29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Mahakimu watakiwa kuzingatia maadili

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM


NAIBU Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Joachim Tiganga, amewataka mahakimu kuzingatia maadili katika utoaji haki ili kulinda heshima yao na kuwajengea wananchi imani juu ya mhimili huo.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo mahakimu wanawake wa Dar es Salaam kuhusu maadili ya viongozi wa umma yaliyoendeshwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Alisema ikiwa mahakimu hawatatenda haki katika uamuzi wanaofanya, watasababisha watu kujichukulia sheria mkononi hali itakayoleta utovu wa maadili kwa wananchi wa kawaida ambao si hulka yao.

“Nafahamu kuwa Mahakama ya Tanzania iko kwenye kampeni kubwa ya kuhubiri na kusimamia maadili kwa viongozi wa umma na watumishi wake.

“Mafunzo haya yamekuja wakati mwafaka na hii ni ishara kwamba maadili sasa ni wimbo wa kila taasisi ya umma, hasa kwa viongozi,” alisema Tiganga.

Aliwataka kuzingatia suala la mgongano wa masilahi kwa sababu ni moja ya mambo yanayosababisha ukiukwaji wa maadili.

Tiganga alisema tatizo hilo limekuwa likizikumba nchi nyingi duniani na lina athari kubwa kwa maendeleo ya nchi kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Alisema mgongano huo hutokea pale kiongozi mwenye dhamana anapofanya uamuzi na kutumia nafasi yake kwa masilahi yake binafsi au ndugu, jamaa na marafiki.

“Unapofanya uamuzi kwa kulinda masilahi ya mtu fulani basi ujue kuwa umejiingiza katika mgongano wa masilahi. Mgongano wa masilahi unasababisha watu kukosa haki na fursa sawa.

“Jambo hili lisipodhibitiwa linasababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya utoaji haki,” alisema.

Pia alisema ni vema kiongozi yeyote kujaribu kwa kiasi kikubwa kuepuka hali hiyo na wafanye uamuzi kwa kuzingatia matakwa ya sheria zinazohusika bila upendeleo wala ubaguzi ili kujenga taifa lenye maendeleo endelevu kwa wote.

Naye Katibu wa Ukuzaji Maadili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Waziri Kipacha, alisema mafunzo hayo yanakusudia kuongeza ushiriki wa wanawake katika kukuza na kusimamia maadili kutokana na utafiti walioufanya na kuonesha kuwa ni asilimia moja pekee ya viongozi wanawake ndio wanaoshiriki katika utoaji wa taarifa za ukiukwaji wa maadili.

“Kwa sababu wanawake ni wazazi na walezi, mafunzo haya yatawasaidia kuwalea watoto katika maadili, kwa sababu naamini maadili yanajengwa tangu watoto wanapokuwa wadogo, tutapata jamii ya watu wenye maadili,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,404FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles