21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

 MAGUFULI ASHUSHA NYUNDO KWA VIGOGO

Na ANDREW MSECHU, DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli ameshusha nyundo kwa vigogo, huku akishangaa kuona mapato katika Jiji la Dar es Salaam yanashuka wakati mkuu wa mkoa aliyemtaja kama rais wa mkoa huo yupo.

Pia Rais Magufuli amesema kuna baadhi ya mawaziri ambao hawajui majukumu yao na kuwataka kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao ipasavyo.

Akizungumza jana baada ya kuwaapisha makatibu wakuu, manaibu katibu wakuu, wakuu wa mikoa na maofisa tawala mikoa, Rais Magufuli ameshangazwa kuona Dodoma yenye watu karibu milioni mbili kuongoza kwa makusanyo ya Sh bilioni 24.5, huku Dar es Salaam yenye zaidi ya watu milioni 5.5 ikikusanya kisi kisichofikia hata nusu ya mapato yaliyokusanywa na Dodoma.

“Juzi (Jumatatu) nilikuwa naongea na mabalozi, nikawaambia Dodoma ndiyo inaongoza katika majiji, manispaa, wilaya kwa Tanzania nzima, hivyo unaweza ukajiuliza kuna nini, unaweza ukajua hapa Dar es Salaam kuna upigaji na viongozi wapo.

“Unaweza kujiuliza Dodoma kuna nini, huyo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Katibu Tawala wa Dodoma, Meya wa Dodoma na wananchi wa Dodoma wana jinsi za namna gani ukilinganisha na Dar es Salaam yenye zaidi ya watu milioni 5.5 iliyokuwa na malengo ya kukusanya Sh bilioni 12 ambazo hazijafikiwa wakati Dodoma ikiwa imekusanya mara mbili zaidi ya malengo ya Dar es Salaam ikiwa na idadi ya watu milioni mbili,” alisema.

Alisema inaonekana Dar es Salaam kuna upigaji tena wa nguvu, lakini viongozi wapo na hata Manispaa ya Kinondoni aliyokuwa akiiongoza aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na kuapishwa jana, Ally Happi ilikuwa ya mwisho.

“Ilifikia wakati nikawa nafikiri sijui nitengue hapa hapa! Lakini aah, unaangalia labda kwa sababu ilikuwa chini ya upinzani. Hivi vitu vinatia aibu, kwanini katika majiji ambayo yako sita, Mbeya iwe jiji la mwisho, yaani jiji nililotangaza miezi mitatu iliyopita ndilo linaongoza, majiji yaliyotangulia yapo tu,” alisema.

Alisema wakuu wa mikoa ndio marais kwenye mikoa yao na hakuna mahali panapoweza kuwakwamisha, kwahiyo marais wa mikoa wakishindwa kusimamia mapato, ni wazi kwamba hawafai kwa sababu maisha ya nchi hii ni mapato na fedha zinazokusanywa ziende kwenye miradi ya maendeleo na Serikali haitakuwa tayari kukusanya fedha mahali pengine na kuyapelekea majiji yanayofanya uzembe.

Rais Magufuli alisema viongozi wa Dar es Salaam wakikutana kwenye vikao wanakaa siku moja au mbili, lakini zitajazwa posho za siku nne, hivyo kwa namna hiyo hawawezi kupata mapato kwa maendeleo ya wananchi.

“Utakuta hata wamachinga wanasimama barabarani hawana mahali pa kufanyia biashara, wakina mama wamedhulumiwa, lakini viongozi wapo, hivyo nataka niwaambie viongozi mlioteuliwa hakuna mwenye garantii ya kazi,” alisema Magufuli.

Aliwataka wateule wapya kujua wajibu wao na kwenda kushughulikia yanayowahusu kulingana na maelezo ya majukumu yao, si kusubiri rais aende kuwatekeleza majukumu yao akieleza kushangaa kuona wapo hata mawaziri ambao hawajui majukumu yao.

“Wakati mwingine kuna mambo ya kushangaza. Kulikuwa na mkubwa mmoja alifanya mambo ya hovyo tu katika wizara fulani, nikamuuliza waziri sitaki kumtaja, kwamba huyo mtu si yuko chini yako na amefanya ya hovyo? Akasema wa kutengua ni wewe, nikasema mimi rais?

“Nikamwambia hebu kasome sheria, mimi najua wa kutengua ni wewe waziri, nikamwambia ninakupa dakika 15 ukikuta mimi ndiye ninayestahili natengua na wewe nakutengua, lakini kama unaweza wewe katengue. Baada ya kama dakika kumi tu nikaona ameshatenguliwa, kumbe mamlaka ya kutengua ni ya huyo waziri,” alisema.

Alisema alikutana na hilo baada ya mmoja wa wasaidizi wake kufanya mambo ya hovyo hadi hata Sweden ikataka kuacha kutoa misaada kwa Tanzania kwa sababu ya mambo aliyoyafanya.

Aliwataka mawaziri wakafanye kazi, kila mmoja akaielewe wizara yake kwa kuwa anaona wapo watu ambao hawajazielewa vizuri wizara zao, hivyo wakafanye jitihada kuzielewa na wakayashughulikie yanayohusu wizara zao na wakayatatue.

Alisema agizo hilo linawahusu pia wote walioteuliwa na kuapishwa jana, akiwataka kila mmoja akatekeleze wajibu wake, japokuwa anajua watakutana na mambo ya ajabu yaliyofanyika, lakini wanatakiwa kuyatafutia suluhu.

Rais Magufuli alisema wateule wake wanatakiwa kutambua kwamba wamepewa dhamana na hakuna mwenye garantii ya kazi aliyopewa, kwa kuwa hata yeye hana garantii ya kuwa rais.

Alisema wakati mwingine amekuwa akipata tabu kwa sababu amekuwa akifanya kazi ngumu na siku nyingine akikosa usingizi usiku kucha akihangaikia majalada yanayoelekezwa kwake, ambayo yote yanatakiwa ayatolee uamuzi na kutoa suluhisho.

Rais Magufuli alisema kuna wakati mafaili mengine yamezagaa hadi chumbani na kwamba kazi za watu ni ngumu, hivyo iwapo watendaji wakuu wa wizara na mikoa wasipotekeleza wajibu wao lazima watapata malipo yao.

Pia aliwataka wakuu wa mikoa wakatoe ushirikiano kwa viongozi walioteuliwa maana wote ni vibarua wa Watanzania na kusisitiza kwamba wote walioteuliwa wanafanya kazi nzuri na kuwasihi wakaongeze bidii mara mbili zaidi kwa maendeleo ya nchi.

Alisema kuna maeneo utakuta mkuu wa mkoa haongei na katibu tawala wake, haongei na katibu tawala wilaya, haongei hata na watu wengine.

Akawataka viongozi hao wakawashirikishe watu, kwa kuwa wanahitaji kufanya kazi pamoja na watumishi watakaowakuta katika maeneo yao.

ILANI YA CCM

Rais Magufuli alisema wateule wote, hakuna atakayeweza kukwepa kutekeleza ilani ya CCM.

Alisema wapo watu wakishateuliwa wanakwenda kusemna wao ni watendaji wa Serikali, wakati aliyewateua ni kiongozi wa CCM.

“Mimi ni CCM, makamu wangu ni CCM, Waziri Mkuu CCM… Katibu Mkuu Kiongozi CCM, angekuja kiongozi kutoka chama kingine hapa hakuna mtu miongoni mwenu ambaye angeteuliwa hapa, kama wewe Happi angekuteua nani wakati ulikuwa unawatukana? Wangeweka watu wao kwa kadiri walivyokuwa wanawaona, hivyo kila mmoja anatakiwa akafanye kazi ya kutekeleza ilani hiyo,” alisema.

 ATETEA UTEUZI WA KAFULILA

Alisema wapo watu wanaosema kwamba amechagua wapinzani katika uteuzi wake, akihoji nani mpinzani Tanzania hii, huku akimtaja David Kafulila, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, ambaye alisema hawezi kuwa mpinzani.

“Alipokuwa huko alipigania suala la IPTL, nani angependea IPTL tulivyofanyiziwa, uwe CCM, CUF au uwe huna chama, suala la IPTL lilikuwa hovyo, lakini alisimama akapinga akaitwa tumbili, lakini hajageuka kuwa tumbili, bado ni yeye. Leo umteue useme umeteua mpinzani, huyu si mpinzani ni mtekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM,” alisema.

Alisema Katibu Tawala Mkoa aliyetoka chama kingine na kuingia CCM ni Kafulila pekee katika wote 13 aliowateua na kwa wakuu wa wilaya wako 31, lakini waliotoka chama kingine ni kama watatu na nusu, akimtaja wa Dodoma mjini, Longido ambaye ni Moses Machali na Bukombe ambaye ni Said Mkumba, ambaye alikuwa CCM na kuhamia upinzani kwa siku chache kisha kurudi CCM.

“Lakini mkiwa kwenye vita, mkateka vifaru na silaha kwani mnaviweka stoo, si unavigeuza kuwapigia hao hao? Hata ukiteka mateka kama mabrigedia jenerali kwani unakuja kuwaweka wakae wale chakula chako tu? Si unawageuza, tena unawapeleka kuwa chambo kuwapigia hao hao na unawapa na silaha,” alisema.

Alisema taifa linatakiwa kwenda mbele na yeyote anayeweza kushirikiana katika hilo anatakiwa ashirikishwe, ndiyo maana alimteua hata Kitila Mkumbo kutoka ACT-Wazalendo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kwa kuwa alitokea CCM ambako walimnyima nafasi kwenye UVCCM, hivyo kuamua kukimbilia upinzani, kwa kuwa hakuwa na sehemu nyingine ya kwenda.

 SAMIA SULUHU

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema kiapo hicho kina maana kubwa hasa katika kuwajibika, akieleza alivyoshuhudia mambo asiyoyatarajia katika ziara yake mikoani.

Alisema uhusiano wao na chama kinachotekeleza ilani ni suala la muhimu kuepusha migogoro kwa kuwa wameona mivutano baina ya watendaji wa Serikali na chama, hivyo wafanye kazi kwa kushirikiana na chama kinachosimamia ilani.

Rais Magufuli alisema katika halmashauri kuna mapato yanayostahili kukusanywa, lakini hayakusanywi ipasavyo, aidha kwa kutokujua, uzembe na wakati mwingine yanakusanywa kinyume na sheria, hivyo ni vyema wasimamie mapato na matumizi.

“Nimeshangaa kuona katika mikoa na halmashauri, mkurugenzi au anayemsaidia bado anafuja pesa mpaka leo, pamoja na maneno mengi tunayowaeleza. Ninashangaa kuona bado kuna wanaume huko chini wanafuja na wanaona wako mbali kufikiwa,” alisema.

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,654FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles