23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MALECELA ASIMULIA MACHUNGU ALIYOPITIA

Na MWANDISHI WETU-DODOMA


WAZIRI Mkuu na Makamu wa Rais wa zamani, John Malecela, amefanya ibada ya shukrani na kueleza machungu aliyopitia, ikiwemo kufanyiwa upasuaji mara kadhaa wa mwili wake.

Kutokana na hali hiyo, alisema haamini ni kwa namna gani Mungu alivyomtendea miujiza ikiwemo ya kuendelea kuwa hai hadi sasa.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa baada ya ibada ya shukrani kwa Mungu, huku akiongozana na familia yake, wabunge, wazee wa Dodoma na watu maarufu kwa ajili ya kushukuru kanisani kutokana na afya yake kuimarika.

Alisema alipitia katika shida kubwa ambayo awali hakuwa anaijua, lakini ghafla alijikuta akipasuliwa mwili wake na kufumuliwa zaidi ili kuurudisha katika hali yake ya awali.

“Kwanza naamini hakuna binadamu ambaye aliwahi kufumuliwa mwili wake kama ilivyotokea kwangu mimi kati ya wote waliojaa ndani ya kanisa hili, nasema ni Mungu pekee tu na wala si kitu kingine,” alisema Malecela.

Alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kila hali kwani ndiye anayewezesha kila jambo na bila mkono wake hali ingekuwa ni ngumu zaidi kwake.

Akizungumza wakati wa kutoa neno ya shukrani kanisani, mtoto mkubwa wa Malecela, Dk. Mwele Malecela, alisema mwanasiasa huyo mkongwe alipitia katika vipindi vigumu zaidi katika afya yake.

Alisema baba yake alifanyiwa upasuaji mkubwa mara tatu; tatizo la moyo alifanyiwa upasuaji mara mbili na kisha akapasuliwa tena kwa tatizo la mgongo.

“Yote hayo yalifanyika katika kipindi cha miaka michache, leo (jana) hii tunapomuona mzee anaimarika na kuwa na afya njema, kwetu sisi ni jambo la kushukuru sana kwa Mungu na ndiyo maana tumeona tuje tuseme asante Mungu,” alisema Dk. Mwele.

Awali Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk. Dickson Chilongani, alisema hakuna mtu aliye mkubwa mbele za Mungu na wala hakuna mwenye cheo cha kumshinda Mungu.

Alisema jambo kubwa ni kwa kila mmoja kuendelea kujishusha na kunyenyekea mbele za Mungu wakati wote ili Mungu awe zaidi ya wote maana ndiye mgawaji mwema.

Kutokana na hali hiyo, Askofu huyo aliwataka Watanzania kuendelea kuilinda amani ya Taifa ili iweze kudumu na kuliepusha kuingia katika machafuko kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani.

Kuhusu Malecela, alimshukuru kwa uamuzi wake pamoja na michango mikubwa aliyotoa ikiwemo kusaidia ujenzi wa Kanisa katika Kijiji cha Chinangali II, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya shukrani zake mbele za Mungu.

Pamoja na hali hiyo, jana aliongoza utoaji wa sadaka kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya utumishi katika kanisa hilo lililoko kijijini hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles