27.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Athari ya uhaba wa matundu ya vyoo kwa elimu ya mtoto wa kike

Na Ashura Kazinja, Morogoro

MSICHANA anayesoma shule ya msingi ndani ya Manispaa ya Morogoro aliyefikia balehe anapoteza wastani wa vipindi 420 kati ya 1,589 anavyopaswa kusoma kwa mwaka, kutokana na uhaba wa matundu ya vyoo na vyumba maalum kwa ajili ya kujistiri, hali inayoathiri ustawi wake kielimu.

Hali hii inayowakumba wasichana inatokana na shule nyingi ndani ya manispaa kutokuwa na matundu ya vyoo ya kutosha, hivyo kumlazimu binti kukosa masomo siku tano kila mwezi, ambazo ni zaidi ya siku 60 kati ya siku 227 kwa mwaka anazotakiwa kusoma pamoja na wenzie.

Idadi hii ya vipindi inakuja kutokana na uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa makala hii, kuwa kila mwezi mwanafunzi anakosa siku tano akiwa kwenye hedhi ambazo ni sawa na vipindi 40.

Aidha, uchunguzi umebaini kutokana na uhaba wa matundu ya vyoo wasichana wengi husalia majumbani kutokana na kutokuwa na uhakika wa maeneo ya kujistiri.

Hali isiyoridhisha ya uhaba wa vyoo na isiyo rafiki kwa mabinti, na kutokuwepo kwa vyoo vilivyotengwa maalum kwa ajili ya mabinti wakati wa hedhi katika shule karibu zote za msingi Manispaa ya Morogoro, husababisha ukosefu wa faragha na hivyo kuwafanya mabinti kujiona wamesahauliwa na kutojaliwa.

Hata hivyo, walimu na wafanyakazi wa shule wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha juu ya changamoto zinazowapata wasicha wakati wa hedhi shuleni kutokana na uhaba wa matundu ya vyoo uliopo, na kuwapa msaada unaohitajika, ikiwa ni pamoja na ruhusa ya kwenda chooni wakati wowote wanapohitaji.

Aprili, 2022 akizungumzia changamoto ya hedhi shuleni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa mkoani Dodoma aalisema kuwa asilimia 48 ya wanafunzi wa kike wanakosa masomo kutokana na kuwa katika mzunguko wa hedhi hali ambayo huathiri uwezo wa wanafunzi hao kujifunza kwa ufasaha.

Hali ya vyoo shule ya msingi Mafiga B.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) juu ya masuala ya maji na usafi wa mazingira shuleni ya mwaka 2018 inaonesha asilimia 66.8 ya shule ndizo zina huduma ya hedhi salama ambapo kati ya hizo zilizobainika kuwa na viteketezi ni asilimia 24 huku asilimia 22.8 zinatupa taka kwenye mashimo na 19.5 zina vichomea taka visivyokidhi.

Waziri Ummy anasema pamoja na jitihada za Serikali na wadau bado tatizo la hedhi salama shuleni ni pana na linahitaji mikakati endelevu, hivyo Serikali iliona kuna haja ya kufanyia utafiti. 

Wazazi wanasemaje?

Baadhi ya Wazazi akiwemo, Rahel Mahende, mkazi wa Mwembesongo anasema uhababa wa matundu ya vyoo hususan vyumba maalum kwa mabinti wakati wa hedhi, katika shule za msingi kunasababisha ukosefu wa faragha na usafi wakati wa hedhi na hivyo kumlazimu yeye kama mzazi kumwacha binti yake abaki nyumbani.

“Kwa kweli jambo hili ni la faragha sana, kwani binti kuwa katika hedhi wakati mazingira aliyopo sio rafiki kwake kuweza kupata faragha na kujistiri, kunaweza kumfanya ajihisi sio salama na kuona aibu na hofu ya kuvuja damu mbele ya wenzake, ndio maana huwa namwacha mwanangu abaki nyumbani akiwa katika siku zake,” anasema Rahel.

Naye mzazi Yespa Said Mohamed, anaeleza kuwa mabinti wanahitaji elimu sahihi juu ya afya ya hedhi na mabadiliko yanayotokea katika miili yao na kwamba hali hiyo itawawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali katika mazingira ya shule zao kama vyoo na sodo (taulo za kike) za kujistiri.

“Mimi ni mzazi pia, swala hili linatuhusu wote hata sisi wababa katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa mabinti zetu, elimu ni muhimu sana kwao juu ya afya ya hedhi na mabadiliko ya mwili wakati wa kipindi cha kukua, pia sio mbaya kulingana na hali ya vyoo kuwa siyo nzuri sana, kuwafundisha namna ya kukabiliana na changamoto hiyo, kwani wengine uamua kubaki nyumbani siku zote za hedhi hali ambayo  inaweza kuwaathiri kimasomo,” anasema Mohamed.

Wanafunzi je?

Mwanafunzi, Gladness Hosia wa darasa la saba shule ya msingi Msamvu B, anasema vyumba maalum kwa ajili ya mabinti wakiwa katika hedhi shuleni hapo havipo, bali huwa wanaelekezwa na walimu kama hali itawatokea ghafla na hutumia vyoo vilivyopo kujistiri, na kwamba baadhi ya mabinti huogopa na kuamua kubaki nyumbani mpaka kipindi cha hedhi kiishe.

“Chumba maalum kwa ajili yetu mabinti tukiwa katika hedhi hakuna, ila tukimfata mwalimu anatuelekeza kama hali hiyo ikitokea ghafla shuleni, wakati wa mapumziko foleni inasumbua kwani inahitaji muda kutumia choo ili kujifanyia usafi na kujistiri wakati wanafunzi wengine wanakupigia kelele utoke nao waingie, ndio maana wakati mwingine tunaamua kukaa nyumbani mpaka siku za hatari ziishe,” anasema Gladnes.

Wito kwa Serikali

Mwanafunziwa darasa la saba shule ya msingi Msamvu B, Amina Selemani anaiomba Serikali iwajengee vyumba maalum kwa ajili ya kujistiri wakati wa hedhi ili kuwaepusha na adha wanayoipata ikiwemo kukosa faragha na masomo kipindi cha hedhi.

“Hakuna chumba wala eneo maalum kwa ajili yetu mabinti wakati wa hedhi hapa shuleni, tunaiomba serikali itujengee vyumba maalum kwa ajili ya mabinti wakati wa hedhi, kwani kwa sasa tunatupa tu sodo ovyo” anasema Amina.

Choo shule ya msingi Magiga B.

Akizungumzia swala hilo Afisa elimu Takwimu Manispaa ya Morogoro, Amna Kova, anakiri kuwepo kwa uhaba wa matundu ya vyoo katika shule za msingi kwa kusema kuwa, Manispaa inashirikisha wadau mbalimbali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya shule ikiwemo ujenzi wa vyoo ili kukabiliana na changamoto hiyo na ikiwezekana kuimaliza kabisa.

Amewataja baadhi ya wadau hao kuwa ni Alliance One ambao wamejenga vyoo 22, Swash na Umoja wa wanawake Mainjinia, na kwamba ingawa kuna changamoto katika shule nyingi lakini ipo shule moja ya Bungo ambayo haina changamoto ya vyoo na ufaulu wake ni mzuri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, anasema tatizo la uhaba wa matundu ya vyoo katika shule za msingi manispaa ya Morogoro lipo kwa kiasi, na kwamba sababu msingi ya uwepo wa tatizo hilo ni ongezeko kubwa la wanafunzi kutokana na elimu bila malipo.

Anasema kwa kuliona hilo serikali imeanzisha mradi wa kuboresha elimu ya awali na msingi nchini (Boost) kwa ajili ya kuboresha shule za msingi ambao mpaka sasa umeshatoa Sh bilioni 1,401,200,000 fedha za maendeleo.

Akijibu swali kuhusiana na bajeti inayotengwa na halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa vyoo, anasema kwamba, bajeti za halmashauri zinavipaumbele vyake ambapo mwaka jana ilikuwa ni ujenzi wa madarasa kutokana na ongezeko la wanafunzi, na mwaka huu 2023/2024 ni madawati, hivyo swala la ujenzi wa vyoo nalo litapewa kipaumbele.

Anasema kwa upande wa  Serikali kuu imeshapeleka fedha kiasi cha Sh milioni 180,000,000 kwa ajili ya ukarabati wa shule mbalimbali, Sh milioni 181,000,000 kwa ajili ya umaliziaji na Sh milioni 400,000,000 kwa ajili ya shule mpya moja itakayokuwa na madarasa 16, vyoo 21 na jengo la utawala na kwamba jumla ya fedha toka serikali kuu ni Sh milioni 661,000,000.

Wanafunzi shule ya msingi Mafisa A.

Hata hivyo, Serikali haina budi kuweka mkakati na kipaumbele zaidi katika kutatua au kuondoa kabisa changamoto ya vyoo mashuleni, kwa kuelekeza bajeti zake na miradi mbalimbali inayoendelea katika swala hilo pia, ili kuweza kuinua zaidi kiwango cha elimu na ufaulu wa wanafunzi, kwa kutoa elimu bora na sio bora elimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles