31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wakazi 5,000 Mwanza kupatiwa vipimo bure wiki ya huduma za maabara

* Ipo pia tezi dume, homa ya ini

Na Clara Matimo, Mwanza

Wananchi 5000  mkoani hapa  wanatarajia kupatiwa huduma ya vipimo bure vya kutambua magonjwa mbalimbali kutoka Chama cha Wanasayansi wa Maabara za Afya (MeLSAT) Mkoa wa Mwanza, ikiwemo viashiria vya saratani ya tezi dume, homa ya ini, kisukari, malaria, shinikizo la damu, kaswende na Virusi vya Ukimwi(VVU).

Wanachama wa Chama cha Wanasayansi wa Maabara za Afya (MeLSAT) Mkoa wa Mwanza, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Mkuu wa mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel, kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya huduma za maabara yanayotarajia kufanyika kimkoa Mei 2 hadi 6 mwaka huu katika uwanja wa furahisha.

Hayo yamebainishwa  jijini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel April 28, ambapo ameeleza kwamba huduma hizo zitatolewa kuanzia Mei 2 hadi 6, mwaka huu katika uwanja wa furahisha uliopo Manispaa ya Ilemela mkoani humo ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya huduma za maabara kimkoa ambayo yameandaliwa na MeLSAT kwa kushirikiana na ofisi yake huku akiwataka wakazi wa mkoa huo kutumia fursa hiyo adhimu kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali.

Ametaja huduma zingine zitakazotolewa katika maadhimisho hayo kuwa ni elimu kuhusu shughuli za Baraza la Wataalamu wa Maabara (HLPC), maonyesho ya vifaa mbalimbali vya maabara kutoka makampuni tofauti tofauti yanayouza vifaa vya maabara nchini  pia wananchi watapata fursa ya kupata ushauri kutoka kwa wataalamu hao.

“Nawasihi wananchi wa mkoa huu watumie fursa hii adhimu wafike uwanja wa furahisha tarehe zilizopangwa ili kufanya  uchunguzi wa magonjwa mbalimbali pamoja na kupatiwa elimu juu ya matumizi sahihi ya huduma za maabara na shughuli zinazofanywa na wanataaluma wa sayansi za afya nchini hasa wanaume wajitokeze kwa wingi wapime viashiria vya saratani ya tezi dume maana utafiti unaonyesha wanaume wengi wanapitia changamoto hizo hasa umri unavyozidi kuwa mkubwa changamoto zinaanza kuonekana wataalamu wa afya wanasema viashairia huwa haviko wazi sana.

“Lakini ukifanikiwa kupima mapema unapata matibabu sahihi na kwa wakati sahihi kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ambapo maisha yako yataboreka, watu wengi tumejikuta tukitembea wakati tuna magonjwa yanatusumbua hadi pale unapofanyiwa uchunguzi wa maabara ndipo itabainika afya yako haiko sawa yapo mashambulizi ya virusi vya  magonjwa mbalimbali ya kuambukiza ambayo yanapatikana ndani ya damu hivyo nasisitiza wananchi wengi wajitokeze  kwenye zoezi hili  muhimu kwa ajili ya kupata  matibabu sahihi na bora ili kupunguza  gharama zisizo za lazima,” amesema Mhandisi Gabriel.

Amesema uwepo wa maonyesho ya vifaa mbalimbali vya maabara kutoka kwa makampuni tofauti tofauti kwenye maadhimisho hayo yanayouza vifaa hivyo nchini, itakuwa ni fursa kwa baadhi ya maabara za mkoa huo kukutana na wauzaji wa vifaa hivyo kujua teknolojia iliyopo, upatikanaji wake faida na changamoto ya teknolojia zilizopita, hali itakayochangia kuimarishwa kwa maabara zilizopo na utasaidia kuongeza ufanisi wa huduma hizo kwa wakazi wa mkoa wa Mwanza na kanda ya ziwa.

Aidha, Mhandisi Gabriel amewaomba wananchi wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi uwanjani hapo kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu katika hospitali za mkoa huo kwani mahitaji ya damu bado ni makubwa kutokana na idadi ya wahitaji wengi wao wakiwa ni watoto chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito, watu wenye magonjwa sugu na wanaopatwa na ajali.

Ametoa wito kw waajiri wote ndani ya mkoa wa Mwanza kuwaruhusu wataalamu wa maabara ili wasshiriki kikamilifu katika tukio hilo muhimu la kitaaluma  na bila kuathiri utendaji wa kazi katika maeneo yao.

Mwenyekiti wa MeLSAT Mkoa wa Mwanza, Bertrand Msemwa, amesema lengo la kuandaa maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu afya zao na kuwapa elimu ya majukumu  walionayo wataalamu wa maabara  ikiwemo kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kwa binadamu na  kutoa majibu  kwa ajili ya kusaidia matibabu.

“Tumeandaa  maadhimisho ili tutoe elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya vipimo kabla ya kumeza dawa ili kuondoa  tatizo lililopo dunia nzima la usugu wa dawa linalosababishwa na  wananchi kutumia dawa bila kufanya vipimo bora vya kimaabara, makadirio yetu ni kuhudumia wananchi 1,000 kwa siku  hivyo nawasisi wakazi wa mkoa huu na mikoa jirani wafike kwenye maadhimisho hayo wapate elimu itakayowasaidia kulinda afya zao,”amesema Msemwa.

Mratibu wa Huduma za Maabara Manispaa ya Ilemela Mkoa wa Mwanza, Isikile Rutashoborwa , amesema wanatekeleza majukumu yao kwa kusimamia miongozo inayowaongoza  lengo ni kutoa huduma na vipimo sahihi kwa wanao wahudumia.

Maadhimisho ya wiki ya huduma za maabara hufanyika  mwishoni mwa Aprili duniani kote kila mwaka, Tanzania mwaka huu inaadhimisha kwa mara ya 13 ambapo Mkoani Mwanza yatafanyika kwa mara ya kwanza,  kauli mbiu inasema ‘vipimo vya maabara  za afya ndio msingi wa matibabu bora’,  kazi iendelee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles