Magereza yaeleza ilivyowaanda gerezani wanafunzi waliofaulu

0
871

Nyembo Malecela -Kagera

JESHI la Magereza mkoani Kagera, limeeleza jinsi lilivyowasaidia kufaulu wanafunzi wanaoshikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi mwenzao wa Shule ya Seminari ya Kiislamu Katoro.

Wanafunzi hao walifanya mtihani wao wa taifa wa kidato cha nne wakiwa gerezani chini ya usimamizi wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

Akizungumza jana kwa niaba ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kagera, Mkaguzi wa Magereza na Mkuu wa Gereza la Bukoba, Jasson Kaizilege alisema waliwaandaa wanafunzi hao kisaikolojia na hatimaye kuweza kufaulu mitihani yao kwa kupata daraja ya pili na tatu.

“Tulipata taarifa kutoka kwa Ofisa Elimu Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, kuhusu watuhumiwa hao kuonekana lipo hitaji la wao wenyewe kufanya mtihani wakiwa gerezani,

jukumu tulilopewa kama magereza ni kuwalinda, kuwatunza pamoja na kuwaandalia mazingira mazuri ili waweze kufanya mtihani wakiwa magereza,” alisema Kaizilege.

Alisema waliandaa vyumba kwa mfumo wa madarasa, madawati na vitendea kazi vyote vinavyohusiana na mitihani.

Lakini wakati wa maandalizi waliwasiliana sana na ofisi ya Ofisa Elimu Mkoa ili kuhakikisha mazingira yako vizuri wanafunzi hao (watuhumiwa) kuweza kufanya mitihani vizuri.

“Kubwa kuliko yote tulilolifanya sisi ni kuwaandaa wanafunzi hao kisaikolojia kwa kuwa ni vijana wadogo, kulingana na matatizo waliyonayo na kufanya mitihani wakiwa gerezani walihitaji msaada mkubwa sana wa kisaikolojia.

“Tulikuwa tunazungumza nao mara kwa mara, hasa mimi ilinichukua muda mwingi, nikiwa kama kiongozi pia kama mzazi kuzungumza sana na hawa vijana, kuwapanga, kuwatunza, kwa akili zao kuonekana wametulia hadi wenyewe wakapenda kufanya mitihani.

“Baada ya kukamilisha taratibu zote za mitihani, nilipewa hadhi ya kuwa mkuu wa shule Kituo cha Mtihani cha Magereza, nilipata barua ya idhini kutoka Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), ukaguzi ukafanyika, tukaandaa maabara na vifaa vilivyokuwa vinatakiwa kwa ajili ya kufanyia, kwa usalama wetu tukajiridhisha kuwa ni salama. Kwa kuwa tulikuwa na kibali, mnamo Novemba 4, mwaka jana mitihani hiyo ikaanza.

“Vijana (watuhumiwa) tuliwatengea muda mzuri, mazingira mazuri, jambo kubwa lilikuwa ni kuwaweka sawa wahalifu wengine wajue kuwa gerezani hapa kuna kituo cha mtihani.

“Katika gereza hili tuna wahalifu zaidi ya 800, hivyo tulitakiwa eneo hili libadilike kutoka gereza kuwa darasa la kufanyia mitihani,” alisema Kaizilege.

Alisema kuwa wamejifunza kuishi na wahalifu, walikubaliana nao wakawa watulivu vipindi vyote vya mitihani hadi wakaguzi wa mitihani wakawa wanashangaa.

“Tulipata wasimamizi na wakaguzi kama ilivyokuwa kwa vituo vingine vya mitihani, kwa taratibu zetu za usalama, wanakuja tunapekuana tukiridhika basi tunawaruhusu waendelee na shughuli zilizowaleta na mimi ndiyo nilikuwa msimamizi mkuu katika kituo hiki,” alisema Kaizilege.

Alisema walipata faraja baada ya matokeo ya mtihani kutoka kwa maana vijana waliokuwa wakiwaandaa wamefanya vizuri.

“Mmoja alipata daraja la tatu la pointi 25, mwingine daraja la tatu la pointi 23, wengine watatu wakapata daraja la pili la pointi 21 na mwingine akapata daraja la pili la ponti 19, matokeo haya yalikuwa faraja kwangu.

“Tulijiuliza hawa vijana pengine wangekuwa nje wangefanya vizuri sana, japokuwa sio lazima huenda wangekuwa nje wasifikie ufaulu huu.

“Kwanini nawaza huenda wasingefaulu vizuri, kwa sababu huku ndani walikuwa wao na mitihani, wao na mkuu wao wa magereza na mazingira yao na mitihani, nafikiri waliweka umakini sana kwenye suala hilo.

“Lakini kama wangekuwa nje kulikuwa na mazingira mengi yanayowazunguka, kama wazazi wao, wenza wao, marafiki zao, pengine wakifikiria chakula na mazingira mengine ya shuleni huenda wangepata wasiwasi ambao ungepelekea wasifanye vizuri.

“Hapa tulikuwa na imani na mazingira tuliyowaandalia ya kuwatunza kisaikolojia ndiyo yamewapelekea kufanya vizuri, tumewapa faraja kubwa sana,” alisema Kaizilege.

Pamoja na hali hiyo, Kaizilege alisema kuwa pia wapo baadhi ya watuhumiwa huingia magerezani hawajui kusoma wala kuandika, hivyo wamekuwa wakiendesha madarasa ndani ya gereza na kutoa taarifa kwa Ofisa Elimu Mkoa kila mwisho wa mwezi.

Alisema wapo walimu, wanafundishana kusoma na kuandika na fursa nyingine nyingi kwa hiyo suala la elimu katika magereza haliwapi shida.

“Kwa upande wa wanafunzi hao, matokeo hayo wameyapokea kwa furaha sana kwa sababu mwanzoni kabisa walikuwa wamekata tamaa, walisema wapo gerezani hivyo hawawezi kufanya mitihani, lakini tukawaweka vizuri kisaikolojia wakakubali changamoto iliyo mbele yao na kuikabili.

“Furaha hiyo imeonekana pia kwa wazazi wa wanafunzi hao kwa siku ya Jumamosi na Jumapili ambapo walikuja kuwasalimilia na kuwapongeza,” alisema Kaizilege.

Wanafunzi hao wanatuhumiwa katika mauaji ya mwanafunzi mwenzao, Mudy Muswadiku.

Kesi hiyo ya mauaji namba 18/2019 inayosikilizwa na Hakimu Frola Kaijage katika Mahakama ya Wilaya Bukoba mkoani Kagera, bado inaendelea kutajwa ambapo Wakili wa Serikali, Juma Mahona alisema upelelezi unaendelea.

Watuhumiwa katika kesi hiyo ya mauaji ya mwanafunzi Mudy aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika shule hiyo ni wanafunzi Sharifu Amri (19), Fahadi Abdulazizi Kamaga (20), Husama Ramadhan (17), Sharifu Huled (19), Abdalah Juma (19) na Hussein Mussa (20).

Wengine ni Majaliwa Abud (35) ambaye ni mwalimu na mlinzi Badru Issa Tibagililwa (27).

Mauji hayo yalitokea Aprili 14, mwaka jana katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic iliyoko katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here