23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

MAJAMBAZI YAPORA DHAHABU, YAJERUHI TISA MGODINI

 

 

NA RAYMOND MINJA-IRINGA

WATU tisa wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa baada ya kuvamiwa na majambazi yaliyokuwa na silaha za moto na za jadi katika machimbo mapya ya dhahabu yaliyoko katika Kijiji cha Nyakavangala, Isimani, Wilaya ya Iringa Vijijini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, alisema tukio hilo lilitokea saa mbili usiku juzi baada ya majambazi hayo kuwavamia wafanyabiashara na kuanza kuwapiga na kuwapora fedha na dhahabu.

Kasesela alisema majambazi hayo yalifanikiwa kupora Sh milioni 81, gramu 490 za dhahabu na simu nne za mkononi kutoka kwa wafanyabiashara hao.

Alisema kwa mujibu wa mashuhuda, majambazi hayo yaliwapiga ili wawaonyeshe alipo mfanyabiashara aliyekuwa na kiasi kikubwa cha fedha, Mginya Paulo, ambaye peke yake walimpora Sh milioni 75.

Kasesela alisema majambazi hayo yaliletwa na gari nyeusi aina ya Land Cruiser na baada ya kupora yalitorokea kusikojulikana kwa kutumia pikipipi zilizokuwa mgodini hapo.

“Nilipigiwa simu na watu 20 na kuniambia wamevamiwa na majambazi wenye silaha za moto na za jadi.

“Niliwasiliana na Jeshi la Polisi wakafanikiwa kwenda huko ingawa si kwa muda mwafaka kutokana na jiografia ya eneo husika na walipofika wakakuta majambazi hayo yameshapora fedha, dhababu na simu na kutokomea,” alisema.

Kasesela alisema polisi wanaendelea na msako mkali ili kubaini majambazi hayo na wanaamini lazima yatapatikana na kufikishwa katika mkono wa sheria.

Pia alisema wameshaanza mchakato wa kujenga Kituo Kidogo cha Polisi kwa kushirikiana na wachimbaji hao ili kupeleka askari watakaokuwa wakilinda eneo hilo.

“Pili tutaanzisha daftari la utambuzi ili watu wajuane wao kwa wao, maana inaonekana majambazi wengine walikuwa nao hapo hapo na ndiyo maana walikuwa wanamlenga mtu mmoja kwa kuwa walikuwa wanajua ana kiasi kikubwa cha fedha, sasa ili kumaliza hilo, wanatakiwa kutengeneza uongozi wao utakaowasimamia na kuanzisha daftari la utambuzi wa watu walioko katika machimbo hayo,” alisema.

Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Mginya ambaye ni mkazi wa Morogoro, Bakari Mzee (Isimani), Sungura Shija (Geita), Fadhili Ramadhani (Morogoro), Nsurwa Msanga (Bariadi), Odrick Michael (Iringa), Kitandu Mabula (Tanga), Daniel Masegu (Simiyu) na Elia Mushi mkazi wa Kilimanjaro.

Kasesela alisema kuwa hali ya Bakari ni mbaya kutokana na kipigo alichopewa na majambazi hayo kwa sababu tangu alipozimia juzi hadi jana alikuwa hajazinduka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles