26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Makampuni yenye ubia na Serikali kubanwa

Dk. Philip Mpango
Dk. Philip Mpango

Na Khamis Mkotya, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameyataka makampuni yote yenye ubia na Serikali kuweka wazi hesabu zao  kuokoa upotevu wa mapato serikalini.

Katika kutekeleza agizo hilo, Dk. Mpango  amemuagiza Msajili wa Hazina (TR) kuyafuatilia makampuni hayo ambayo baadhi  yamekuwa yakidanganya na hivyo kuikosesha Serikali mapato.

Dk. Mpango alitoa agizo hilo jana katika ukumbi wa Hazina Ndogo mjini hapa, baada ya kupokea mfano wa hundi ya Sh bilioni 4.5 ambalo ni gawio lililotolewa na Kampuni ya Mafuta ya PUMA, kutokana na faida ya mwaka 2015.

Kampuni hiyo imeingia ubia na Serikali kwa kila upande ukiwa na asilimia 50, ambako katika kipindi kilichoishia Desemba  mwaka jana, kampuni hiyo ilipata faida ya Sh bilioni tisa, ambayo nusu yake imetolewa kama gawio kwa Serikali.

“Tuna kila sababu ya kumshukuru mbia mwenza amefanya kazi nzuri si tu katika kuliongoza lakini pia hata kwa upande wa huduma, napenda kuwashukuru kwa kuwa mbia wa kuaminika, hizi ndizo zitatuwezesha kama serikali kuwahudumia wananchi.

“Msajili unayo kazi ya kufuatilia huko ambako tumewekeza fedha za wananchi nako tupate gawio ni muhimu sana…mbona sijaona wakifunga biashara?  Wao wako hapa wanasema wanapata hasara lakini kuondoka hawaondoki inawakuwaje?

“Nawataka wabia wetu wawe wazi katika miamala yao, huu ndiyo umuhimu wa kuwa na ubia wa kuaminiana, lakini katika biashara upo, yakija mahesabu unasema umepata hasara haiwezekani,” alisema.

Dk. Mpango pia amevitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi  kubaini mianya ya upotevu wa mafuta bandarini na kuagiza   wote walihusika na upotevu huo wachukuliwe hatua.

“Hili linanikera sana, wizi huu hatuwezi kuendelea na nchi ya namna hii lazima tuchukue hatua.

“Pamoja na kuunda chombo cha kudhibiti upotevu wa mapato, lakini mimi ningependa turudi nyuma, hawa waliokuwa wanatupotezea asilimia tatu  haiwezekani wanaenda wanatamba mtaani tutumie vyombo vyetu tuwatafute haya mafuta yalikua yanaenda wapi?

“Naomba wizara mlisimamie vizuri, vinginevyo wajanja wachache wanafaidika halafu wananchi wanyonge wanalala chini hospitalini.  Nilisema jana (juzi) na leo narudia yeyote anayetukwamisha kwenye maendeleo ni msaliti lazima washughulikiwe bila huruma,” alisema.

Awali, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, aliipongeza kampuni hiyo kwa kutoa gawio hilo. “Mwaka 2014 tulipata gawio la Sh bilioni tatu, mwaka huu tumepata bilioni 4.5 ni matarajio ya Serikali kwa mwendo huu mwakani tunaweza kupata bilioni sita.

“Niyatake makampuni mengine yenye ubia na Serikali ambayo hayatoi gawio yaanze sasa kutoa. Mantiki ya gawio ni kwamba kampuni inafanya kazi na inapata faida, inapokuwa haitoi gawio mantiki yake ni kwamba kampuni inafanya kazi haipati faida,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya PUMA, Dk. Beni Moshi, alisema tatizo la upotevu wa mafuta bandarini limekuwa changamoto kubwa katika sekta ya mafuta nchini.

Kwa mujibu wa Dk. Moshi,    mwaka 2014/2015 kampuni hiyo ilipata hasara ya Dola za Marekani milioni 1.4 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 2.5 kutokana na upotevu huo wa mafuta.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles