27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Magufuli awapa kibarua mabalozi wapya

Nora Damian-Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli amewataka mabalozi wapya kusimamia uchumi na kuhakikisha wanatengeneza ajira kwa Watanzania katika nchi wanazowakilisha.

Akizungumza jana wakati wa kuwaapisha mabalozi hao, alisema kila nchi walizopangiwa zina umuhimu wake, hivyo akawataka kujenga uchumi wa kisasa kulingana na mikakati iliyomo katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Mabalozi hao na nchi wanazowakilisha kwenye mabano ni Meja Jenerali mstaafu, Gaudence Milanzi (Afrika Kusini), Dk. Modestus Kapilimba (Namibia), Profesa Emmanuel Mbennah (Zimbabwe) na Dk. Benson Bana (Nigeria).

“Kahakikisheni mnatengeneza ‘employment’ (ajira) kwa Watanzania katika nchi mnazowakilisha, nendeni mkiamini kwamba mnawakilisha taifa lenye mwelekeo mpya katika maendeleo ya watu wake,” alisema Rais Magufuli.

Pia aliwataka mabalozi hao kuripoti haraka katika vituo vyao vya kazi badala ya kuanza kuaga kama ilivyokuwa ikifanyika kwa viongozi wengine.

“Pamekuwa na tabia mtu akishateuliwa balozi anataka akaage, mmeshateuliwa ninyi ni mabalozi, barua zao ziletwe mapema, ikiwezekana ndani ya wiki moja au mbili muwe mmeshaenda.

“Unapoteuliwa kafanye kazi kwani hii ndiyo maana ya hapa kazi tu,” alisema Rais Magufuli.

WAZIRI WA MAMBO YA NJE

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alimtaka Balozi Milanzi kuhakikisha mchakato wa kuanza kufundishwa Kiswahili Afrika Kusini unakamilika haraka.

“Utakapofika kazi ya kwanza tafuta ahadi ukutane na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, jambo hilo likamilike kabla ya Februari, tusifanye makosa mara ya pili kukosa fursa hiyo.

“Fursa hiyo ilikuwa imetupita, ni uzembe wetu wenyewe. Kiswahili wengi sasa wanakimanya na walimu wengi wa Kiswahili ni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” alisema Profesa Kabudi.

Pia alimtaka Dk. Kapilimba, kufuatilia sekta za uvuvi wa bahari kuu, nyama na biashara ya nafaka ili Tanzania iweze kufaidika na fursa hizo.

“Yalikuwa ni maamuzi halali ya rais kuanzisha ubalozi Namibia, tunayo maelekezo tutakayompa rais kuhusu Balozi wa Namibia asimamie nchi gani.

“Nyumba ya kuishi na ofisi ya kuanzia tumehakikisha zinapatikana ili kazi zisichelewe,” alisema Profesa Kabudi.

Kwa upande wa Zimbabwe, alisema mbali ya makubaliano ya SADC ya kupaza sauti nchi hiyo iondolewe vikwazo, lakini zipo fursa ambazo Tanzania inaweza kufaidika nazo.

“Nataka wala siyo naomba, ndani ya mwezi mmoja mtuletee ripoti ni maeneo gani ya fursa zilizoko Zimbabwe,” alisema Profesa Kabudi.

Kuhusu Dk. Bana anayekwenda Nigeria, alimtaka ahakikishe kunakuwapo na ushirikiano katika kubadilishana uzoefu kwenye kilimo, hasa zao la korosho kwani nchi hiyo imepiga hatua kubwa.

“Kwa mwaka Nigeria inazalisha tani 750,000 za korosho wakati sisi tuna tani 250,000. Tufuatilie jinsi ya kushirikiana katika zao la korosho, hasa kuongeza thamani,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema pia balozi huyo atapunguziwa baadhi ya vituo ambavyo vitahamishiwa katika balozi nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles