MATUKIO TISA YATIKISA NUSU MWAKA

0
758

Na AGATHA CHARLES – Dar es Salaam

MWAKA huu uko mbioni kugawanyika baada ya Juni kuingia, huku kukiwa na matukio makubwa yaliyotikisa nchi na kuacha alama isiyofutika kwa baadhi ya watu.

Katika matukio hayo yapo yaliyotikisa kisiasa, kielimu, kiuchumi na kisaikolojia.

Matukio hayo ambayo idadi yake inafika tisa, yalisababisha mtikisiko na hata kujadiliwa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya ndani na kimataifa.

DAWA ZA KULEVYA

Moja ya tukio lililotikisa katika kipindi hiki cha nusu ya mwaka huu ni sakata la dawa za kulevya ambalo lilishika kasi katika Mkoa wa Dar es Salaam na kusababisha baadhi ya waliodaiwa kuhusika kwa namna moja ama nyingine kutajwa hadharani na kutakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano.

Orodha ya kwanza ya majina ya wanaodaiwa kujihusisha na matumizi au biashara ya dawa za kulevya, ilitolewa Februari 2, mwaka huu na kujumuisha askari zaidi ya 10 wa Jeshi la Polisi na wasanii, akiwamo aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu, wasanii wa filamu na muziki wa kizazi kipya, wakiwamo Khaleed Mohamed (TID), Winfrida Josephat (Recho), Khery Sameer (Mr Blue), Hamidu Chambuso (Dogo Hamidu), Babuu wa Kitaa na Rashid Makwiro (Chid Benz).

Majina hayo yalitajwa hadharani na Mkuu wa Mkoa, ambaye katika awamu ya pili alitaja majina 65 yaliyohusisha wanasiasa, viongozi wa dini na wafanyabiashara, wakiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan.

Hatua ya kiongozi huyo kuendelea kutaja majina hadharani, hususani yale ya vigogo, ilitikisa si Dar es Salaam tu bali maeneo yote nchini, ambako suala la dawa za kulevya lilijadiliwa kwa uzito na upana wake.

Hata hivyo kitendo cha kutaja majina hadharani kilikosolewa na wanasiasa kuwa ni kinyume na haki na utaratibu kwa kuwa kinawachafua watu kabla ya kupatikana na hatia kisheria.

Kutokana na hilo, orodha ya awamu ya tatu ya majina 97 iliyokuwa itajwe Februari 13, mwaka huu ilikabidhiwa kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), William Sianga, anayeishughulikia kimyakimya.

 BASHITE

Jina la Daud Bashite liliibuka baada ya sakata la dawa za kulevya kukolea.

Miongoni mwa walioliibua ni pamoja na Askofu Gwajima aliyedai kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa akitumia jina la bandia badala ya jina hilo alilodai kuwa ndiyo halisi.

 CLOUDS, NAPE

Machi 19, mwaka huu, picha zilisambaa katika mitandao ya kijamii zikimwonyesha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akiingia ndani ya Kituo cha Clouds Media Group akiongozana na askari wenye silaha.

Kitendo hicho kilimwibua aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, aliyeunda kamati ya saa 24 ili kuchunguza tukio hilo.

Baada ya Nape kuunda kamati na kupokea ripoti yake, aliondolewa katika nafasi yake na saa chache baadaye aliitisha mkutano wa waandishi wa habari, lakini ulizuiliwa na alitishiwa kwa bastola na mtu ambaye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alikanusha kuwa hakuwa askari polisi.

MAUAJI KIBITI

Tukio jingine lililotikisa ni mauaji ya viongozi wa kisiasa na askari katika wilaya za Rufiji, Ikwiriri na Kibiti mkoani Pwani.

Mauaji hayo yalianza tangu Mei, mwaka jana na kuendelea kushamiri mwaka huu na kwa kipindi kifupi tu takriban watu 38 waliuawa wakiwamo askari polisi.

Miongoni mwa matukio hayo ni lile la Aprili 14, mwaka huu ambalo askari wanane waliuawa, ikiwa ni siku chache baada ya askari kuwaua kwa risasi wanaume watatu waliovalia baibui.

Tukio la hivi karibuni ni lile la Juni 9, mwaka huu katika Kijiji cha Nyamisati wilayani Rufiji, ambako watu watatu wanadaiwa kuuawa na maiti zao hazijulikani zilipo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, akiwa Morogoro alisema mambo yanayotokea katika matukio ya mauaji ya mfululizo maeneo hayo hayazungumziki hadharani kutokana na sababu za kiusalama. 

VYETI FEKI

Aprili, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alimkabidhi Rais Dk. John Magufuli orodha ya watumishi wa umma wenye vyeti feki.

Orodha hiyo ilibeba zaidi ya majina 9,000 na ilitikisa watumishi wa ngazi mbalimbali serikalini wakiwamo walimu na sekta ya afya.

Watumishi wengi muhimu wa sekta ya afya walikumbwa na dhahama hiyo ya vyeti feki, huku Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ikibaini watumishi 134 kughushi vyeti na wengine 38 kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mshipa (MOI).

AJALI YA WANAFUNZI

Mei 6, mwaka huu ilitokea ajali ya kusikitisha iliyosababisha simanzi kwa taifa na kutikisa vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.

Katika ajali hiyo iliyohusisha basi la wanafunzi wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ya mkoani Arusha lililotumbukia katika korongo eneo la Marera, Rhotia wilayani Karatu na kusababisha vifo vya watu 35, wakiwamo wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja.

Ajali hiyo iliripotiwa pia na vyombo vya nje ya nchi kama BBC, CNN na VOA.

Wanafunzi watatu kati yao walinusurika na kwa sasa wanaendelea na matibabu nchini Marekani na inaelezwa kuwa afya zao zinazidi kuimarika.

MABADILIKO CCM

Machi, mwaka huu, Mkutano Mkuu maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulipitisha mabadiliko ya Katiba ya chama hicho yenye lengo la kuboresha na kufanya mfumo wake kuwa wa manufaa kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.

Katika mkutano huo, pia CCM ilichukua uamuzi mgumu wa kuwafukuza uanachama makada wake, akiwamo aliyekuwa mbunge wa viti maalumu na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba na waliokuwa wenyekiti wa chama hicho wa mikoa, Ramadhani Madabida (Dar es Salaam), Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga) na Christopher Sanya (Mara), huku makada wengine wakipewa onyo.

MAKINIKIA

Machi, mwaka huu, Rais Magufuli alizuia makontena zaidi ya 200 kwenye Bandari ya Dar es Salaam ili kuchunguza mchanga wa madini (makinikia) uliokuwa unasafirishwa nje ya nchi kwenda kuchenjuliwa, ukiwa ni mali ya Kampuni ya Acacia Mining Plc ambayo ni mshirika wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation.

Baada ya zuio, Rais Magufuli aliteua kamati mbili kuchunguza makinikia hayo, huku ya kwanza iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma iliyoundwa na wanasayansi ilibaini kiasi kikubwa cha madini yanayoibwa kupitia mchanga huo.

Kamati ya pili iliyoongozwa na Profesa Nehemia Osoro, ilibaini nchi kupata hasara ya zaidi ya Sh trilioni 100 ambazo zingepatikana kupitia usafirishaji wa makinikia hayo, huku sheria nyingi za madini zikikutwa na kasoro inayotoa upenyo wa wawekezaji kutorosha madini.

Baada ya ripoti hizo kuwasilishwa, wiki hii Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Profesa John Thornton, alifika nchini na kufanya mazungumzo na Rais Mafuguli na kukubaliana kukaa meza ya mazungumzo ili kupata mwafaka wa jambo hilo.

UHABA WA CHAKULA

Mwanzoni mwa mwaka huu, Serikali ilisema bungeni kuwa kuna uhaba wa chakula katika halmashauri 55.

Jambo hilo lilipewa nguvu na matokeo ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza uliosema uhakika wa chakula umepungua katika vipindi ya Septemba, mwaka jana na Februari, mwaka huu.

Upungufu huo ulielezwa kuwa ni kutoka asilimia 45 Septemba, mwaka jana hadi kufikia asilimia 65 Februari, mwaka huu.

Uchunguzi ulionyesha kuwa Desemba, mwaka jana kilo moja ya mchele ilinunuliwa kwa Sh 1,800 lakini hivi sasa inapatikana kwa hadi Sh 2,500.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here