28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

NAMNA YA KUSHUGHULIKIA MASHINDANO YA NDUGU WANAOFUATANA

Na CHRISTIAN BWAYA


WATOTO wanaofuatana kwa uzao mara kwa mara hujikuta kwenye mazingira ya kushindana. Mtoto wa kwanza kwa mfano, anakuwa haelewani na mdogo wake ambaye kimsingi anataka na yeye anaonekane anaweza.

Kwa upande wa pili, ujio wa mtoto wa pili kwa namna fulani humfanya mtoto wa kwanza awe na wasiwasi na usalama wa nafasi aliyonayo kwa wazazi. Tunafahamu mtoto mchanga anapozaliwa hupata kila aina ya uzingativu unaomfanya mkubwa ‘asahaulike’ kwa muda. Hali kama hii huweza kumfanya mkubwa asiwe na amani kwa kuhisi mdogo anatishia nafasi yake.

Wakati mwingine jinsia inaweza kuwa sababu. Mtoto wa kiume anaweza kuwa na shida na mwenzake wa kike kwa sababu tu anaonekana kuelewana zaidi na baba.

Pia kuna umri, mtoto wa miaka mitano anaweza kucheza na mwenzake wa miaka nane lakini mmoja anapofikisha miaka 13 anayefuata akawa na miaka 10 wanatengana. Shughuli zao zinakuwa tofauti na yule mdogo anakuwa mshindani kwa mkubwa wake.

Mashindano kati ya ndugu ni ile hali ya mtoto kutumia muda mwingi kujilinganisha na mwenzake kwa minajili ya kutaka kuonekana kuwa bora kuliko mwenzake. Shauku ya kutaka kuwa bora humfanya amlalamikie mwenzake, amsingizie na kumbebesha lawama; amwonee wivu pale mwenzake anapoonekana kufanya vizuri au kupata upendeleo.

Pamoja na sababu hizo, kubwa ni mtazamo wa wazazi kwa watoto. Kuna mazingira ambayo sisi wazazi huonesha upendo kwa baadhi ya watoto kwa sababu ya nafasi zao kwenye familia, umri wao, jinsia zao, tabia zao na wakati mwingine kufanya tunayoyataka.

Ingawa tabia ya mashindano kati ya watoto wanaofuatana inaweza kuwa sehemu ya utoto tu, hatua zisipochukuliwa, upo uwezekano wa ndugu hawa kuendelea kushindana na hata kuwa mahasimu ukubwani.

Namna moja ya kushughulikia tabia hii ya ushindani kwa watoto ni kutokuwalinganisha. Kila mtoto ana upekee wake. Kutaka watoto wote wafanye kama anavyofanya mmoja wao ni jambo lisilowezekana. Weka utaratibu unaomwezesha kila mtoto kufikia malengo yake mwenyewe bila kulazimika kufanya kama mwenzake.

Kadiri inavyowezekana, ondoa mazingira yanayomfanya mtoto ashindane na mwenzake. Wafanye watoto washirikiane. Pia, ni vyema watoto wazoeshwe kumaliza tofauti zao bila kulazimika kuleta mashtaka kwa wazazi. Hili linaweza kuwa gumu, lakini kidogo kidogo watoto wanaweza kujifunza kuelezana hisia zao, kuombana msamaha na kupanga namna njema ya kuhusiana.

Kama tulivyoona, ujio wa mtoto mchanga unaweza kuwa chanzo cha matatizo. Pamoja na kumfurahia mtoto mchanga aliyezaliwa, heshimu hisia za mtoto mkubwa. Mabadiliko madogo ya namna unavyojali mambo yake yanaweza kumfanya mtoto akaanza mashindano yasiyo na sababu na kichanga.

Ukweli ni kwamba watoto wana tabia ya kufuatilia mambo madogo ambayo wakati mwingine mzazi anaweza asiyachukulie kwa uzito. Kwa kuwa mtoto anayejisikia kuonewa hataweza kugombana na mzazi mara nyingi atajitetea kwa kujenga ukuta na mwenzake.

Lakini pia, epuka kupuuza hisia za hasira kwa mtoto. Inapotokea mtoto anajisikia kutotendewa haki na mwenzake au na wewe mzazi, usimfanye ajisikie hatia kwa sababu ya hasira. Ukweli ni kuwa hasira haina ubaya kama itadhibitiwa. Mtoto anapoonesha hasira maana yake kuna tatizo hivyo msaidie kulibaini na mlishughulikie.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,307FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles