24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAKINIKIA YAGONGA VICHWA CHADEMA, WABUNGE

KULWA MZEE na AGATHA CHARLES-DODOMA/DAR ES SALAAM

SAKATA la mchanga wa dhahabu (makinikia) limezidi kushika kasi baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vicent Mashinji, kuitaka Serikali kuweka hadharani mikataba yote ya madini huku wabunge nao wakiendelea kulijadili bungeni wakati wa mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2017/2018.

Dk. Mashinji alitoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kutokana na ripoti mbili za kamati ikiwamo ya Profesa Nehemia Osoro zilizoundwa na Rais Dk. John Magufuli kuchunguza usafirishaji wa makinikia nje ya nchi unaofanywa na Kampuni ya Acacia Mining Plc.

Akifafanua zaidi, Dk. Mashinji, alisema Serikali inapaswa kuwajibika kwa kuiongoza vibaya nchi kiasi cha kuporwa rasilimali zake kwa muda wote huku akikitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitafakari kama bado kina uhalali wa kisiasa kubaki madarakani.

“Hili jambo linahitaji umakini kama mtu anaweza akapanda ndege akaja nchini kujadili hili suala lazima ulipe uzito unaostaili. Kila aliyehusika katika kutaasisisha na kurasimisha wizi na uporaji huu awajibike au awajibishwe kwa mujibu wa sheria hata kama ni mkubwa kwa kiwango gani. Pia Magufuli hatofaulu vita hii kama Serikali yake itaendelea na utamaduni wa kutubagua (Chadema) au kutosikiliza sauti za upande wa pili, ni vyema akajua hata Ilani ya chama chake ukurasa wa 26 na 28 haikuzungumzia kabisa hoja za mikataba na sheria za madini kuhitaji kurekebishwa au kuandikwa upya,” alisema.

Pia alisema ajenda ya kupigania na kudai haki, masilahi na matakwa ya Taifa katika kulinda rasilimali yakiwamo madini ni ya Chadema na alisema wanashangazwa na kitendo cha Rais Magufuli kuwaonya watu wenye maoni tofauti katika sakata hilo.

“Rais wakati ametoka kuomba Taifa liwe pamoja katika vita ya kutetea rasilimali zetu, hapo hapo anawaonya watu wenye maoni tofauti tena anatoa maagizo kwa mihimili mingine (kinyume na sheria na misingi ya utawala bora) kushughulikia watu ambao mawazo yao mbadala ndiyo yamesimamia vita hii muda wote, yeye (Rais) na wenzake wa CCM walitetea uwekezaji na wawekezaji hawa kwa kuwatungia sheria zinazowasaidia kutupora na kutia mikataba ya siri,” alisema.

Alisema ili kuwapo na uwazi katika vita hiyo ni vyema Bunge likarudi kuwa mubashara ili wananchi wawaone na kuwajua wabunge ambao ni mawakala wa uporaji rasilimali.

Dk. Mashinji alisema hakuna haja ya kutafuta mchawi kwa sababu CCM ndio imeifikisha Taifa hapa lilipo, mbali na kufanya mabadiliko kwa kuweka uwazi katika mikataba na kubadili sheria, lakini kunapaswa kufumua hali ya kulindana ili kuweka mfumo na taasisi imara.

“Ikiwamo ile ya sekta ya ujenzi, uuzwaji wa nyumba za Serikali, kuuzwa kwa mashirika ya umma na mingine. Lazima tujue majukumu ya kila siku, unapokuwa na kiongozi wa juu kama rais kufuatilia utendaji wa kila siku, nani kahamisha nini, nani kasaini nini, tuko mbali sana kiuchumi, anapaswa atupe dira.

“Nchi inayumba, inashangilia bila kukaa chini na kutafakari kuwa ni sawa tumeibiwa makinikia yenye thamani ya matrilioni yaliyotajwa, hivyo watu wanapaswa kutafakari ikiwa huo ni ukweli au ni kiki za kisiasa,” alisema.

Dk. Mashinji alisema Watanzania wengi wanashabikia lakini hawajui hivyo ni vyema wakaelezwa ukweli kuwa makanikia hayo yana thamani kubwa lakini nchi inapaswa kupatiwa asilimia nne na mwekezaji anabaki na asilimia 96.

Alimuomba Rais Magufuli azitoe hadharani ripoti zote za makinikia kwa sababu kuna maswali mengi wakati wa uchunguzi wa sakata hilo ikiwamo sampuli zilizochukuliwa, utaratibu uliotumika maabara na njia zilizotumika kufikia hitimisho la kiwango cha dhahabu na madini mengine.

“Kuna tofauti kubwa sana kati ya kipimo cha Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) na kipimo cha kamati zile, kuna tofauti ya karibia asilimia 20, sasa kwa sisi tuliosoma kemia tunajua. Waje waseme hadharani, kama ni kweli yana thamani ya Shilingi trilioni 108, tuambiwe tangu tuanze kuchimba tumepata faida gani. “Tuache kushangilia, kisaikolojia jambo ambalo hulijui lazima uweke shaka kidogo,” alisema.

Dk. Mashinji alisema yote hayo ili yawe sawa inapaswa ipatikane Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya Watanzania yaliyokusanywa na iliyokuwa Tume ya Rasimu ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Joseph Warioba.

 

MJADALA BUNGENI

Akichangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali jana, Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige, aliitaka Acacia wailipe Kahama zaidi ya Sh trilioni 2.2.

Maige alisema anapozungumzia mapato ya Serikali kwa mbunge anayetoka Bulyanhulu hawezi kuacha kuzungumzia makinikia.

“Kuna mbunge mmoja humu aliwahi kusema tume nyingi zimewahi kuundwa na hii ya Profesa Abdulkarim Mruma na Profesa Nehemia Osoro ni idadi tu, Tume ya Jaji mstaafu Mark Bomani niliyokuwa mjumbe mmojawapo kazi yetu ilikuwa kufanya mapitio ya sera na sheria kuangalia nchi nyingine wanafanyaje ili tutoe mapendekezo kwa Serikali katika maeneo tusiyofanya vizuri, hatukuwa tunafanya uchunguzi,” alisema na kuongeza:

“Niliwahi kusema Acacia ni fedhuli, hawawezi kuingia katika meza ya mazungumzo bila kuwabana, wameingia katika mazungumzo wakati uchunguzi umefanyika na data zipo za kutosha.

“Wananchi kule ambako makinikia yanatoka wanahoja zao ambapo moja, pamoja na kuibiwa Serikali kuu, Halmashauri Kahama pia tumeibiwa tunadai Shilingi bilioni 795 hadi Shilingi trilioni 2.2 za kodi ya huduma kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka huu na hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Profesa Osoro.

“Wakati mnaingia katika majadiliano mzingatie hoja hizo tunataka fedha za halmashauri tuzipate.”

Naye Mbunge wa Kiteto (CCM), Emmanuel Papian, alisema kabla ya kufanya mazungumzo ya kulipa Sh trilioni 108 ambazo Serikali ilipoteza kwa sababu ya makinikia hayo, waweke mezani kwanza Sh trilioni 35 kwa ajili ya bajeti ya Tanzania kisha waanze mazungumzo.

“Wakikaa na hao wenzetu wajue jinsi gani ya kuwatega ili nchi isiendelee kupoteza katika madini. Rais kwenda nje si vizuri, hao wa nje nao waje Ikulu wainame, kila siku ukienda kuwainamia wanafikiri sisi wajinga,” alisema.

 

Kwa upande wake, Mbunge wa Vunjo, (NCCR -Mageuzi), James Mbatia, alisema haoni kwanini wanaona aibu kuomba radhi Watanzania katika suala la madini, sababu ni mfumo wa uwajibikaji wa pamoja.

“Mwaka 1994 hadi leo sheria ya mikataba ni uwajibikaji wa pamoja, huwezi kusema Serikali ya mwaka 1995 ni tofauti na Bunge hili, kushabikia tu hapa ndani. mwaka 2002 nilienda Zimbabwe kwenye mgogoro wa kiuchumi, vita ya kiuchumi ni mbaya sana, leo hii Zimbabwe haina hata sarafu yake, imeangamia kabisa,” alisema Mbatia.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza, alisema kuna haja Serikali ikazungumza na wawekezaji wote wa sekta ya madini pia kuna mkanganyiko kwa sababu ni Kamati ya Lawrence Masha ya mwaka 2006 na ile ya Jaji mstaafu Mark Bomani ya mwaka 2008 zinaonyesha kwamba Mgodi wa Bulyanhulu ulianza uzalishaji mwaka 2001 wakati Kamati ya Profesa Mruma na Profesa Ossoro zinaeleza kwamba uzalishaji katika mgodi huo ulianza mwaka 1998.

“Taarifa zinakinzana ingawa nataka kuiamini Serikali kwa ripoti ya tume zake lakini naomba tuangalie na kuzihakiki taarifa tulizozitoa na Serikali iende hatua mbele zaidi kuhakiki ili kama tunaenda kwenye mazungumzo twende na watu wasomi, timu na watu wanaoweza kusimamia kitu kilichopo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles