25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

BANDARI YA DAR ES SALAAM KUFANYIWA UPANUZI

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa

 

 

Na KOKU DAVID – DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) jana ilitiliana saini mkataba na Kampuni ya China Harbour Engineering ambayo itafanya wa upanuzi wa kina cha bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema kuwa Serikali imeamua kutanua bandari ya Dar es Salaam ili kuiwezesha kubeba mizigo mingi.

Alisema mradi huo utagharimu karibu Sh bilioni 336 na unatarajia kuanza baada ya Rais Dk. John Magufuli kuweka jiwe la msingi mwanzoni mwa mwezi Julai na kwamba utakamilika baada ya miezi 36.

Profesa Mbarawa alisema bandari ya Dar es Salaam haina uwezo wa kubeba mizigo mingi kutokana na kuwa ina kina kifupi, ikiwa ni pamoja na miundombinu isiyoendana na wakati.

Alisema wanatarajia kuijenga upya gati namba sifuri ambayo itakuwa ikitumika kushushia magari na kuchimba kina katika gati namba moja hadi saba na kufikia urefu wa mita 15 pia wataboresha miundo mbinu.

“Katika gati namba nane kina chake ni mita 10.5 hadi 11 wakati kina kinachotakiwa ni mita 12 hadi 13 hivyo ili kuifanya bandari yetu kukimbiliwa na kila mtu tutarefusha kina hadi kufikia mita 15 pamoja na kuboresha miundombinu, kujenga reli ya kisasa na kuweka mashine zitakazoweza kupakuwa mizigo kwa muda mfupi.

“Pesa za ujenzi wa mradi huu zimetokana na mkopo wa dola milioni 345 ambazo Serikali imekopeshwa na Benki ya Dunia na kwamba tunatarajia ujenzi huu utakamilika kwa muda uliopangwa,” alisema Profesa Mbarawa.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, alisema kuwa mradi huo wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam utakapokamilika, wanatarajia ongezeko la mizigo kutoka tani milioni 14 hadi 28 ifikapo mwaka 2022.

Alisema bandari hiyo hupokea meli 30 hadi 40 za mwambao na za kimataifa, lakini takribani meli nane hadi 10 husubiria nje kutokana na kina cha mita 10.5 hadi 11 kilichopo bandarini hapo ambacho hakina uwezo wa kupokea meli nyingi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya China Harbour Engeneering, Xu Xinpei, alisema kuwa baada ya makubaliano hayo, wanatarajia kukamilisha ujenzi huo kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.

Alisema wataijenga bandari hiyo katika viwango vya juu na kuifanya kuwa ya kwanza kwa ubora na huduma nzuri katika eneo la Afrika Mashariki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles