24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

MAKOPO MAWILI YA SODA HUONGEZA HATARI MARADHI YA MOYO

WATU wenye tabia ya kunywa makopo mawili ya soda kwa siku wana uwezekano maradufu wa kufa kutokana na maradhi ya moyo, utafiti mpya umeonya.

Hata hivyo, watafiti hawakupata matokeo kama hayo lilipokuja suala la ulaji wa vyakula vyenye sukari.

Watafiti wanaamini utofauti huo baina ya vinywaji na vyakula vya sukari katika kusababisha vifo unatokana na ukweli kuwa kwa vinywaji vya sukari; Sukari hutiririka mwilini kirahisi pasipo kizuizi ilhali vyakula vya sukari kasi ya mtiririko wake hupunguzwa kutokana na uwapo wa mafuta na protin katika vyakula.

Utafiti huo mpya kutoka Chuo Kikuu cha Emory nchini Marekani ni wa karibuni zaidi katika mlolongo wa tafiti zinazoweka wazi hatari mbaya za afya kutokana na vyakula vilivyoingizwa utamu wa sukari kama soda, ambayo mauzo yake duniani yamekuwa yakizidi kuporomoka.

Tafiti za nyuma ziliona uhusiano baina ya sukari iliyoongezwa na unene na maradhi mengine mbalimbali sugu, lakini ni wachache walioweza kuangalia uhusiano baina ya sukari iliyoongezwa na vifo.

“Kulikuwa na maeneo mawili, tulitaka kufahamu.

“Kuongeza sukari kunachagiza zaidi hatari ya kifo kutokana na maradhi ya moyo au visababishi vingine, na iwapo ni hivyo, Je, kuna tofauti ya hatari baina ya vinywaji vitamu vya sukari na iwapo kuna tofauti ya hatari baina ya vinywaji sukari na vyakula sukari?” alihoji mtafiti Dk. Jean Welsh, Profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Emory kilichopo katika Jiji la Atlanta jimboni Georgia.

Watafiti wakiongozwa na Dk. Welsh walichambua data za watu 17,930 wazima weusi na weupe wenye wastani wa umri wa miaka 45. Watu hao walifuatiliwa kwa karibu miaka sita.

Walikadiria kuwa suala la matumizi ya vyakula na vinywaji kwa kutumia swali la mara kwa mara la chakula.

Katika utafiti, vinywaji viliwekwa utamu wa sukari ikiwamo soda na vinywaji vya matunda. Wakati vyakula vya sukari kama vile keki, peremende na vyakula vilivyowekwa sukari vya kifungua kinywa pamoja na vyakula ambavyo vina kalori zenye vitamu kama vile sukari zilizoongezwa.

Haikuweza kujulikana iwapo ‘diet soda’ zilihusishwa katika utafiti huu, lakini vinywaji hivyo pia vina utamu uliotokana na sukari haribifu.

Uchaguzi pia uliangalia rekodi za visababishi vya vifo kwa kuchambua sababu ya vifo hivyo.

Ilibainika kuwa watu waliotumia zaidi vinywaji vya sukari waliongeza uwezekano wa hatari ya vifo kutokana na maradhi ya moyo kama vile shambulio la moyo, moyo kushindwa kazi na visababishi vingine.

Lakini pia waliotumia ‘ounces’ 24 – sawa na makopo mawili ya soda – au vinywaji vingine zaidi vya sukari kila siku walikuwa na uwezekano wa mara mbili ya kufa kwa maradhi ya moyo kulinganisha na wale waliotumia chini ya ounce moja.

Matokeo hayo yalipatikana wakati yalipohusisha vigezo kadhaa ikiwamo kipato, utaifa, elimu, historia ya uvutaji sigara na shughuli za kimwili.

Wakati watafiti pia walipodhibiti sababu nyingine zinazofahamika kuwa hatarishi kwa maradhi ya moyo kama vile matumizi ya jumla ya kalorie, shinikizo la juu la damu na uzito wa mwili, matokeo yalibakia kama yalivyo.

Hata hivyo, hawakuona ongezeko lolote la hatari ya kifo kwa matumizi ya vyakula vya sukari.

Wanaamini kuwa hiyo ni kutokana na namna vinavyovunjwa vunjwa mwilini kwamba vinywaji vya sukari havina virubishi vingine vyovyote na mwili utakabiliana ghafla na mtiririko wa sukari wakati vyakula vya sukari hutolewa taratibu zaidi.

“Kiwango cha matumizi ya vinywaji vya chakula kimetokana na sababu kwamba vina virutubisho vichache na kusababisha mtiririko wa kasi wa sukari inayohitaji kupitia mchakato wa uvunjikaji na uundaji wa kemikali mwilini yaani ‘metabolism,’ watafiti waliandika.

“Wakati watu wanapotumia sukari katika vyakula, mara nyingi huwa kuna virutubisho vingine kama vile mafuta au protin, ambazo husaidia kupunguza kasi ya mchakato wa ‘metabolism’ na ndiyo maana kuna matokeo tofauti baina ya vyakula na vinywaji vya sukari,” waliongeza.

Tafiti za nyuma zilihusisha vinywaji laini vyenye sukari na ongezoko la kuibua hali ya usugu wa afya.

Utafiti wa mwaka 2014 uliochapishwa na Jarida la Utabibu la JAMA, ulibaini kuwa watu waliotumia zaidi ya asilimia 25 ya kalori kwa siku kama sukari iliyoongezwa walikuwa na uwezekano wa mara mbili zaidi ya kufariki dunia kutokana na maradhi ya moyo kama wale ambao mlo wao ulihusisha chini ya asilimia 10 ya sukari iliyoongezwa.

Kadhalika ripoti iliyochapishwa na Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani mwaka 2013, ilifichua kuwa karibu vifo 180,000 vinavyohusiana na unene duniani vilitokana na matumizi ya vinywaji vya sukari.

Katika utafiti wa sasa watafiti walisema matokeo waliyobaini yanapaswa kuwachochea madaktari kuwauliza wagonjwa wao kuhusu matumizi ya vinywaji vya sukari wakati wanapozuru hospitali ili kufungua milango kuhusu mlo ambao unaweza kufanywa ili kupunguza hatari.

“Tunajua iwapo watoaji wa huduma za afya hawatowauliza wagonjwa kuhusu staili zao za maisha zinazohusiana na unene na maradhi sugu ya maisha, wagonjwa watafikiria kwamba hilo si muhimu,” Dk. Welsh alionya.

Alisema kuwauliza wagonjwa kuhusu matumizi yao ya vinywaji vya sukari kuna thamani kubwa kwa afya zao.

Kauli hiyo inakuja wakati Jarida la Boys Life, liliwahi kuwatafiti wasomaji wake na kugundua kuwa asilimia 8 ya wasomaji wake wanakunywa soda 8 au zaidi kwa siku.

Aidha lilifanya utafiti juu ya matumizi ya vinywaji hivi hospitalini nchini Marekani na kugundua zaidi ya asilimia 85 ya wagonjwa wanahudumiwa chakula pamoja na vinywaji hivi baridi.

Kwa kiasi kikubwa, kuna imani miongoni mwa watu wengi kuwa vinywaji hivi vinaweza kuwa mbadala wa mahitaji ya mwili kwa maji.

Imedhaniwa kuwa kwa sababu tu vinywaji hivi vina maji, mwili utakuwa umekamilishiwa mahitaji yake ya maji, dhana ambayo ni potofu.

Kuongezeka kwa matumizi ya soda zenye kafein, kunaunda vyanzo vingi vya matatizo ya kiafya kwenye jamii zetu.

Imani hii potofu kwamba vimiminika vyote ni sawa na maji kwa mahitaji ya mwili, ndiyo chanzo kikuu cha magonjwa kwa mwili wa binadamu ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzito kupita kiasi, wataalamu wanasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles