26.1 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli selema

Pg 1Na Waandishi Wetu

MARA baada ya kuteuliwa na chama chake kuwania urais, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, alianza kwa kuimba kibwagizo ‘aliselema’.

Hili ni neno la kisukuma lenye maana ‘anakwenda’  na wafuasi wake wakiitikia ‘alija’  wakimaanisha anaenda, ndiyo hivyo hivyo jana mgombea huyo alivyofungua kampeni zake kwa mbwembwe katika viwanja vya Jangwani, Jijini Dar es Salaam.

Kama ilivyo kwa kibwagizo chake hicho, Dk Magufuli na viongozi wengine wa chama hicho waliozungumza katika mkutano huo walisema watashinda Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.

Dk. Magufuli ambaye katika hotuba yake alizidisha dakika 33 baada ya saa 12:00 jioni ambapo kisheria mikutano ya kampeni inatakiwa kumalizika saa 12:00 kamili.

Dk. Magufuli alisema anajua shida za Watanzania na wananchi wanataka mabadiliko ambayo kupitia kwake watayapata bila kubadili chama.

Aliwataka wananchi kuacha jaziba katika kufanya uamuzi na kuichagua CCM ili kuleta maendeleo ya kweli.

“Uwingi wenu unaonyesha kwamba mmekubali kupata mabadiliko ya uhakika….hali iliyonifanya nikumbuke maneno ya Rais wa pili Ali Hassan Mwinyi kwamba ‘Kila zama na kitabu chake’ hivyo mkusanyiko huu unaonyesha kwamba Watanzania wanataka kitabu kipya kutoka kwangu,” alisema.

Alisema maendeleo hayo yamefanikishwa na viongozi waliopita katika serikali zilizopita kwa Tanzania bara na Tanzania visiwani tangu kuasisiwa kwake.

“Shida za Tanzania nazijua ….natambua Watanzania wote wanataka maisha mazuri, kwa wale wenye bodaboda wanatamani kumiliki gari na wapangaji wanatamani kujenga nyumba lakini natambua maendeleo hayo hayatafanikiwa kama kutakuwa na ufisadi,” alisema.

Dk. Magufuli alisema akichaguliwa kuongoza serikali hiyo atapambana na ubadhirifu na ufisadi ili awezeshe kupatikana mabadiliko kwa kupitia CCM.

“Nataka kumaliza matatizo ya mikopo, kushughulikia ajira. Kuwasaidia wakulima kwa kuwawezesha kupata umiliki wa ardhi, pembejeo, masoko ya uhakika na serikali yangu haitawakopesha tena wakulima na mama ntilie hawatawasumbuliwa na Mgambo pindi nitakapoingia watatafutiwa kazi nyingine,” alisema.

Magufuli alisema akichaguliwa atawawezesha wanamichezo kiuchumi na kuondoa dhana ya kutumika kwenye maendeleo na si katika majukwaa ya kisiasa peke yake.

“Ninafahamu Watanzania wanataka mabadiliko bora ya kweli ya maendeleo, nimefanya mambo mengi ya kuwezesha kulinda umoja wa kitaifa ikiwamo na kutokuwa mkabila,” alisema.

Alisema kuwa anatarajia kuunda serikali itakayolinda Muungano kwa kushughulikia dosari zilizopo ikiwamo na kulinda ulinzi na usalama na hataingilia kazi za Bunge ila ataliwezesha kusimamia serikali.

“Nitafunga mafisadi na majizi haraka…Nitalala nao polepole ili wajue Tanzania ni mahali pa kuishi salama hasa kwa wananchi wanyonge,” alisema.

Alisema kuwa ataimarisha majeshi yote ikiwamo Polisi kwa kupewa vyombo vya kisasa na silaha za kisasa, Jeshi la Ulinzi na Usalama (JWTZ) ataongeza mambo mazuri yaliyofanywa na serikali ya awamu ya nne, Jeshi la zimamoto na Magereza.

“Nikichaguliwa nitaimarisha sekta ya viwanda kwa kujenga viwanda vingi ili watanzania wapate ajira, tutaleta wawekezaji wengi ili wajenge viwanda na maofisa watakaochelewesha mahali pa kujenga watatafuta pa kuishi,” alisema.

Dk. Magufuli alibainisha kwa kuwezesha Tanzania ya Magufuli inakuwa ya viwanda atajenga viwanda vingi kwa nia ya kutengeneza ajira kwa asilimia 40.

Sekta ya Kilimo itaendelezwa kwa kuleta vitendea kazi vingi ikiwamo na kutumia benki ya wakulima atakayoitumia kutengeneza viwanda vingi vya kilimo.

Alisema sekta ya mifugo Tanzania katika Afrika inashikilia nafasi ya pili hivyo atawezesha sekta hiyo kujenga soko na viwanda vya nyama na maziwa.

“Hakuna sababu ya kusherehekewa wiki ya nyama au maziwa wakati bidhaa hizo hazipo nchini, nitashugulikia hilo ili watanzania wengi wapate ajira,” alisema.

Dk. Magufuli alisema suala la madini ya Tanzania atahakikisha yanatambulika na kufaidisha nchi, pia ataimarisha sekta ya Afya kwa kuziwezesha hospitali zilizopo kuwa za kisasa.

Pia alisema atahakikisha anatoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne kama ilani ya chama hicho ilivyoelekeza na kutimizwa katika awamu ya nne.

Katika sekta hiyo ya elimu alisema atajenga nyumba nyingi za walimu ikiwamo na kuondoa usumbufu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaocheleweshewa mikopo.

“Nitahakikisha pindi mwanafunzi anapoingia anapewa na pia nitahakikisha ninasiamamia ujenzi wa mabweni ya kisasa kwa wanafunzi kwa kutumia Mfuko wa hifadhi ya Jamii (NSSF),” alisema.

Alisema atasimamia maslahi ya kila mfanyakazi ikiwamo kwa madereva na atasimamia nishati ya gesi ili ihudumie wananchi wengi kwa kuwezesha viwanda vingi kujengwa.

“Barabara za lami zitakamilishwa na kuongezwa zaidi ikiwamo na madaraja, Barabara ya Chalinze itajengwa ikiwamo na barabara za juu saba (fly over) zitakamilishwa.

Dk. Magufuli aliwataka Watanzania kuchagua CCM ili aweze kusimamia ilani ya CCM ili Watanzania wapate mabadiliko katika serikali ya awamu ya tano ambayo itakuwa rafiki wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa na wadogo kwa kulinda maslahi na mali zao.

“Hiyo ndiyo Tanzania ninayoitaka….mimi kazi tu, kwa wafanyakazi nitalinda maslahi yao na kuyaboresha. Nitatetea na kulinda haki za  walemavu ikiwamo na kulinda uhuru wa habari.

“Wanahabari nitalinda umoja wao, na nitasimamia uhuru wao wa habari na ningeomba muunde umoja wenu ili nikichaguliwa mnieleze matatizo yenu kupitia umoja huo nione namna ya kuwasaidia,” alisema.

Dk Magufuli alibainisha kwamba mabadiliko ya kweli yanatakiwa kufanywa na mtu aliye na uzoofu katika utendaji na chama makini ambacho ni CCM.

Magufuli alisema kuwa kiongozi anayestahili kupewa nafasi ya kuongoza nchi hii ni Magufuli kwa kuwa ndiye mwenye uwezo wa kukuza uchumi.

“China imefikia hapo katika maendeleo makubwa ya kiuchumi lakini hawakubadili chama chao cha kikomunisti hivyo msidanganyike kwa kuwa wamefanikiwa kwa kukiacha chama chao hicho hadi leo.

“Watanzania tusiwe kama fundi selemala na Sanja aliyetaka kukarabati kabati lake. Wakati akikarabati mke wa Sanja alianguka na kuumia hivyo fundi akamkimbilia mke huyo kumsaidia.

“Alivua shati na kumfunga mkewe wa sanja mara ghafla akafika Sanja na kumshuhudia mkewe akihudumiwa na fundi kwa kumpuliza na shati akamfikiria vibaya.

“Ghafla akaingia Sanja akamkuta fundi akiwa amevua shati akimpepea mkewe akampiga na gogo akamuua mara mwanaye alipoingia alimwambia alikwenda kumtafuta baba yake ili kumwambia fundi alikuwa akimsaidia mkewe, Sanja alihuzunika sana, hivyo watanzania tusiwe kama Sanja kukiondoa CCM bila kutafakari tutajuta,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na Shabani Matutu, Tunu Nassor, Koku David, Veronica Romwald, Christina Gauluhanga na Elizabeth Hombo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles