23.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

Watoto waliopata ulemavu wa ghafla kufuatiliwa

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kuanza kuwafuatilia watoto walio na umri chini ya miaka mitano ambao wamepata ulemavu wa ghafla sambamba na utoaji chanjo ya matone ya polio.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija na watumishi wengine wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakifuatilia mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo, Dk. Elizabeth Nyema, kwa kamati ya msingi ya afya ngazi ya jamii kuhusu utoaji chanjo ya polio.

Ulemavu wa ghafla wa viungo ni mojawapo ya madhara ya ugonjwa wa polio ambao husababishwa na kirusi cha polio kinachoambukizwa kutoka kwa mtu aliyeathirika kwenda kwa mwingine kwa kunywa au kula chakula kilichochafuliwa na kwa kinyesi chenye vimelea.

Ugonjwa wa polio uliibuka nchini Malawi mwanzoni mwa Februari mwaka huu hatua iliyolazimu Serikali kuanza kutoa chanjo kuwakinga watoto kwakuwa nchi hiyo ni jirani na Tanzania.

Akizungumza jana Aprili 27,2022 wakati wa mafunzo kwa kamati ya msingi ya afya ngazi ya jamii Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Elizabeth Nyema, amesema wanatarajia kuchanja watoto 228,382 kuanzia Mei 12 hadi 15 bila kujali kama walishapata chanjo hiyo katika ratiba zao za kawaida.

“Ugonjwa huu hauna tiba lakini unaweza kuzuilika kwa njia ya matone na mtoto asiyepata chanjo anaweza kuambukiza wagonjwa wengine, tutakapokuwa tunatoa chanjo pia tutawatafuta na kuwafuatilia watoto wote chini ya miaka mitano ambao wamepata ulemavu wa ghafla nyumba kwa nyumba,” amesema Dk. Nyema.

Aidha amesema chanjo hiyo imeshasambazwa katika vituo vyote 77 na kwamba kutakuwa na timu ya watu 1,551 ambayo inahusisha wachanjaji, wahamasishaji na waandikishaji pamoja na wasimamizi 169.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, amewataka wananchi kutoa ushirikiano wakati wa zoezi hilo na kuepuka upotoshaji kwani chanjo hiyo ni salama haina madhara yoyote na hutolewa kwa matone na si kuchomwa sindano.

“Chanjo haijaanza leo tumekuwa nayo kwa muda mrefu na tunajua umuhimu wake, hatujawahi kufeli tunategemea zoezi hili tutafanya vizuri na tutafikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema Ludigija.

Mara ya mwisho mgonjwa wa polio alipatikana nchini Julai 1996 na mwaka 2015 Tanzania ilitangazwa rasmi kuwa nchi isiyokuwa na ugonjwa wa polio katrika nchi za Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles