Na JUDITH NYANGE, MWANZA
MFANYABIASHARA raia wa China, Maihaimiyan Mai (33) mkazi wa mtaa wa Mahina Kata ya Mhandu wilayani ya Nyamagana ameuawa kwa kupigwa risasi kifuani nyumbani kwake na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao pia walijeruhi watu wengine watatu na kupora Sh milioni 1.1.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Augustino Senga, alisema tukio hilo lilitokea Novemba 27, mwaka huu usiku wakati Mai akitoka kwenye shughuli zake za biashara.
Alisema wakati Mai alipokuwa akiingia kwenye lango la nyumbani kwake alikutana na watu watatu waliovamia nyumbani kwake huku mmoja kati yao alionekana kuwa na silaha ambaye alifyatua risasi moja iliyompiga kifuani na kufariki dunia papo hapo.
“Majambazi hao walimshambulia kwa kumpiga na rungu sehemu mbalimbali za mwili, Ayoni Mai (29) ambaye ni mdogo wa marehemu, pamoja na mke wake Christina Kinyonge na kuwapora Sh miloni 1.1 na simu mbili za mkononi.
“Pia walimjeruhi mlinzi wa nyumba hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Pascal (35) kwa kumpiga risasi iliyomparaza kisogoni wakati akitaka kuruka ukuta na kukimbia.
“Majeruhi wote watatu wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando wakiendelea kupatiwa matibabu na mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi, ” alisema Senga.
Senga alisema jeshi la polisi linawasaka watuhumiwa wote waliohusika katika tukio hilo.
Aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mwanza kutoa ushirikiano kwa jeshi la hilo kuhusu taarifa za wahalifu hao waweze kuwakamata na kufikishwa katika vyombo husika kwa hatua za sheria.