25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 17, 2022

MAISHA YA GHETO YANAVYOCHOCHEA MAAMBUKIZI YA TB

Mratibu wa Kifua Kikuu (TB) na Ukoma, Mkoa wa Ki-TB Ilala II na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Mary Kajiru.

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

SI jambo la ajabu hata kidogo ukifika katika mitaa yetu ya ‘Uswahilini’ kama Manzese, Tandale, Magomeni na kwingineko, kukuta watu zaidi ya watano wakiishi katika chumba kimoja.

Ni hali ambayo wengi wetu ama tunaishi au tumewahi kuishi katika mazingira ya namna hiyo na tumeshaizoea.

Kundi la vijana ndilo hasa ambalo hupenda kuishi kwa mtindo huo ingawa lipo kundi lingine la mafundi ujenzi ambao mara nyingi huhama kutoka eneo moja hadi lingine kulingana na kazi zao.

Wasemavyo vijana

Johnson Elius (25), ni kijana mwenyeji wa Mkoa wa Iringa ambaye amekuja Dar es Salaam kutafuta maisha na wenzake wengine watano.

Kijana huyo anasema awali walipofika jijini humo hawakuwa na mahala pa kulala hivyo walilazimika kulala katika vituo vya daladala.

Anasema kwa kuwa hakuwa amezoea mazingira ya jiji hilo ilikuwa ngumu kwake hasa kukimbizana na magari kuuza bidhaa yake hiyo.

Anasema ili kuokoa fedha ilimlazimu kushirikiana na mwenzake kupanga chumba kimoja katika maeneo ya Manzese ambacho hunalipa Sh 40,000 kila mwezi.

Wakati mwingine unaweza kukuta watu zaidi ya watano wanapanga chumba kimoja ikifika wakati wa kulipa kodi wanachangishana maisha yanaendelea.

Wanafunzi nao wanatabia ya kuishi maisha kwa mtindo huo, hasa wale wanaoishi mbali na shule.

Ni hatari kwa afya

Mratibu wa Kifua Kikuu (TB) na Ukoma, Mkoa wa Ki-TB Ilala II na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Daktari Mary Kajiru anasema mtindo huo wa maisha si salama kwa afya.

Anasema huongeza uwezekano wa wahusika kuambukizana magonjwa mbalimbali hasa Kifua Kikuu (TB), iwapo mmoja wao atakuwa na vimelea vya ugonjwa huo.

Anasema TB ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria ambao kwa kitaalamu wanaitwa Mycobacterium Tuberculosis.

Anasema ugonjwa huu huenezwa kwa njia ya hewa hivyo watu wanapoishi wengi ndani ya chumba kimoja na mmoja wao akawa ana maambukizi haya ni rahisi kuwaambukiza wengine.
Anasema mbaya zaidi ni pale ambapo chumba wanachoishi kinapokuwa na madirisha madogo ambayo hayapitishi hewa ya kutosha.

Makundi mengine

Anasema watu wanaokunywa pombe kupindukia nao wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya Kifua Kikuu  kuliko wale wanaokunywa kwa kiasi.

Anataja kundi jingine lililopo katika hatari ya kupata ugonjwa huo kuwa ni lile la wavuta sigara na wanaojidunga na kuvuta dawa za kulevya.

“Watu wanaokunywa pombe kupindukia, wanaojidunga sindano au kuvuta dawa za kulevya na wale waovuta sigara mara nyingi hupendelea kukaa au kuishi pamoja ‘gheto’.

“Wengi huwa na lishe duni kwa sababu tabia hizo huwafanya wakose au wapungukiwe na hamu ya kula chakula, hivyo miili yao hudhoofu kwa kukosa virutubisho muhimu vinavyohitajika,” anasema.

Anasema kwa kuwa miili yao huwa dhaifu, hali hiyo huchochea uwezekano wa kushambuliwa na magonjwa ikiwamo TB.

“Wale wanaovuta sigara ndiyo hujiweka kwenye hatari pia kwani ule moshi unaoingia ndani ya miili yao huenda moja kwa moja kwenye mapafu na kufanya uharibifu,” anasema.

Wenye VVU 

Anasema watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) nao huwa ni rahisi kwao kupata ugonjwa wa TB, kwa kuwa magonjwa haya hushabihiana.

Kwenye misongamano

“Watu wanaokaa kwenye maeneo yenye msongamano mkubwa kama sokoni, kwenye daladala, wazee wenye miaka zaidi ya 65, watoto chini ya miaka mitano, nao wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya TB,” anasema.

Anataja kundi lingine kuwa ni la watu wenye magonjwa ya muda mrefu kama kisukari, saratani na mengineyo lakini hawa ni kwa kiwango kidogo.

TB ni tishio duniani

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha kila mwaka watu milioni tisa huambukizwa ugonjwa huu. 

Shirika hilo linaeleza kwamba changamoto iliyopo ni kwamba kati ya watu hao milioni tisa, milioni tatu huwa hawapati matibabu kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa mujibu wa WHO mwaka 2012 watu milioni 8.6 waliambukizwa ugonjwa huo na watu milioni 1.3 kati yao walifariki dunia wengi ni waishio katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania.

Hali ilivyo nchini

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk. Beatrice Mutayoba anasema pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa kudhibiti ugonjwa huo, bado ni tatizo kubwa nchini.

Anasema takwimu za WHO zinaonesha Tanzania inashika nafasi ya 18 katika nchi 22 duniani zenye wagonjwa wengi wa TB na inashika nafasi ya sita barani Afrika.

“Kuanzia mwaka 1980, Kifua Kikuu kimekuwa kikiongezeka, ambapo hadi 2013 waligundulika wagonjwa 65,000 ikilinganishwa na wagonjwa 11,000 ambao waligundulika mwaka 1983,” anasema.

Anafafanua kwamba mpango huo umepewa jukumu la kuwezesha na kuhakikisha uchunguzi unafanyika mapema kwa wagonjwa na wanaogundulika kuwa na TB wanapata matibabu mapema.

“Mpango unatakiwa kuhakikisha wamepona kabisa ugonjwa huo ili kuhakikisha tunautokomeza kabisa nchini,” anasema.

Dk. Mutayoba anasema katika kutimiza lengo hilo miaka mitano ya hivi karibuni wagonjwa wapatao 63,000 wamekuwa wakisajiliwa kila mwaka kwa ajili ya matibabu.

“Kwa miaka 10 mfululizo takwimu zilizokuwa zimekusanywa kutoka vituo vya kutolea huduma za afya zinaonesha Mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi.

“Mikoa mingine ni Mwanza, Shinyanga, Mbeya, Morogoro, Mara, Arusha, Tanga , Kilimanjaro na Iringa. Mikoa hiyo 10 imechangia asilimia 60 ya wagonjwa wote kwa takwimu za mwaka 2013,” anabainisha.

Dk. Kajiru anasema ugonjwa huo umegawanyika katika makundi makuu mawili, ambayo ni TB ya ndani ya mapafu na TB ya nje ya mapafu.

“TB ya ndani ya mapafu ni hatari zaidi kuliko ile ya nje ya mapafu ambayo mara nyingi vimelea huweza kukaa sehemu yoyote ya mwili kwa mfano kwenye jicho, uti wa mgongo, shingoni (kwenye tezi) au kwenye mifupa,” anasema,

Anaongeza; “TB ya ndani ya mapafu huambukiza kwa urahisi kuliko ya nje ya mapafu. Vimelea vya TB vinavyokaa kwenye makohozi ni vibaya zaidi kuliko vinavyokaa sehemu zingine za mwili. Mgonjwa anapokohoa hutoa vimelea kwa wingi (zaidi ya milioni) kwa njia ya mdomo, si rahisi kuviona kwa macho kama nilivyoeleza hapo awali,” anasema.

Anasema lakini vimelea ambavyo hukaa nje ya mapafu huwa si rahisi kusambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine labda kama vinakuwa vimesambaa hadi kwenye mapafu.

“Kwa mfano vimelea vikikaa jichoni, mtu ataona jicho lake linavimba mara kwa mara, lakini asijue ni TB, ikikaa kwenye uti wa mgongo wengi huhisi maumivu ya mgongo,” anasema.

Dalili

Daktari huyo anasema mtu mwenye maambukizi ya TB ya mapafu hupata kikohozi, homa za mara kwa mara jioni zaidi ya wiki mbili, hutokwa jasho jingi kuliko kawaida usiku, hupungua uzito na hutoa makohozi yaliyochanganyika na damu.

Anasema dalili za TB ya nje ya mapafu zinategemea jinsi mgonjwa anavyojieleza, kuna ambao hulalalamika kupata maumivu ya mgongo na kwamba wakifanyiwa kipimo cha X-ray hugundulika kuwa wana TB ya uti wa mgongo.

Anaongeza “Wengine huvimba tezi shingoni, karibu na sikio, au kwenye makwapa. Huwa tunachukua maji maji au kinyama kidogo toka sehemu iliyoathirika na kupima.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,727FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles