28.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Umaskini unavyochochea ndoa za utotoni Tanzania

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

“Sina furaha kabisa na ndoa hii, natamani kutoka lakini kinachonibakisha ni watoto wangu wawili, sitamani tena kuzaa mtoto mwingine nasubiri watoto wangu wakiwa wakubwa niachane kabisa na huyu mwanaume.

“Naendelea kujuta sana kwani ningekuwa hata Daktari wa Watoto sasa hivi kama ningeendelea kuvumilia kazi ngumu na manyanyaso niliyokuwa nayapitia wakati nikiishi kwa Mjomba.

“Kwani nilitumika kuchunga ng’ombe, kulima, kupika na hata kukata majaani ya ng’ombe kila siku iendayo kwa Mungu, lakini hata nilipotoroka kwenda kwa baba yangu Mzazi nikijua naenda kutimiza ndoto zangu kielimu kumbe ndio nilikuwa naenda kuangukia kwenye ndoa licha ya umri wangu kuwa mdogo,”.

Hiyo ni sehemu ndogo tu ya safari nzito aliyoipitia Binti wa miaka 25, ambaye katika makala haya tutampa jina la Rehema Zabroni, ambaye kwa sasa ni mama wa watoto watatu mmoja akiwa ametangulia mbele za haki.

Ilikuwaje

Rehema ambaye anaonekana kuwa na kinyongo moyoni dhidi ya maisha anayoishi na mume wake ni wa pili kuzaliwa katika ya watoto sita kwa mama yake, Stela Ngailo(48) ambaye alizaa na wanaume tofauti.

Kwa mujibu wa Rehema, baba yake anafahamika kwa jina la Zabron Sanga,machungu ya maisha yake yalianza wakati akiwa na umri wa miaka minne tu mwaka 2000 wakati huo wakiishi katika kitongoji cha Lupila kilichoko mkoani Njombe, Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania.

“Hapo tayari na mimi nilikuwa na mdogo wangu wa miaka miwili huku mama yangu akiwa ni mjamzito ila kila mmoja alikuwa na baba yake.Hali ya maisha yetu haikuwa ya kuridhisha sana kwani tulikuwa tunaishi na mama tu,” anasema Rehema.

Rehema anasema ili kutoa nafasi ya matunzo kwa wadogo zake, alilazimika kwenda kuishi na mjomba wake anayemtaja kwa jina moja la Jasanga, katika kijiji cha Ikonda.

“Nilienda kwa mjomba ambaye pia alikuwa akiishi na mke wake(Shangazi) kwa bahati mbaya au nzuri wote hawakuwa na mtoto, hivyo mimi ndio nilikuwa mtoto pekee.

“Maisha yaliendelea kwa siku za mwanzo ambapo nilikuwa nikipatiwa mahitaji muhimu kulingana kwamba nilikuwa tayari nimeshaandikishwa kuanza elimu ya msingi,” anasema Rehema.

Changamoto zikaanza

Rehema anasema kuwa changamoto zilianza wakati akiwa darasa la tatu ambapo hapo alinza kwenda shamba pamoja na kushughulika na mifugo ambayo ni ng’ombe na mbuzi na kufanya vibarua vya kusomba tofari.

“Hiyo ilikuwa ni baada ya mjomba kuniambia kuwa nilitakiwa nijifunze kujitegemea kwa kufanya kazi mbalimbali kutokana kwamba kwetu tulikuwa maskini, hivyo nilivumilia changamoto hizo nikamaliza darasa la saba.

“Bahati nzuri matokeo yalipotoka nilichaguliwa kujiunga na shule ya Sekondari ya Lupalilo,” anasema Rehema.

Hata hivyo, safari ya masomo ya Rehema haikudumu kutokana na kushindwa kumudu ada shuleni.

“Wakati huo serikali ilikuwa bado haijaondoa ada shuleni, hivyo tulikuwa tukilipa Sh 20,000 hivyo muhula wa kwanza Mjomba alinilipia Sh 10,000 lakini mhula wa pili alikataa kwa kile alichosema kwamba sikufanya kazi kwa bidii wakati wa likizo, hivyo akanitaka nitafute fedha ili nijilipie pamoja na michango mingine.

“Nilienda shuleni bila ada lakini nikarudishwa, nilivorudi kumwambia mjomba akaniambia natakiwa kufanya kazi kwa bidii mara mbili zaidi ili niweze kupata hiyo fedha, jambo ambalo lilinishinda,” anasema Rehema.

Maamuzi magumu

Rehema anasema kutokana na changamoto hiyo aliamua kuchukua uamuzi mgumu wa kutoroka na kurudi kwa mama yake kwa lengo lakutaka kumuuliza ni wapi alipo baba yake.

“Baada ya kufika na kumuuliza, alinieleza baba yangu ni nani na alikuwa wapi kwa wakati huo. Nilichukua jukumu la kumtafuta baba yangu lakini nilichokikuta sikukitarajia kwani baba ndiye ilikuwa mwanzo wa mimi kuolewa kabla ya umri wangu.

“Kwanza baba alinikubali kama mwanae na kunirejesha shule iliyokuwa jirani kwa jili ya kuendelea na masomo, lakini niliacha shule sababu ya mateso kutoka kwa mama wa kambo,” anasema Rehema.

Anasema kutokana na manyanyaso ya mama wa kambo alianza kupoteza mwelekeo wa masomo kwani alikuwa akimpiga ikiwamo kumnyima chakula hatua liyompeleka kuacha shule akiwa kidato cha kwanza.

“Nilitoroka na kwanda Njombe mjini kwa kumdanganya mwenye gari kuwa mama yangu atakuwa stendi na ndiye atalipa nauli,baada ya kufika hapo wakati kondakta akishusha mizigo ya abiria wengine nilikimbia bila kuniona,” anasema.

Safari ya ndoa

Rehema anasema akiwa hapo aliingia kwenye moja ya nyumba zilizokuwa wilayani hapo wakati huo haujawa mkoa.

“Nilienda kuomba kazi za ndani na bahati nzuri nilikubaliwa ila sikulipwa mshahara, badala yake nikawa napewa vyakula na zawadi ndogo ndogo kutokana kwamba nami sikuwa na sehemu ya kwenda alafu umri wangu mdogo sikujua kama nilikuwa nanyima stahiki zangu.

“Nilifanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja, baadaye yule mama ambaye ni bosi wangu akatokea kunipenda kutokana na ufanyaji kazi wangu, hivyo akanitaka niolewe na kijana wake, namimi nilikuwa sijui mambo ya ndoa nikijua nikuishi tu vizuri, nikakubali,” anasema Rehema ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16.

Anasema baada yakukubali ombi hilo, mabosi wake hao walimwambia kuwa walihitaji kufika kwa wazazi wake, ambapo aliwapeleka kwa mama yake.

“Baada ya kufika walimpatia mama zawadi na wao wakaeleza hitji lao, na wakakubali niolewe kwa mahari ya Sh 500,000 fedha ambayo walilipa siku hiyohiyo, baadae tulirejea nyumbani na nikaanza kuandaliwa kama mke wakati huo nikiwa na umri wa miaka (16).

“Wakati maisha yalikiendelea nikiwa na umri wa miaka 17 nilibahatika kupata ujauzito ambao hata hivyo mtoto alifariki dunia kutokana na njia kuwa ndogo.

“Kwa sasa nina watoto wawili ambao mmoja nilijifungua kawaida nikiwa na miaka 20 na mwingine kwa njia ya upasuaji, hivyo nimelazimika kukubaliana na hali halisi licha ya ukweli kwamba inaniuma sana kuona ndoto zangu hazijatumia za kuwa daktari bingwa wa watoto,” anasema Rehema ambaye kwa sasa anaishai jijini Dar es Salaam na Mume wake huyo.

Machapisho na tafsiri mbalimbali vinachambua kuwa ndoa za utotoni ni pale msichana au mvulana wanapoingia katika ndoa wakiwa chini ya umri wa miaka 18.

Kwa kawaida, ndoa hiyo huwa kati ya msichana na mwanaumwe aliyemzidi umri. Yaweza pia kuwa ndoa kati ya msichana na mvulana.

Zipo sababu nyingi zinazosababisha baadhi ya wanaume wenye umri mkubwa kutaka kuoa wasichana.

Mara nyingi ni juu ya mila na tamaduni, na mawazo ya kizamani juu ya wanawake na wanaume.

Wakati mwingine, wasichana huolewa kwa kuwa wamepata mimba, au kwa sababu ya shinikizo kutoka kwenye familia kuwataka waolewe kabla hawajapata mimba.

Wazazi pia wanaweza kuweka shinikizo kwa vijana kuingia katika ndoa kutokana na mila, au kwa vile wao ni maskini.

Athari za ndoa za utotoni

Ndoa za utotoni huathiri afya ya msichana, elimu, usalama na furaha. Wasichana waolewapo wakiwa chini ya umristahiki tafsiri yake ni kwamba huacha kwenda shule na kama tunavyofahamu kwamba bila elimu nzuri, wasichana hawawezi kupata kazi nzuri itakayomuwezesha kuendesha maisha na kujimudu kwa ujumla.

Aidha, wasichana hupata mimba wakiwa katika umri mdogo, kabla miili yao kuwa tayari. Hii huongeza hatari matatizo ya hatari, maradhi na hata kusababisha kifo.

Pia wasichana wapo katika hataari zaidi ya kupata VVU na magojwa yatokanayo na ngono, kwa kuwa hawajajengeka kikamilifu.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani linalohusika pia na afya ya uzazi (UNFPA) ya mwaka 2014 iliyopewa jina la Early Marriage Fact Sheet inabainisha kuwa nchini Tanzania, wasichana walioolewa kati ya umri wa miaka 15-24 wana uwezekano mkubwa wa kuwa na VVU kuliko wasioolewa (2.5% / 2.0%).

Hali ikoje Tanzania?

Tanzania kama ilivyo nchi nyingine nayo imekuwa ni mhanga wa changamoto hii ya ndoa za utotoni.

Kwa ni tumeshuhudia ripoti na machapisho mbalimbali yote yakizungumzia juu ya changamoto hii ya ndoa za utotoni.

Ni ukweli uliobayana kwamba changamoto ya ndoa za umri mdogo inaanzia mbali.
Mfano mwaka 2021 Ripoti ya Benki ya Dunia ilibainisha kuwa zaidi ya wasichana 120,000 huacha shule kila mwaka nchini Tanzania.

Kati ya hao 6,500 ni kwa sababu ya ujauzito au kuwa na watoto.

Kama hiyo haitoshi ripoti nyingine ya benki hiyo kuhusu Tathimini ya Ukatili wa Kijinsia Tanzania(Tanzania Gender Based Violence Assessment) iliyozinduliwa Aprili 5, 2022 inabainisha kuwa msichana mmoja kati ya watatu aliolewa kabla ya kufikia miaka 18.

“Takwimu za mwaka 2015-2016 zinaonyesha kuwa zaidi ya msichana 1 kati ya 3 nchini Tanzania wameolewa kabla ya kutimiza miaka 18.

“Hii inawakilisha kupungua kidogo, kutoka asilimia 40 mwaka 2010 hadi asilimia 36 mwaka 2015-2016,” inabainisha sehemu ya ripoti hiyo.

Aidha, inabainisha kuwa katika utafiti wa mwaka 2017 kuhusu vichochezi na madhara ya ndoa za utotoni nchini Tanzania, Wizara ya Afya ilithibitisha kuwa tatizo la ndoa za utotoni bado liko juu katika mikoa mingi nchini.

Tathimini pia inaonyesha kuwa kiwango cha ndoa za utotoni kiko juu miongoni mwa baadhi ya makabila kama vile Wamasai na Wagogo, pia ndoa hizo za utotoni huusishwa kwa karibu na vitendo vya ukeketaji.

Aidha, hali inaonyesha kuwa mazingira pia yamekuwa ni kichocheo cha ndoa za utotoni, kwani kwa mujibu wa ripoti hiyo wanaume na wanawake wanaoishi katika maeneo ya mijini huchukua muda mrefu kuoa ua kuolewa ikilinganishwa na wennzao wa vijijini.

Elimu pia inaelezwa kama msaada kwani wanawake walio na angalau na kiwango cha elimu ya sekondari huchelewa kuolewa tofauti na wale wasio na elimu kabisa hasa wenye umri wa miaka 23.6 hadi 17.8.

Hii ina maana kwamba elimu ni muhimu kwa mtoto wa kike na jamii kwa ujumla kwani iwapo watapata msingi bora wa itawasaidia wao na taifa kwa ujumla kudhibiti ombwe hili la ndoa katika umri mdogo.

Sanjari na hiyo ni muhimu tuwawezeshe wasichana kutimiza uwezo wao wa kila siku na kuzifikia ndoto zao.

Takwimu

Takwimu za ripoti ya Benki ya Dunia imetaja mikoa ambayo ilikuwa kinara kwa wanawake kukuolewa chini ya umri wa miaka 18 kwa lugha nyingine waliolewa katika umri mdogo.
Mikoa hiyo na viwango vyake katika mabano ni Tabora(76%), Shinyanga(64%), Mara(55%), Dodoma(45%) na Manyara(44%).

Hata hivyo,ni bayana kwamba ndoa katika umri mdogo ndiyo imekuwa chanzo cha ukatili na unyanyasaji kwa wanawake.

Hali inaonyesha kuwa wasichana walioolewa katika umri mdogo ndio waliofanyiwa ukatili zaidi.

Takwimu za mwaka 2015 hadi 2016 kwa wanawake wanaofanyiwa ukatili na wenza wao zinaonyesha kwamba mikoa kinara yenye kiwango cha juu kwa wanawake kufanyiwa ukatili nchini Tanzania ni pamoja na Mara na Shinyanga ambazo zote zina asilimia 78 huku kiwango cha nchini kikiwa ni katika mikoa ya Kaskazini Pemba asilimia 8 na Kusini Pemba asilimia 9.

Mikoa mingine ni Tabora(71%), Kagera(67%), Geita(63%), Simiyu(62%), Kigoma(61%), Mwanza(60%), Njombe(53%), Katavi(50%), Dodoma(50%), Rukwa(46%), Manyara(46%),Arusha(45%), Mbeya(45%), Ruvuma(44%), Dar(39%), Iringa(37%), Lindi(37%), K’manjaro(35%), Pwani(35%),Mtwara(33%),Tanga(25%),Kusini Unguja(22%), Mjini Magharibi(18%) na Kaskazini Pemba(13%).

Sanjari na hayo, zaidi ya asilimia 44 ya wanawake wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 49 wamekiri kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili na ule wa kingono na wenza wao.

Kiwango hicho ni cha juu zaidi tofauti na makadirio ya kimataifa ya ushamiri wa unyanyasaji kutoka kwa wenzi wa maisha(IPV) kwa wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 sawa na asilimia 27 huku wastani wa kikanda wa Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ukiwa ni asilimia 33.

Upande wa makadirio ya ripoti ya Shirika la Afya Duniani(WHO) inahitaja Tanzania kama nchi ambayo unyanyasaji wa wanawake wanaofanyiwa na wenza wao ni jambo la kawaida ikilinganisha na mataifa mengine zilizofanyiwa utafiti kama huo.

Aidha, WHO inaiweka Tanzania katika kundi la nchi 12 zenye hatari zaidi ya unyanyasaji wa wanawake katika ukanda wa Afrika.

Sambamba na hayo, ripoti ya karibuni ya Tanzania Demographic and Health Survey(TDHS) inaonyesha kuwa ukatili kwa wanawake wenye umri zaidi ya miaka 15 hadi 49 ni asilimia 40.

Sheria inasemaje

Nchini Tanzania Sheria ya Ndoa imeweka umri wa chini wa kuolewa kuwa 15 kwa wasichana na 18 kwa wavulana.

Mwaka 2016 Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa uamuzi kwamba umri wa chini kabisa kwa mtoto wa kike ni kinyume cha Katiba, na uamuzi huo ulikubaliwa na Mahakama ya Rufani mwaka 2019.

Kama sehemu ya uamuzi huo, serikali iliagizwa kubadili umri wa chini wa kuolewa kwa wasichana. kuwa 18 ndani ya mwaka mmoja, lakini hii bado inasubiri hadi sasa.

Hali ikoje nchi nyingine

Katiba ya Uganda, kifungu cha 31(1) (b): Mwanaume na Mwanamke ana haki ya Kuoa au kuolewa ikiwa tu ni kila mmoja ana umri wa miaka 18 za zaidi na wanayo haki katika umri huo.

Aidha, Katiba ya Namibia, Kifungu cha 14(1): Wanaume na wanawake wa
umri kamili, bila kizuizi chochote kwa sababu ya rangi, kabila asili, utaifa, dini, imani au hali ya kijamii au kiuchumi atakuwa na haki ya kuoa au kuolewa na kupata familia.

Janga la Uviko 19 latajwa

Wakati ripoti hiyo ya benki ya dunia ikibainisha hayo, upande mwingine ripoti nyingine mpya iliyotolewa Machi Aprili mwaka huu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) kuhusu Haki za Binadamu, inabainisha kuwa ndoa za umri mdogo na mimba za utotoni ziliongezeka wakati wa janga la Uviko-19.

LHRC inasema kuwa tumaini pekee ambalo limesaidia kurejesha ndoto za wasichana hao ni juu ya uamuzi wa Serikali ya wamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza fursa nyingine kwa wanafunzi waliopata ujauzito kurejea tena shuleni.

“Kupitia uchunguzi wa vyombo vya habari na ufuatiliaji wa haki za binadamu,
LHRC ina kumbukumbu 37 matukio ya ndoa za utotoni, mbili zaidi ya zile zilizoandikwa mwaka 2020.

“Matukio haya yalikuwa kuripotiwa katika mikoa kama Katavi, Shinyanga, Mara, Mtwara, Lindi, Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma na Rukwa.

“Wasichana wengi waliofunga ndoa za utotoni walikuwa katika kundi la umri wa miaka 13 hadi miaka 16,” inaeleza ripoti hiyo ya LHRC.

Mahari ndio kichocheo

Ripoti hiyo inafafanua zaidi kuwa mahari inayotolewa kwa ajili ya kuozeshwa wasichana hao ndio imekuwa kichocheo kikubwa zaidi kwa wazazi kuwalazimisha watoto wao kuolewa.
Katika hilo wazazi wa kiume wa mabinti kwa maana ya baba ndio wamekuwa mstari wa mbele kushinikiza watoto wao kuolewa chini ya umri stahiki.

“Mdogo zaidi mwathirika, ambaye aliokolewa kutoka ndoa ya utotoni ilikuwa miaka 11. Karibu nusu ya matukio (46%) yaliripotiwa katika Kanda ya Ziwa (20%), hasa mkoani Mara, ukifuatiwa na Ukanda wa Magharibi, hasa Mkoa wa Katavi hata hivyo wengi wa wahusika walikamatwa,” ainabainisha ripoti hiyo.

Mimba za utotoni na ndoa za utotoni huwazuia wasichana kupata haki yao ya elimu.
Kulingana na 2020 Takwimu Muhimu za Msingi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, zinazhambua kuwa, idadi ya wasichana wanaoshuka kutokwenda shule kwa sababu ya ujauzito imeongezeka.

Kwa mfano,idadi ya wasichana walioacha shule kutokana na ujauzito iliongezeka kutoka 3,439 mwaka 2015 hadi 5,398 mwaka 2019.

Ni wajibu wa nani kukomesha hili?

Ni wazi kwamba hakuna mbinu rahisi yakuweza kutokomeza ndoa za utotoni iwapo kila mmoja atafanya kazi peke yake.

Hii ina maana kwamba lazima tufanye kazi pamoja kwani kila mmoja anayo nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko iwapo tutaungana pamoja.

Ni wajibu wetu kupaza sauti katika jamii dhidi ya ndoa za utotoni nchini na kuwasaidia wasichana kubaki shuleni na kutimiza ndoto zao.

Kwani kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto(UNICEF) Mwaka 2010 kulikuwa na vifo 644 katika kila vizazi hai 100,000 huku kufikia mwaka 2017 serikali ilipiga hatua kwa kupunguza idadi hiyo hadi kufika 524.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles