24.6 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Majukumu ya Jaji yazima shauku hatima uenyekiti wa Lipumba

PATRICIA KIMELEMETA -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeahirisha kutoa uamuzi juu ya uhalali wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, baada ya Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Benhaj Masoud, kupangiwa majukumu mengine.

Kesi hiyo namba 13/2016, ilifunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kwa upande unaomuunga mkono Maalim Seif, ukipinga kutambuliwa kwa Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho.

Katika kesi hiyo, upande wa waleta maombi (Maalim Seif) wanawakilishwa na Daim Khalfan na wajibu maombi (Lipumba) wakiwakilishwa na Mashaka Ngole, wakati Serikali ikiwakilishwa na Rehema Mtulia.

Mahakama hiyo ilikuwa itoe uamuzi wa uhalali wa Lipumba kwenye chama hicho jana, lakini ilishindikana baada ya Jaji Masoud ambaye alitakiwa kusoma uamuzi, kupangiwa majukumu mengine.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 17, mwaka huu, kwa ajili ya kutoa uamuzi huo.

Nje ya Mahakama, akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF upande wa Maalim Seif, Mbarara Maharagande, alisema kesi hiyo imeahirishwa kwa sababu Jaji ana majukumu mengine.

Alisema upande wa Maalim Seif umefungua kesi nyingi mahakamani hapo na nyingine tayari zimeshatolewa uamuzi, ikiwamo ya kutokuwa na uhalali wa Bodi ya Wadhamini wa CUF walioteuliwa na Lipumba.

“Tunaamini Mahakama itatoa haki katika kesi hii kwa kumuweka pembeni Lipumba ili chama kiweze kuendelea na majukumu yake, hivyo basi matarajio yetu ni kupokea uamuzi huo kwa sababu haki itakuwa imepatikana,” alisema Maharagande.

Akizungumzia historia ya chama hicho, Maharagande alisema kuwa, Maalim Seif ndiye mwasisi wa chama hicho, ambaye alimkaribisha Lipumba mwaka 1995.

Alisema hatua hiyo ilikuja baada ya miaka 8 ya harakati ya kudai ya mabadiliko ya mfumo wa kisiasa nchini na kuingia kwenye mfumo vyama vingi ndani ya Tanzania, hali iliyosababisha Maalim Seif kukaa kizuizini miaka mitatu.

“Tumeshangazwa kuona Lipumba akiyafanya aliyoyafanya, licha ya kukaribishwa mwaka 1995, lakini mwaka 2015, aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wakati chama kipo kwenye harakati za uchaguzi mkuu,” alisema.

Alisema wanachama walimuomba asifanye hivyo, lakini alikataa na kukiacha Chama katika kipindi kigumu, huku Dk. Duni Haji akiwa mgombea mwenza wa aliyekuwa Mgombea wa Rais anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa. Alisema japo walipata mafanikio, lakini kitendo cha kuondoka kwake kilisababisha mvurugano ndani unaosababisha shughuli za chama hicho kuyumba mpaka sasa.

Akizungumzia mkanganyiko wa uamuzi wa juzi uliotolewa mahakamani hapo kuhusiana na bodi ya wadhamini, Maharagande alisema kuwa, Mbunge Ali Saleh alifungua kesi ya kuhoji uhalali wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini walioteuliwa na Lipumba na kusajiliwa na Mamlaka ya Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), huku majina yaliyowasilishwa na Maalim Seif hayakusajiliwa.

“Bodi iliyokuwepo ni ya Lipumba ambayo ilisajiliwa na Rita, ya kwetu haikusajiliwa, ndiyo maana bodi ya Lipumba imeondolewa kwa sababu haikuwepo kisheria,” alisema Prof.

Lipumba alipotangaza kujiuzulu uenyekiti wa CUF, Agosti 6, 2015, kwa madai kuwa haungi mkono makubaliano yaliyofikiwa kumuunga mkono Lowassa.

Hata hivyo, Juni 13, 2016, alirejeshwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa madai kuwa Mwenyekiti huyo ni halali kwa mujibu wa Katiba ya CUF, hususan ibara ya 117 (2), ambayo inaonyesha mchakato wa kujiuzulu kwake ulikuwa bado haujakamilika. Kwa mujibu wa kifungu hicho, ili uamuzi wa kujiuzulu ukamilike, ni lazima kuitishwe mkutano mkuu wa Taifa wa chama hicho ambao ndio wenye mamlaka ya uteuzi wake, ukae ili kuridhia au kukataa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles