MANGULA ATANGAZA PANGA JIPYA CCM

0
822
Makamu wa Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, akihutubia viongozi wa chama hicho kutoka katika mashina, kata na wilaya za Dar es Salaam jana. Picha na Deus Mhagale.
Makamu wa Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, akihutubia viongozi wa chama hicho kutoka katika mashina, kata na wilaya za Dar es Salaam jana. Picha na Deus Mhagale.

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

KWA mara nyingine tena, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza  kuwafukuza wanachama wake wasaliti waliosababisha kishindwe Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi kwa makosa ya makusudi.

Uamuzi wa CCM kuwafukuza makada wake kwa kosa la usaliti, unakuja wakati Machi, mwaka huu chama hicho kilimfukuza kigogo wake ambaye alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) CCM, Sophia Simba.

Mbali na Sophia, makada wengine waliofukuzwa ni pamoja na wenyeviti wa mikoa mine; Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga), Ramadhan Madabiba (Dar es Salaam) na Christopher Sanya (Mara).

Wengine waliofukuzwa kwa makosa hayo hayo ni wajumbe wa NEC, Ally Sumaye wa Wilaya ya Babati Mjini na Mathias Manga wa Wilaya ya Arumeru.

Pia wenyeviti wa wilaya wa chama hicho, Omari Awadhi (Gairo), Ally Msuya (Babati Mjini), Makolo Laizer (Longido) na Salumu Madenge (Kinondoni) nao walifukuzwa.

Akizungumza jana katika hafla ya kumpongeza Rais Dk. John Magufuli baada ya kuzuia mchanga wa madini (makinikia), iliyoandaliwa na wanachama wa chama hicho wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Phillip Mangula, alisema katika  kikao kilichopita cha Halmashauri Kuu Taifa kiliteua timu ya wajumbe walioagizwa kufanya uchunguzi katika mikoa mitano iliyoshindwa katika uchaguzi uliopita.

Mangula alisema mikoa iliyoteuliwa kufanyiwa uchunguzi ili kubaini endapo kutakuwa na makosa ya makusudi ama bahati mbaya ni Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Mbeya na Kagera.

“Halmashauri Kuu ya Taifa iliyopita ilitutuma tukaangalie nini kilifanya tupoteze majimbo, hasa katika sehemu ambayo haina hata mbunge mmoja maana sehemu kama hiyo hakuna viongozi.

“Wiki iliyopita nilikuwa Mbeya kuangalia waliojiangusha na nimewapata, sasa baada ya hapa unapaswa kuchagua moja kati ya haya, uturudishie kadi yetu ama usigombee. Lakini ngoja ninyamaze nisije nikachafua hali ya hewa,” alisema.

Mangula alisema kama kuna kiongozi anajijua alishiriki katika mchezo mchafu uliosababisha kukiangusha chama hicho, asichukue fomu ya kugombea.

“Ukijijua ulishiriki bora usichukue fomu, afadhali ughairi maana jina lako likifika kwetu sisi hapiti mtu na hakuna atakayekatwa bila kuhojiwa, tutamuweka kitimoto na kumsomea mashtaka yake ili ajijitetee na sio atoe utetezi wa chuki, tutamtaka ajibu hoja,” alisema.

Pia alisema mwaka juzi kulikuwa na mechi kali na CCM kazi yake ilikuwa kuangalia wachezaji walikuwa wapi dhaifu au  waliteleza, lengo likiwa ni kujipanga na kuhakikisha mwaka 2019 makosa hayajirudii.

“Kama umeuza mechi ama umeachia goli unatarajia tukupange tena mchezo ujao, aliyeonyesha udhaifu achana naye kabisa, nilizunguka majimbo yote Dar es Salaam, tukapinga kwa maana usiposhinda unaondoka,” alisema.

Mangula alisema wachezaji wote walioachia magoli kwa makusudi ama bahati mbaya au kwa kununuliwa ili auze timu hawawezi tena kutumika kuwahujumu katika uchaguzi ujao.

“Tunapanga timu mpya, hatuwezi kwenda na watu wenye makovu ya kujiangusha, kwenye kijiwe chetu kile kama unajijua uliuza mechi hapiti mtu pale, siwafichi nasema kweli,” alisema.

Mangula alisema falsafa hiyo inapaswa itumike pia kuanzia ngazi ya mashina na kuwaagiza viongozi hao kutokubali kuongozwa na watu waliojiangusha katika uchaguzi kwa makusudi.

“Nitawashangaa sana, na nyinyi nitawashangaa mkirudisha watu wa namna hiyo,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here