23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Lazima wakae Ngao ya Jamii

WAKISHANGILIA GORI (4)Wachezaji wakishangilia baada ya mchezoNA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

LAZIMA wakae! Hizo ndizo tambo za mashabiki, makocha wa timu za Azam na Yanga kuelekea mchezo wao wa kuwania Ngao ya Jamii utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa 10.00 leo jioni.

Mchezo huo wa aina yake ni kwa ajili ya kufungua pazia la Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2015/16, utakaoanza rasmi Septemba 12, mwaka huu.

Kocha Mkuu wa Azam, Mwingereza Stewart Hall, amesema kuwa anataka kuendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji mfululizo kwa kuifunga Yanga leo na anaamini ya kuwa kikosi chake kimeiva kutimiza kazi hiyo.

“Wachezaji wangu wanapenda mechi kubwa kama hizi, Yanga ni timu kubwa tunaiheshimu, natarajia mchezo mgumu lakini naamini morali tuliyokuwa nayo itatimiza malengo tuliyojiwekea,” alisema.

Naye Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm, raia wa Uholanzi, amesema kikosi chake kimeimarika tofauti na kile kilichoshiriki Kombe la Kagame, hivyo anatarajia makubwa kwa timu yake.

“Huu mchezo utakuwa tofauti na ule tuliocheza kwenye Kagame, kikosi changu kipo vizuri sana, nadhani utakuwa mchezo mzuri kutokana na ubora wa timu zote, ila tumejipanga kushinda,” alisema.

Katika kujiandaa na mchezo huo, Azam iliweka kambi ya wiki moja Zanzibar, huku Yanga nayo ikitumia siku nane kujinoa vilivyo jijini Tukuyu, Mbeya.

Ikiwa Zanzibar, Azam ilicheza mechi tatu za kirafiki na kushinda zote dhidi ya KMKM (1-0), Mafunzo (3-0) na JKU (2-0), Yanga nayo vivyo hivyo ikizifunga Kimondo (4-0), Prisons (2-0) na Mbeya City (3-2).

Timu zote mbili zitaingia uwanjani zikiwa na hasira ya kulipizana kisasi, Yanga ikitaka kulipa kisasi cha kutolewa kwenye Kombe la Kagame dhidi ya matajiri hao kwa mikwaju ya penalti 5-3.

Azam nayo itataka kulipa kisasi cha kufungwa mara mbili mfululizo na Yanga kwenye Ngao ya Jamii, iliichapa bao 1-0 mwaka juzi na mwaka jana ikainyuka 3-0, mchezo uliomng’arisha Mbrazil Geilson Santos Santana ‘Jaja’, aliyefunga mawili.

Lakini Azam bado inashikilia rekodi ya kutisha tokea iliposhiriki Kombe la Kagame hadi kutwaa ubingwa huo, mpaka sasa haijafungwa kwenye mechi 13 mfululizo, ikiruhusu mabao mawili chini ya Hall na mechi 12 mfululizo bila wavu wake kuguswa.

Yanga yenyewe imecheza mechi 12, imeambulia ushindi mara tisa, sare moja na vipigo mechi mbili, ikiwa imeruhusu kufungwa mabao sita.

Ni wazi ya kuwa leo itakuwa ni vita kati ya mfumo wa 3-5-2 unaotumiwa na Azam uliowapa mafanikio makubwa sana ndani ya muda mfupi na ule wa 4-4-2 anaoutumia Kocha Pluijm wa Yanga.

Timu zote mbili zipo vizuri langoni, Yanga ikiwa na mkongwe Ally Mustapha ‘Barthez’ na Azam inaye kinda anayetikisa, Aishi Manula, ambaye alidaka penalti ya Mwinyi Haji, iliyoiondoa Yanga katika Kagame.

Azam ina mabeki bora zaidi wa kati wakiongozwa na Pascal Wawa na Agrey Morris, Yanga nayo imeimarisha eneo hilo kwa kumsajili beki Mtogo, Vincent Bossou, ambaye huenda akaanza na Kelvin Yondani ama Nadir Haroub au Mtogo huyo akasugua benchi kuwapisha wazoefu wa mechi hiyo.

Bado timu zote zinatakiwa kuwa makini sana kwenye eneo la ushambuliaji kutokana na takwimu kuonyesha wanakosa mabao mengi ya wazi.

Azam chini ya nahodha John Bocco, Kipre Tchetche, Shomari Kapombe na Farid Mussa (Wingbacks) kwenye eneo la ushambulizi, wameonyesha ubora, lakini wanakosa mabao mengi sana mchezoni.

Hata Yanga yenye Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Malimi Busungu, Deus Kaseke, nayo imekuwa vivyo hivyo, wanatengeneza nafasi nyingi bila kuzitumia vema.

Mpira ni mabao. Hivyo utakuwa ni mchezo wa mbinu nyingi na sidhani kama tunaweza kushuhudia idadi kubwa ya mabao kama wengi wanavyotarajia kutokana na ubora wa pande zote.

Kiungo cha Yanga kinaweza kuwa na Thabani Kamusoko, atakayecheza sambamba na Haruna Niyonzima, Salum Telela na Mbuyu Twite kama Said Juma atakuwa hayuko fiti.

Hivyo watakuwa na vita kubwa dhidi ya wale watano wa Azam, Jean Mugiraneza “Migi’, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Himid Mao, Farid na Kapombe, wanaocheza pembeni.

Migi na Himid wamekuwa bora sana kuilinda safu yao ya ulinzi isifikiwe kirahisi iwe kushoto, kulia na katikati. Uimara wao na safu ya ulinzi pia ndio umechangia mafanikio yao mpaka sasa.

Yeyote atakayemzidi mwenzake kwenye eneo hilo, basi ana nafasi kubwa ya kuibuka kidedea.

 

Rekodi nyingine

Kihistoria timu hizo zimekutana mara 14 kwenye ligi (misimu saba tokea Azam ipande), zote zimeshinda mara tano na sare nne kila mmoja, lakini Wanajangwani hao wamefunga mabao 20 na wapinzani wao 19.

Yanga ina ukame wa mechi tatu sawa na dakika 270 za kushindwa kuifunga Azam, mechi ya mwisho iliifunga Septemba 14 mwaka jana, ikishinda mabao 3-0 kwenye Ngao ya Jamii.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles