Makonda awapa ujumbe mawaziri

0
709

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaomba mawaziri wasiwe na haraka ya kufanya ziara katika mkoa wake kwa sasa, hadi atakapokalimisha baadhi ya miradi ya kimkakati aliyoelekezwa na Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumza na wanahabari kwenye eneo la ujenzi wa machinjio mapya huko Vingunguti jijini Dar es Salaam jana, Makonda alisema analiomba Baraza la Mawaziri limpe muda wa alau miezi miwili, kabla ya kufanya ziara katika mkoa huo.

Alisema kwa sasa anawajibika kuhakikisha kuwa miradi yote iliyokuwa aidha imekwama au imechelewa kuanza inapatiwa ufumbuzi wa kiutekelezaji.

“Ninawaomba mawaziri wanivumilie kidogo kwa angalau miezi miwili ndio waje kuutembelea mkoa wangu. Ninaomba nipewe muda wa kufuatilia utekelezaji kwa mujibu wa maelekezo ya Rais (John Magufuli), maana mara nyingine wanaweza kuwa wanapata maneno mengi kwa watu wasio sahihi tofauti na hali halisi,” alisema.

MAELEKEZO

Akiwa katika ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti, Makonda alisema anaridhishwa na kasi inayoendelea ambapo wakandarasi wamefanya kazi usiku na mchana na tayari, tangu ukuanza kwa ujenzi wiki iliyopita wameokoa siku tano.

Alisema tayari wameshajipanga kukamilisha mradi huo wa zaidi ya Sh bilioni 12 ndani ya miezi mitatu na wanatarajia kuunkabisli mwishoni mwa Desemba mwaka huu.

Alisema wakati ujenzi huo ukiendelea, sasa ni wakati wa Manispaa ya Ilala kuangalia namna ya kuijenga kwa hadi ya kisasa barabara inayoingia kwenye eneo hilo la machinjio ya Vinginguti, ikitoke Barabara ya Nyerere ambayo haizidi urefu wa kilometa moja.

Makonda alisema ujenzi wa barabara hiyo kwa sasa ni wa muhimu ili kuifanya iendane na hadi ya machinjio hiyo inayojengwa, kwa kuwa tayari kutakuwa na upanuzi wa bishara ya nyama na kuongeza wafanyabiashara wanaofikisha ng’ombe na wanaokwenda kuchukua nyama.

Aliema suala jingine muhimu ni kuangalia uwezekanao wa kuunganisha kipande cha reli inayofika kwenye machinjio hayo ili kuruhusu uchukuzi kwa kutumia mabehewa ya kisasa ya treni ambayo yatakiwa yakisafirisha nyama kutoka kiwandani hapo kwenda mikoa mbalimbani nchini.

Alisema hatua ya ujezni wa reli kuingia kiwandani hapo ni muhimu kwa kuwa katika nchi zilizoendelea, viwanda vyote vikubwa vimekuwa vikiangalia namna ya kutoa huduma kwa urahisi kwa wateja wake kwa kuhakikisha wanaweza kufika na kuchukua bidhaa bila usumbufu.

 “Tunahitaji haya yote yafanyike kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa wingi wa mifugo Afrika, kwa hiyo kukamilika kwa kiwanda hiki kutasababisha ongezekola mahitaji, kwa hiyo tunaweza kuuza nyama hata nje ya nchi,” alisema.

Agizo jingine la Makonda kwa uongozi wa Manispaa ya Ilala ni kuangalia uwezekano wa kuwalipa fidia ya majengo yao na kuondoa nyumba zaidi ya 20 zilizoko ndani ya eneo la machinjio hayo.

Alisema upanuzi wa eneo hilo ni muhimu kwa kuwa kwa kauangalia ndani ya miaka 10 hadi 20 ijayo shughuli za machinjio hayo zitapoanuka zaidi na kuhitaji eneo la ziada.

“Kwa hiyo, hebu tuangalie namna ya kuwalipa fidia hawa watu ambao nyumba zao zinapakana na eneo hili ili tuwe na eneo pana zaidi la kutiosha muhimili maendeleo ya kiwanda hiki,” alisema.

Alisema kwa sasa uongozi wake unaendelea kufuatilia kwa karibu hatua kwamhatua ukanulishaji wa miradi hiyo ya kimkakati ambayo inatakiwa kukamilika kabla mwaka huu haujamalizika.

Kwa upande wake, mhandisi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wanaojenga mradi huo, Elisante Ulomi alisema ujenzi unaendelea vizuri na kwa kasi, ambapo kwa sasa wanamalizika kurudisha na kushudilia udongo ndani ya msingi.

Alisema ndani ya siku tatu zijazo watamaliza upangaji wa mawe kwenye msingi huo na kufunga nondo, kwa ajili ya kuweka jamvi kwenye msingi wa jengo hilo.

“Ni kwamba hadi kufikia Oktoba 10 tutakuwa tumeshaweka jamvi na kufikia Novemba 20,  jengo la chini litakuwa limekamilika,” alisema.

Naye Meya wa Ilala, Omari Kumbilamoto alisema ujio wa Rais Dk. John Magufuli kwenye eneo hilo la Vingunguti umekuwa wa manufaa kwa kuwa umeibua mkwamo huo na kusababisha kuharakishwa kwa usimamizi na utekelezaji.

Alisema kwa sasa anapokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kuhusu ujenzi wa barabara, reli na suala la kulipa fidia wakazi wanaozunguka eneo hilo kwa ajili ya utekelezaji.

“Tukitoka hapa, tutakaa na wataalamu kujadili namna ya kuyafanyia kazi maagizo haya na kusimamia utekelezaji wake kwa kasi. Ninamuomba Mkuu wa Makoa asiwe na wasiwasi kwa maana sasa nimeamua kuingia mwenyewe sight,” alisema.

Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika eneo la machinjio ya Vingunguti Septemba 16 mwaka huu, ambapo alieleza kusikitishwa kwake na kukwama kwa baadhi ya miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa machinjio hiyo ya  kisasa na uboreshaji wa eneo la Coco Beach.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli alieleza kutoridhishwa na mazingira ya eneo hilo na mradi wa machinjio ya kisasa na kusdma kuwa hakuna kinachofanyika licha ya fedha kukusanywa na kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Jumanne Shauri akitaka kujua fedha zinazokusanywa, kujibiwa kuwa ni Sh milioni 100 kila mwezi.

Baada ya maelezo hayo Rais Magufuli, aliagiza kutokusanywa kwa fedha hizo hadi ujenzi utakapokamilika, kutaka fedha zitoke kwenye vyanzo vingine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here