29.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Matundu ya vyoo yatesa shule 72 Morogoro – 2

*Ni moja ya sababu kuu inayoathiri ufaulu wa wanafunzi shule za msingi

Na Ashura Kazinja, Morogoro

SHULE za msingi 72 za Manispaa ya Morogoro zenye takribani wanafunzi 64,362 zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi na walimu, ambapo yapo matundu 892 badala ya mahitaji halisi ya matundu 2,574. 

Takwimu ya idadi ya matundu ya vyoo kutoka Idara ya Elimu ya Msingi Manispaa inaonyesha ukiukwaji wa Mwongozo wa Wizara ya Elimu ambao unaelekeza tundu moja linapaswa kutumiwa na wanafunzi kati ya 20 na 25. 

Ni sababu ya utoro

Upungufu huo wa matundu ya vyoo kwa shule za Msingi za Manispaa ya Morogoro kunachangia utoro, wanafunzi wa kike kubakia majumbani wakati wa hedhi na hivyo kuathiri maendeleo ya elimu na kushuka kwa ufaulu.

Tatizo la huduma hii muhimu pia linawagusa waalimu, ambao pia nao utendaji wao hushuka kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta maeneo ya kujistiri, mengi yakiwa kwenye makazi yaliyo jirani na shule.

Wanafunzi shule ya msingi Mafisa A, wakiwa wamepanga foleni ya kuingia chooni wakati wa mapumziko.

Uchunguzi uliofanyika katika shule kadhaa umebaini kuwa, kutokana na msongamano mkubwa wakati wa mapumziko wakati wa kujisaidia, wanafunzi wengi hutumia fursa hiyo kutorudi darasani kwa kuhofia kupewa adhabu kwa kuchelewa kurudi baada ya muda wa mapumziko kumalizika na hivyo kukosa vipindi.

Kwa upande wa walimu huwa vivyo hivyo kwani nao huchelewa kurejea madarasani kutokana na kutumia muda mwingi wa kwenda kupata huduma ya faragha kwenye makazi yaliyoko jirani au hata kwenye nyumba za wageni.

Hali ni mbaya zaidi kwa wasichana hasa wanapokuwa katika vipindi vya hedhi ambapo hulazimika kusalia majumbani kwa takriban siku tano kila mwezi jambo ambalo huathiri maendeleo yao kielimu na hivyo kuathiri ufaulu.

Ikiwa kuna idadi ndogo ya matundu ya vyoo shuleni isiyolingana na idadi kubwa ya wanafunzi, hii inaweza kusababisha msongamano na uchafu, wanafunzi wanapokabiliana na mazingira machafu na yenye magonjwa wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa kama vile kuhara, minyoo na magonjwa ya ngozi, ambayo yanaweza kuwaathiri kiafya na kusababisha kukosa masomo na kushindwa kuhudhuria shule.

Sera ya elimu

Kulingana na sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na sheria ya elimu ya mwaka 2016, pamoja na sheria ya afya msingi ya mwaka 2017 zinaelekeza kuwa shule zinapaswa pamoja na mambo mengine kuwa na vyoo bora na vya kutosha kwa walimu na wanafunzi.

Aidha, kwa upande wa miundombinu ya vyoo mashuleni, sera ya afya inaelekeza kuwa shule zinapaswa kuwa na vyoo salama, safi na vya kutosha, ikiwa na lengo la kulinda haki za wanafunzi na wafanyakazi wa shule ya kufanya kazi katika mazingira safi na salama.

Elimu bure na Miundombinu

Februari 2020 akizungumza na wenyeviti pamoja na wawakilishi wa Kamati  za Shule za Msingi za Serikali Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kujadili mwenendo wa utoaji wa taaluma na changamoto zake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga, anasema Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ilikuwa kinara kwa miaka yote katika matokeo ya mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi lakini ilipofika mwaka 2017 hali ya matokeo ilianza kubadilika kwa kuwa nyuma ya Halmashauri za Ulanga na Malinyi.

Anasema kuwa ufaulu ulikuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka isipokuwa mwaka 2019 ulishuka kutoka asilimia 88.13 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 87.74 mwaka 2019, na kuzitaja miongoni mwa sababu zilizosababisha kushuka kwa ufaulu kuwa ni pamoja na ongezeko kubwa la uandikishaji wa wanafunzi kufuatia utekelezaji wa dhana ya elimu bila malipo, ambapo ongezeko hilo halijaenda sambamba na idadi ya miundombinu ikiwemo ya madarasa na vyoo.

Serikali na Boost

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki, January 9, 2023 mjini Morogoro, alisema Serikali imetenga kiasi cha Sh Trilioni 1.15 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya shule za msingi zilizochakavu kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu wa fedha. 

Aidha, anasema ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule hizo ulitarajia kuanza Januari na Februari, mwaka huu nchini kote na kuwa baadhi ya shule zitavunjwa na kujengwa upya.

Sambamba na hilo, alisema kuwa shule nyingine zitafanyiwa ukarabati mkubwa pamoja na mdogo kwa lengo la kuzifanya ziwe na mazingira bora kulingana na hali ya sasa kwa walimu na wanafunzi.

Wazazi wanasemaje?

Mzazi na mkazi wa Kilakala, Hanifa Kibwana anasema uhaba wa matundu ya vyoo unasababisha kukosa masomo mara kwa mara kutokana na utoro, jambo ambalo lina athari kwa maendeleo ya elimu na ufaulu kwa ujumla.

Anasema wanafunzi wanapopata haja ya kwenda chooni wakati wa mapumziko na hakuna matundu ya kutosha, hulazimika kusubiri muda mrefu au hata kukosa fursa ya kwenda chooni kabisa, hali inayoweza kuwafanya wanafunzi washindwe kuzingatia vizuri katika masomo yao na kuathiri uwezo wao wa kujifunza na kufaulu.

“Mwanafunzi analazimika kuacha masomo mara kwa mara kutokana na  uhaba wa matundu ya vyoo, anakosa fursa sawa za kujifunza na kushiriki katika masomo kama wenzake, anaweza kukosa maelezo muhimu, mazoezi na majaribio ambayo yanaweza kumsaidia kufaulu mtihani,” anasema Hanifa. 

Naye mzazi na mkazi wa Mawenzi, Rhoda Mayemba, anasema uhaba wa matundu ya vyoo shuleni unaweza kusababisha unyanyapaa na aibu kwa wanafunzi, endapo watajisaidia kwenye nguo wanapokosa fursa ya kwenda chooni kwa wakati.

Anasema hii inaweza kuathiri hisia zao na kuwafanya washindwe kujieleza vizuri darasani, pia kukosa utulivu na wasiwasi wanapokuwa darasani kwa kuchekwa na wenzao.

“Uhaba wa matundu ya vyoo kwa shule zetu ni tatizo na linawatesa sana watoto, kuna wengine wanashindwa kuvumilia foleni wakati amebanwa sana, anajikuta haja inatoka hivyo  kusababisha kujisaidia kwenye kaptura au nguo, wenzake watamcheka, hivyo lazima akose kujiamini na kushindwa kujieleza au hata kumsababishia kutoelewa vizuri darasani, ni watoto wetu yanawakuta hayo na wakati mwingine anakwambia hataki kwenda shule kwa aibu hiyo,” anasema Rhoda.

Mzazi Zuhura Mzigila mkazi wa Mafiga anasema hali ya vyoo katika shule za msingi Mafiga A na B hairidhishi kwani vyoo ni vichache watoto ni wengi, pia ni vichafu na vimejaa hivyo kusababisha magonjwa kama kuhara, kichocho na kipindupindu.

“Kwa nini manispaa haijengi matundu ya vyoo kulingana na mahitaji ya kila shule, wala haitengi bajeti kwa ajili ya vyoo, na kama kuna watu wanahujumu kwanini wasichukuliwe hatua, mwanangu mdogo wa darasa la pili ana wiki mbili hajaenda shule alijisaidia kwenye nguo akiwa kwenye foleni ya kuingia chooni wenzie wakamcheka,” anaeleza.

“Wakati mwingine kutokana na foleni kubwa za kuingia chooni watoto wengine wanaokaa jirani na shule wanakimbilia nyumbani huku wenzao wanafundishwa hivyo kipindi kinampita, na mwingine unamkuta kila leo anaumwa, kwahiyo ufaulu sio mzuri na uhaba wa vyoo ndio unachangia hilo,” anasema Zuhura.

Upande wake, Emmanuela Msangi mkazi wa kata ya Tungi anasema uhaba wa vyoo katika shule za msingi katika kata hiyo kuna sababisha wengine kuogopa kula ili kuepuka kwenda chooni au kurudi nyumbani kujisaidia, na hivyo kupunguza umakini katika masomo kwani hakuna anayeweza kuelewa akiwa na njaa. 

Mwanafunzi Baraka Anakti wa darasa la Saba shule ya msingi Msamvu B anasema kuwa uhaba wa matundu ya vyoo, kuziba kwa vyoo, uchafu na mazingira yasiyorafiki kuna mfanya aathirike kimasomo na pia kupoteza kabisa hamu ya kwenda chooni.

Walimu, Wanafunzi wanena

Naye mwanafunzi Shalom Kise wa darasa la nne shule ya msingi Muungano anasema kukaa muda mrefu bila kujisaidia kunamfanya kutokuwa makini na kushindwa kumsikiliza mwalimu vizuri.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mafisa A, Mdaku Rajabu anasema shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 850 ina matundu ya choo saba, na kwamba ingawa ufaulu wa wanafunzi shuleni hapo siyo mbaya lakini changamoto iliyopo ya vyoo inapunguza ubora wa viwango vya elimu kwa ujumla.

Mdaku anasema kutokana na kutokuwepo kwa choo cha walimu shuleni hapo inawalazimu wakati mwingine walimu kujisaidia kwenye choo cha nyumba ya kulala wageni (loji) inayojulikana kwa jina la ‘Maraha’ hali inayoweza kusababisha walimu kufikiriwa visivyo.

Upande wake, Mwalimu Mkuu msaidizi shule ya msingi Mafiga A, Semeni Kapera anasema ufaulu ni mzuri shuleni hapo mbali na changamoto ya matundu ya vyoo, kutokana na jitihada za walimu kukabiliana na hali hiyo kwa kuwasaidia wanafunzi pale wanapokumbwa na shida hususani wanafunzi wadogo ambao wengine kutokana na changamoto ya vyoo hujisaidia katika nguo.

Afisa Elimu Kata ya Mkundi, Osward Tarimo, anasema uhaba wa matundu ya vyoo katika shule za kata ya Mkundi upo kwa kiwango cha kati, na kwamba uhaba huo unaathiri ufaulu wa wanafunzi kwa njia mbili, ikiwemo kutumia muda mrefu kwenye foleni ya kujisaidia mpaka muda unaisha na hivyo kumfanya mwalimu kushindwa kuendelea na kipindi kwani wanafunzi wanakuwa bado wako nje na ya pili mtoto anaathirika kisaikolojia kwa kufikiria atajisaidia wapi na vipi kutokana na foleni kubwa. 

Matundu ya vyoo Shule ya Msingi Mafisa A.

Mwenyekiti Mtaa wa Nanenane, Mwajuma Tengeni, anasema changamoto ya matundu ya vyoo ni mojawapo ya sababu zinazochangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi kutokana na kupoteza muda mwingi kutafuta huduma ya choo na kupanga foleni ya muda mrefu.

Afisa Afya kata ya Magadu, Elda Msigara, anasema hamna taarifa yoyote ya uwepo wa ugonjwa wa kichocho kwa shule za msingi zilizopo kata ya Magadu na kwamba mwezi wa nne mwaka huu zilitolewa dawa za kichocho na minyoo kwa shule zote na hata kwa watu wa majumbani. 

Afisa Elimu anasemaje?

Akizungumzia swala hilo Afisa elimu Takwimu Manispaa ya Morogoro, Amna Kova, anakiri kuwepo kwa uhaba wa matundu ya vyoo katika shule za msingi kwa kusema kuwa, Manispaa inashirikisha wadau mbalimbali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya shule ikiwemo ujenzi wa vyoo ili kukabiliana na changamoto hiyo na ikiwezekana kuimaliza kabisa.

Amewataja baadhi ya wadau hao kuwa ni Alliance One ambao wamejenga vyoo 22, Swash na Umoja wa wanawake Mainjinia, na kwamba ingawa kuna changamoto katika shule nyingi lakini ipo shule moja ya Bungo ambayo haina changamoto ya vyoo na ufaulu wake ni mzuri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, anasema tatizo la uhaba wa matundu ya vyoo katika shule za msingi manispaa ya Morogoro lipo kwa kiasi, na kwamba sababu msingi ya uwepo wa tatizo hilo ni ongezeko kubwa la wanafunzi kutokana na elimu bila malipo.

Anasema kwa kuliona hilo serikali imeanzisha mradi wa kuboresha elimu ya awali na msingi nchini (Boost) kwa ajili ya kuboresha shule za msingi ambao mpaka sasa umeshatoa Sh bilioni 1,401,200,000 fedha za maendeleo.

Akijibu swali kuhusiana na bajeti inayotengwa na halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa vyoo, anasema kwamba, bajeti za halmashauri zinavipaumbele vyake ambapo mwaka jana ilikuwa ni ujenzi wa madarasa kutokana na ongezeko la wanafunzi, na mwaka huu 2023/2024 ni madawati, hivyo swala la ujenzi wa vyoo nalo litapewa kipaumbele.

Anasema kwa upande wa  Serikali kuu imeshapeleka fedha kiasi cha Sh milioni 180,000,000 kwa ajili ya ukarabati wa shule mbalimbali, Sh milioni 181,000,000 kwa ajili ya umaliziaji na Sh milioni 400,000,000 kwa ajili ya shule mpya moja itakayokuwa na madarasa 16, vyoo 21 na jengo la utawala na kwamba jumla ya fedha toka serikali kuu ni Sh milioni 661,000,000.

Hata hivyo, Serikali haina budi kuweka mkakati na kipaumbele zaidi katika kutatua au kuondoa kabisa changamoto ya vyoo mashuleni, kwa kuelekeza bajeti zake na miradi mbalimbali inayoendelea katika swala hilo pia, ili kuweza kuinua zaidi kiwango cha elimu na ufaulu wa wanafunzi, kwa kutoa elimu bora na sio bora elimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles