23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Makala: Serikali ilivyoimarisha huduma za Afya ya Uzazi 2021/22

Na Yohana Paul, Geita

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya ya Uzazi, ikiwa ni pamoja huduma kabla ya kujifungua, Wakati wa ujauzito, Wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

Mapema mwezi mei mwaka huu, Waziri mwenye dhamana akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Afya, Ummy Mwalimu anasema serikali imefanya juhudi kubwa kulenga kuboresha  na kuimarisha huduma hizo kwa mwaka uliopita wa fedha (2021/2022).

Huduma Kabla ya Ujauzito

Akizungumuzia maboresho ya huduma ya afya ya uzazi kabla ya ujauzito, Waziri Ummy anabainisha kuwa katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, kwa upande wa huduma kabla ya ujauzito Wizara kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ilinunua na kusambaza vidonge vya uzazi wa mpango dozi 1,755,349 sawa na asilimia 82 ya lengo.

Waziri waAfya, Ummy Mwalimu.

Anaweka wazi, jumla ya sindano za uzazi wa mpango (aina ya depo-provera) dozi 2,125,625 sawa na asilimia 93 ya lengo na vipandikizi 206,000 sawa na asilimia 78 ya lengo zimesambazwa katika Halmshauri zote nchini.

“Katika kipindi hicho, (mwaka 2021) jumla ya wateja waliotumia njia za uzazi wa mpango walikuwa 4,189,787 ukilinganisha na wateja 4,357,151 waliokuwa tayari kupokea na kutumia huduma ya uzazi wa mpango kwa mwaka 2020.

“Njia hizo za uzazi wa mpango zimetolewa katika vituo mbalimbali vya huduma za afya nchini ni pamoja na vipandikizi asilimia 57.1, sindano asilimia 18.5, vidonge asilimia 10.1, kondomu asilimia 5.3, kufunga kizazi mama asilimia 0.4, Kitanzi asilimia 7.2 na njia zingine asilimia 1.4,” anasema Waziri Ummy.

Huduma wakati wa Ujauzito

Katika hatua nyingine Waziri Ummy anabainisha kuwa, wizara pia imeendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu na huduma za afya wakati wa ujauzito (Antenatal Care) ambapo inakadiriwa kuwa kila mwaka akinamama wapatao milioni 2.3 hutarajiwa kupata ujauzito nchini Tanzania.

“Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, jumla ya Wanawake wajawazito 1,784,809 walihudhuria  Kliniki na kupatiwa huduma za Afya na kati yao, asilimia 99.7 ya akinamama wajawazito walifanya mahudhurio manne au zaidi ikilinganishwa na asilimia 85 mwaka 2020.

Waziri Ummy anakiri kuwa bado ipo changamoto kubwa kwa wanawake wajawazito kuchelewa kuhudhuria kliniki wapatapo ujauzito kwa sababu mbalimbali ikiwemo elimu duni na dhana potofu.

“Takwimu zinaonesha kati ya wajawazito 1,784,809 ni wajawazito 656,040 sawa na asilimia 37.6 walianza kupata huduma za wajawazito chini ya wiki 12 za mwanzo wa ujauzito, ikilinganishwa na asilimia 36 ya kipindi kama hiki mwaka 2020.

 “Aidha, katika kipindi Julai 2021 hadi Machi 2022, asilimia 99.7 ya akinamama wajawazito walifanya mahudhurio manne au zaidi ikilinganishwa na asilimia 85 mwaka 2020,” anasisitiza Waziri Ummy.

“Ongezeko hili kubwa la matumizi ya 2021 huduma za kliniki wakati wa ujauzito limetokana na  kubadilika kwa mwongozo wa huduma muhimu wakati  wa ujauzito kutoka mahudhurio ya kila baada ya miezi mitatu na kuwa mahudhurio ya kila mwezi,” anasema.

Anasema hatua hiyo imefanya jumla mahudhurio ya kliniki kwa wajawazito kufikia nane  au zaidi kwa kipindi chote cha ujauzito huku uhamasishaji uliofanyika juu ya uhumimu wa wajawazito kuhudhuria kliniki ngazi ya jamii umechochea mahudhurio hayo.

Huduma wakati wa kujifungua

Waziri Ummy anaeleza kuwa kwa upande wa huduma ya afya wakati wa kujifungua, Serikali imeendelea kutoa elimu ya umuhimu wa akina mama wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Anasema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, wajawazito 1,398,778 walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya sawa na asilimia 79.5 ikilinganishwa na wajawazito 890,909 sawa na asilimia 80 ya waliojifungulia kliniki kipindi kama hicho mwaka 2020.

Anaeleza kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, wajawazito 1,340,239 walihudumiwa na watoa huduma wenye ujuzi, ikilinganishwa na wajawazito 851,040 waliohudhuria kliniki kipindi kama hicho mwaka 2020.

Anaongeza, ndani ya mwaka huu wa fedha (2021/2022) Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imeratibu ujenzi na ukarabati mkubwa wa vituo vya Afya 304.

Anasema mradi huo umetekelezwa ili kuviwezesha vituo hivo vya afya kutoa huduma kwa wajawazito wanaopata uzazi pingamizi wakati wa kujifungua (CEmONC), huduma ambayo imesaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Anabainisha kuwa hadi kufikia Machi, 2022 jumla ya vituo vya Afya 250 sawa na asilimia 82.2 vilikuwa vimeanza kutoa huduma kamili ya huduma kwa wajawazito wenye uzazi pingamizi ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.

“Wizara inaendelea kuhakikisha vituo vyote vya afya vilivyojengwa ambavyo havijaanza kutoa huduma vinapata watumishi wenye ujuzi hasa Madaktari, watoa dawa za usingizi na wakunga pamoja na vifaa tiba kwa lengo la  kuharakisha kuanza utoaji wa huduma,” anasema.

Huduma Baada ya Kujifungua

Waziri Ummy anabainisha, wizara imeendelea kuboresha huduma za Watoto wachanga ambapo katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022 jumla ya Wodi 30 za Watoto Wachanga Mahututi zimeanzishwa katika hospitali za Halmashauri na kuwezesha kuwepo kwa jumla ya wodi 165 za watoto wachanga.

“Takwimu zilizokusanywa zinaonyesha kuwa jumla ya watoto wenye ulemavu 32,586 walizaliwa katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, na kati yao Watoto 31,640 sawa na asilimia 97 walizaliwa katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Kati ya watoto waliozaliwa, 54 walibainika kuwa na ulemavu wa kuzaliwa ambapo 14 walizaliwa wafu na 40 walikuwa hai na walipatiwa rufaa kwa matibabu zaidi ya kitaalamu. Huu ni wastani wa watoto 2 kuzaliwa na ulemavu kwa kila vizazi 1,000.

“Kulingana na takwimu zinazokusanywa kutoka katika vituo vya kutolea huduma zinaonesha kuwa vifo vya Watoto vimeendelea kupungua mwaka hadi mwaka ambapo vifo vya Watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 8,190 mwaka 2020 hadi vifo 6,741 mwaka 2021,

“Vifo vya Watoto wa chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka vifo 2,657 mwaka 2020 hadi vifo 1,092 mwaka 2021 na vifo vya Watoto umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 3,482 mwaka 2020 hadi vifo 1,512 mwaka 2021. Takwimu hizi hazijumuishi vifo vinavyotokea kwenye ngazi ya jamii,” anabainisha Ummy.

Makadirio ya Bajeti ya Wizara

Ikumbukwe, utekelezaji wa miradi, uboreshaji wa huduma na usimamizi wa sera na mipango kwenye sekta ya afya ikiwemo  elimu na huduma za afya ya uzazi  kwa mwaka wa fedha 2021/2022  ulifanyika ndani ya bajeti ya wizara iliyopitishwa na bunge iliyokuwa na kiasi cha Sh. 1,077,759,224,000.

Akisoma bajeti ya mwaka huu wa fedha, Waziri Ummy anabainisha ili kuendeleza juhudi mbalimbali za kuboresha huduma ya afya nchini ikiwemo huduma ya afya ya uzazi, kwaa mwaka 2022/23, Wizara ijimepanga kutumia kiasi cha Sh 1,109,421,722,000  kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Wizara pamoja na miradi ya maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles