Magufuli: nimemsamehe Nape, kama atakengeuka itakuwa juu yake

0
1126

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Siku chache baada ya Rais John Magufuli kutangaza hadharani kuwasamehe wabunge wa January Makamba na William Ngeleja kwa kumtukana kwenye simu, hatimaye Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye naye ameomba radhi.

Mbunge huyo amekutana na kumuomba radhi Rais Magufuli leo Jumanne Septemba 10, Ikulu jijini Dar es Salaam, kutokana na kuhusika kwake katika mazungumzo yasiyofaa dhidi ya rais.

“Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kukubali ombi lake la kukutana naye na kunisikiliza,, kwa hiyo baada ya kupata fursa nimekuja nimemuona, na mle ambamo nilimkosea kama baba yangu nimeongea naye na amenielewa, ameniambia amenisamehe na amenipa ushauri ambao nitaufanyia kazi na naamini baada ya hapa mambo yatakwenda vizuri, na kwa kweli kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru sana sana, amenipa fursa kubwa, ndefu na ameongea maneno mengi kwangu na ushauri wake nimeuchukua” amesema Nape.

Kwa upande wake, Rais Magufuli amesema Nape amekuwa akiomba kukutana naye mara nyingi kupitia kwa watu mbalimbali wakiwamo wasaidizi wake, viongozi wastaafu na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kwamba baada ya kukutana naye na kumuomba radhi ameamua kumsahehe.

“Yote nimesamehe, huyu bado ni kijana mdogo, ana matarajio makubwa katika maisha yake, mimi nikiendelea kumshikilia kwenye moyo wangu kwanza ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu na tumefundishwa katika maandiko yote tusamehe saba mara 70, kwa hiyo nimemsamehe na Mungu amsaidie katika shughuli zake.

“Akafanye kazi zake vizuri, akalee mke wake na familia yake, akakitumikie chama, akawatumikie wananchi wa jimbo lake vizuri, mimi nimemsamehe, labda kama yeye atakengeuka hiyo itakuwa ni juu yake, lakini mimi kutoka moyoni mwangu nimeshamsamehe na nimemsamehe kweli,” amesema.

Nape anatuhumiwa kuzungumza kwenye simu na baadhi ya viongozi wastaafu wa CCM mazungumzo yenye nia ovu dhidi ya rais akiwamo January na Ngeleja ambao tayari waliomba radhi na kusamehewa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here