UPELELEZI KESI YA ‘NDAMA’ BADO HAUJAKAMILIKA

0
668

Na MANENO SELANYIKA

-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imeahirisha kesi ya mfanyabiashara maarufu, Shabani Hussein (44) “Ndama mtoto ya Ng’ombe” hadi Julai 20, mwaka huu kwa sababu upelelezi bado haujakamilika.

Shauri hilo lilikuja jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, upande wa mashtaka ukisimamiwa na wakili Shedrack Kimaro, wakati wa utetezi ukiongozwa na mawakili wawili Wabaya Kung’e na Nashon Nkungu.

“Mheshimiwa mshtakiwa aliyeko mbele ya mahakama yako anakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu lakini tunaomba tarehe nyingine kwa sababu upelelezi bado haujakamilika,” alidai wakili Kimaro.

Kwa upande wa utetezi uliwataka Jamhuri kufuatilia upelelezi wa shauri hilo ili kujua kama upelelezi umefikia hatua gani.

Mwanzoni mwa wiki hii Ndama alifanikiwa kutimiza vigezo vya dhamana vilivyomtaka kuwa na wadhamini wawili watakaoweka saini ya maandishi Sh milioni 600 au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Katika mashtaka hayo, Ndama anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014, Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa Kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye Benki ya Stanbic, alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa dola za Marekani 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Shtaka jingine anadaiwa Februari 20, 2014, Dar es Salaam, alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Machi 6, 2014, Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonesha kilogramu 207 za dhahabu kutoka nchini Congo zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.

Aidha, anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi fomu ya forodha yenye namba za usajili R.28092 akionesha kampuni ya Muru imeilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa ambazo zina uzito wa kilogramu 207 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kutoka Congo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here