nyingine mbili zinazofanana nayo, safari hii zikihusu usalama wa Clinton ikiwamo kutaka walinzi wake wanyang’anywe silaha ili ‘akione cha moto.’

Tuhuma za uhalifu mtandaoni dhidi ya Marekani zinamwendea Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ambaye Trump hasiti kumsifu kwa kuwa kiongozi imara, kitu kinachomfurahisha mno Putin. Ni nadra kwa wanasiasa wanaojitambua wa Marekani kufanya hivyo!

Mamlaka husika tayari zinachunguza udukuaji huo wa mawasiliano dhidi ya Kamati ya Taifa ya Democratic na Kamati ya Kampeni za Kibunge ya Democratic pamoja na mfumo wa uchaguzi.

Ijapokuwa Putin amekana Moscow kuhusika au kuwa na uhusiano na wahalifu hao, hakukataa kama wanatokea Urusi.

Kwa sababu hiyo, kitendo cha wadukuzi hao wa mawasiliano kujikita kuushambulia upande mmoja kinatia shaka.

Kwanini wahalifu hao wa kipindi hiki wasiilenga Urusi na kwingineko na bali Marekani?

Kwanini walenge upande mmoja tu wa kisiasa nchini humo na mashambulizi kutokea kipindi hiki, ambacho kampeni za urais zimepamba moto?

Maswali hayo yanayoaminisha wengi uhusika wa Kremlin kuilenga Democratic hayakumfanya Trump akose la kusema.

Wakati akiitetea Urusi kuwa hadhani kama inahusika na uhalifu huo, anasema ni kazi ya Democratic kutafuta mapema kisingizio cha kushindwa au kutaka kumchafua wakati huu wa kampeni kuwa anahusika nao.

Alisema hayo wakati akizungumza na Mtandao wa Habari wa RT America, wenye ubia na Mtandao wa Russia Today, unaoungwa mkono na Serikali ya Urusi.

Lakini Waziri wa Ulinzi Marekani, Ash Carter alitoa onyo kwa Moscow wiki iliyopita wakati akiwa Ulaya.

“Hatutapuuza jaribio lolote la kuingilia mchakato wetu wa demokrasia,” Carter alisema.

Alipoambiwa baadaye atoe ufafanuzi wa kauli hiyo, Carter alisema kwamba alikuwa akirejea matumizi ya Urusi ya mashambulizi mtandaoni ili kuingilia masuala ya ndani ya mataifa.”

Kunasa barua pepe za watu na taasisi binafsi ni kitu kimoja na kuingilia mifumo ya uchaguzi wa majimbo ni kitu kingine, kwani kinaweza kukwaza uhalali wa uchaguzi wa Novemba 2016.

Kwa sasa maofisa wanachunguza kiwango cha ushiriki wa Urusi katika uingiliaji wa uchaguzi huo.

Mwezi uliopita Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) lilituma tahadhari kuwaonya maofisa wa majimbo kuimarisha usalama wa mifumo yao ya uchaguzi kutokana na uwapo ushahidi wadukuzi kutoka Urusi waliingilia mifumo ya data ya majimbo mawili.

FBI haikutaja majimbo hayo, lakini tovuti za uchaguzi za majimbo ya Illinois na Arizona zimekumbana na mashambulizi yaliyoshuhudia sehemu za tovuti hizo zikifeli kufanya kazi ya uandikishaji wapiga kura.

Bila kujali iwapo Urusi au Warussia walishambulia mifumo ya chama cha siasa, nini itakuwa shabaha ya Putin kufanya hivyo? Ziko nyingi kwa kuangalia kiwango cha uhasama wake na utawala wa Democratic.

Putin ni wazi si shabiki wa Hillary Clinton, ambaye wakati akiwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani walishambuliana vikali hadharani.

Lakini pia licha ya kuonekana kuungwa mkono na Trump au yeye kumuunga mkono bilionea huyo kama alivyowahi kukaririwa akisema ‘yu mwenye kipaji ambaye nadhani nitafanya kazi naye vyema,’ Putin hayuko salama kwa mgombea huyo wa Republican.

Naam, Putin yu salama zaidi mikononi mwa Clinton, anayetabirika kuliko Trump asiyetabirika.

Trump anaweza kumtetea Putin kwa sasa, lakini pia bado tabia yake ya uropokaji na ukinyonga anaouonesha katika masuala mbalimbali ya kisera, inamaanisha wakati wowote anaweza kumgeuka Putin.

Kuathiri chaguzi kwa njia zozote zile si kitu kipya nchini Marekani.

Inadaiwa ukoo wa Rais wa 35 wa Marekani John F. Kennedy ulipora uchaguzi wa mwaka 1960 katika majimbo ya West Virginia na Illinois.

Al Gore, aliyekuwa makamu wa Rais wakati wa utawala wa Bill Clinton, huenda alishinda urais dhidi y George W Bush mwaka 2000 iwapo Mahakama ya Juu Marekani isingeingilia kati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,606FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles