29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Mahabusi ajinyonga akiwa rumande

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo.

Na ELIYA MBONEA, ARUSHA

MAHABUSI  Victoria Edward (51),  mkazi wa Lemara jijini hapa  amekutwa amejinyonga hadi kufa akiwa ndani ya choo cha mahabusu ya wanawake katika Kituo Kikuu cha Polisi  Arusha mjini.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana mjini hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha kujinyonga kwa mahabusi huyo ambaye alikutwa na kipande cha nguo.

Alisema tukio hilo lilitokea Agosti 24, mwaka huu saa 6:30 usiku  ambapo mahabusi huyo aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kuchoma nyumba alikutwa akiwa amejinyonga kwa kutumia kipande cha nguo yake.

“Ni kweli uchunguzi wa awali unaonesha mahabusi wenzake walikuwa wamelala na mahabusi mmoja alipostuka usingizini alimwona mwenzake akiwa amening’ing’inia pembeni mwa mlango wa choo,” alisema Kamanda Mkumbo na kuongeza:

“Baada ya tukio hilo mahabusi walipiga kelele za kuomba msaada ndipo askari wakaingia ndani na kumkuta Victoria amejitundika, walimfungua kipande cha nguo alichokuwa amejifunga kwenye nondo juu ya mlango,” alisema.

Kamanda Mkumbo alisema askari hao baada ya kufanikiwa kumshusha walimkimbiza hospitalini, ili kunusuru maisha yake lakini hata hivyo baada ya kupimwa na daktari ilibainika kuwa tayari alikuwa ameshafariki dunia.

Marehemu alifikishwa kituo cha polisi Agosti 21, mwaka huu akituhumiwa kuchoma maduka manne na nyumba inayomilikiwa na mfanyabiashara Erasto Kivuyo (30), mkazi wa Lemara pamoja na nyumba nyingine inayomilikiwa na Edward Wenga (58).

Kutokana na nyumba hizo kuchomwa moto mali zote zilizokuwa ndani ziliteketekea na thamani ya mali hizo ilikuwa bado haijajulikana.

Akielezea kuhusu chanzo cha kuchomwa moto nyumba hizo Kamanda Mkumbo alisema kuwa mgogoro uliokuwapo wa umiliki wa mali kati ya wanandoa yaani marehemu na mumewe Wenga huenda ulichangia.

“Hawa wanandoa walikuwa na kesi mahakamani ikihusisha mgogoro wa ndoa yao,” alisema Kamanda Mkumbo.

Mwili wa marehemu Victoria umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru ukisubiria taratibu za maziko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles